Esma vs Msizwa kama picha la Shilole

KIMENUKA! Hivyo ndivyo unavyoweza kusema, baada ya wanandoa Esma Platnumz na Msizwa kuamua kumwagiana mboga na ugali baada ya kuvunjika kwa ndoa yao miezi michache iliyopita.

Esma ambaye ni dada wa msanii maarufu nchini Diamond Platnumz, alimwaga mboga ikiwa ni siku mbili tangu mumewe, Msizwa kumwaga mboga kuhusiana na mgogoro ndani ya ndoa hiyo ambayo imekuwa ikifuatiliwa tangu walipofunga Juni, mwaka jana na kufuatiwa na bonge la sherehe.

Hata hivyo, ndoa hiyo ilidumu kwa miezi isiyozidi mitano kabla ya kuvunjika.

Akizungumza katika mahojiano na Zamaradi Tv, Esma aliweka hadharani kilichovunja ndoa yao huku akidai mwanaume huyo alienda kumuoa kwa ajili ya kutafuta umaarufu na kutaka biashara zake ziende.

Pia katika mahojiano hayo, Esma alienda mbali zaidi na kueleza kwamba mumewe ambaye lilikuwa chaguo la mama yake, awali alipokwenda kumchumbia alimweleza ni mtu mwenye hela, lakini alipoishi naye aligundua hana lolote ni mtu wa kawaida.

“Yaani nimeamini mwanaume yeyote akiwa anakutaka anaweza kukuigizia na usijue, kwani Msizwa alikuwa mtu ambaye alionyesha hapendi mambo ya mitandao ni mtu aliye busy na kutafuta hela, kumbe ndivyo sivyo,” alieleza Esma na kuongeza kuwa katika harusi yao aliolewa na mahari ya milioni mbili kati ya milioni tano ambazo mfanyabiashara huyo alitakiwa atoe.

“Pia alitaka kumtumia ndugu yangu Diamond na mama yangu katika kutangaza biashara zake, jambo ambalo nilikuwa mkali nalo na hivyo kuzua migogoro ya mara kwa mara.”

Aidha, alidai uharaka wa bwana huyo kutaka harusi ya harakaharaka ni moja ya mambo yaliyompa maswali mengi, lakini kwa kuwa alitaka kumridhisha mama ambaye alionekana kumpenda kaka huyo ilibidi akubali.

Wakati Esma akisema hivyo, Msizwa naye alisema Esma naye alikwenda kwake kimaslahi na mbaya zaidi anaona alichotarajia hajakipata ndio maana wameshindwana.

“Huyu alikuja kwangu kwa nia ya kuchuma pesa, lakini tulivyoishi akaona matarajio aliyoyategemea hajayaona na hivyo kuanza visa hadi kufikia hatua hiyo ya kutengana.


Shilole v Uchebe

Wakati Esma na Msizwa wakituhumiana kwa hayo, hata Shilole wakati ndoa yake ilipovunjika na Uchebe aliyaanika mengi ya mumewe huyo.

Shilole katika maelezo yake alisema Uchebe alikuwa anajificha nyuma ya mgongo wa dini, kumbe sivyo alivyo.