Dk Abbas: Marufuku kuwafungia wasanii nyimbo, filamu bila kuwaita

Dk Abbas: Marufuku kuwafungia wasanii nyimbo, filamu bila kuwaita

Muktasari:

  • Badala yake ametaka wasanii hao wawe wanaitwa kwanza na kuelezwa kosa lao kwa kuwa lengo ni kuwasaidia lakini na sio kuwaadhibu.

KATIBU Mkuu wa Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dk Hassan Abbas, ametaka wasanii wasifungiwe hovyo nyimbo na filamu zao bila kushirikishwa.

Badala yake ametaka wasanii hao wawe wanaitwa kwanza na kuelezwa kosa lao kwa kuwa lengo ni kuwasaidia lakini na sio kuwaadhibu.

Dk Abbas ameyasema hayo leo Jumatano Desemba 2,2020 alipokutana na wasanii wa filamu na sanaa za maonyesho katika kikao cha mazungumzo kati yao na serikali, kikao ambacho kilihudhuriwa na Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa (Basata), Godfrey Mngereza na Katibu Mtendaji Bodi ya Filamu, Dk Kiagho Kilonzo.

Katibu huyo ambaye pia ni msemaji wa serikali, alisema katika serikali hii wasingependa kuona wasanii wakifungiwa hovyo kazi zao bila kushirikishwa.

"Wasanii ni watu wakubwa, wasichukuliwe poa ikiwemo kuwafungia hovyo kazi zao bila kuwataarifu, watu wameingia lokesheni wametumia gharama kubwa kuzitengeneza, halafu unaamka asubuhi unaita waandishi unatangaza umeifungia kazi fulani, hii haikubaliki," amesema.

Katika kulifanya jambo hili vizuri Dk Abbas amesema ni vyema ukamuita kwa utaratibu msanii husika, ukampatia hata chai, chapati na juisi, kisha mkazungumza taratibu na kumuelewesha kosa lake kisha mwisho wa siku mnaweza kuipangia kazi daraja ya kutazamwa muda gani.

Akizungumzia kuhusu kikao hicho, Dk Abbas amesema ni katika kupata maoni kutoka kwa wasanii hao kuangalia namna gani ya kukuza sekta hiyo ya filamu ili iweze kusonga mbele.

Pia kuikuza na kuwa kama nchi nyingine ikiwemo Marekani, India na Nigeria na kuwaelekeza kufikisha malalamiko yao sehemu husika badala ya kupitia watu ambao hawana msaada nao zaidi ya kutumika kama wapambe.

Kwa upande wa wasanii wamesema ipo haja ya mashirikisho kupewa meno na kusikilizwa badala ya sasa hivi ambapo mengi yao yapo tu na kutokuwa na msaada na wasanii na baadhi ya  viongozi wake wengine kuwa kisiasa zaidi na kwa maslahi yao wenyewe.

Sanday Temba amesema ipo haja ya wasanii kupewa elimu ya mara kwa mara ikiwemo namna ya kuishi kistaa, kujieleza mbele za watu na kujua nini unapaswa kujibu na kutojibu kwa umma.

............................

Na Nasra Abdallah