Dongo Janja kikaangoni

Dogo Janja ahojiwa polisi, adaiwa kushawishi abiria wasipime Covid-19

Muktasari:

Jeshi la Polisi Kikosi cha Viwanja vya Ndege nchini limesema linaendelea na uchunguzi ili kubaini kama tuhuma zinazomkabili msanii wa Bongofleva, Abdulaziz Chende (26) na wenzake wawili ni za jinai ili wafikishwe mahakamani.

Dar es Salaam. Jeshi la Polisi Kikosi cha Viwanja vya Ndege nchini limesema linaendelea na uchunguzi ili kubaini kama tuhuma zinazomkabili msanii wa Bongofleva, Abdulaziz Chende (26) na wenzake wawili ni za jinai ili wafikishwe mahakamani.

Kauli hiyo imetolewa leo Ijumaa Mei 7, 2021 na Kamanda wa kikosi cha Viwanja vya Ndege nchini, Jeremia Shila kuhusu kuhojiwa na kuachiwa kwa msanii huyo na wenzake kwa tuhuma za kuwashawishi abiria kutopima maambukizi ya ugonjwa wa Covid-19 mara baada ya kuwasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa mwongozo uliotolewa na Serikali, wenyeji wanaorejea na wageni kutoka nje wanatakiwa kuwasilisha kipimo kinachothibitisha hawana maambukizi ya Covid-19, huku wanaotoka nchi zenye maambukizi wakitakiwa kupimwa kwa kipimo maalum ambacho kitagharimu Dola 25 za Marekani, sawa na Sh57,500 kwa kila msafiri.

Inadaiwa kuwa Dongo Janja aliyekuwa akitokea Afrika Kusini alipinga kufanya kipimo hicho ambapo kupitia ukurasa wake wa Twitter ameandika, “hii nchi Tanzania bado ina uonevu wa kishamba sana, sidhani kama mama yetu Rais Samia Suluhu  anafahamu.. muda huu nafika uwanja wa ndege wa kimataifa nikitokea Afrika Kusini na Afrika Kusini huko  nimepima na nina majibu ya  corona lakini hawayataki wanataka hela kutupima upya.”

“Sasa ndugu zangu wa Tanzania mimi nina hela lakini sitoi hata kumi..., mniletee uji kituo nitakachokuwepo nikikosekana hewani shughulikeni na Polisi wa uwanja wa ndege.”

Katika maelezo yake Shila amesema jana Alhamisi Mei 6, 2021  saa 10 jioni polisi katika uwanja huo waliwahoji watatu hao waliokuwa wakitokea nchi mbalimbali kwa tuhuma za kuwashawishi abiria wengine kukataa kufanyiwa kipimo na kulipia kiasi hicho cha fedha.


Mbali na Dogo Janja wengine waliohojiwa ni Shaeb Hamad (43) na Sylvia  Kisamo(30) .