DIDI STONE: Binti wa Koffi Olomide mwenye nyota zake

Muktasari:
- Kati ya hayo, ni kuzaliwa kwa mtoto wao wa kwanza, Didi Stone, 24, binti mrembo ambaye amegeuka lulu katika ulimwengu wa mitindo barani Afrika na Ulaya huku akiwa na ushawishi katika mitandao ya kijamii.
NDOA ya tatu ya gwiji wa muziki Afrika kutokea DR Congo, Koffi Olomide na mwanamitindo wa zamani wa Ufaransa, Aliane ambayo ilifungwa huko Paris hapo Aprili 1994, ina mengi mazuri tunayoweza kusimulia kwa umahiri.
Kati ya hayo, ni kuzaliwa kwa mtoto wao wa kwanza, Didi Stone, 24, binti mrembo ambaye amegeuka lulu katika ulimwengu wa mitindo barani Afrika na Ulaya huku akiwa na ushawishi katika mitandao ya kijamii.
Kwa ujumla ndoa hiyo ilijaliwa watoto wawili, mwingine ni Del Pirlo na kumfanya Koffi kuwa na jumla ya watoto saba wanaotambulika ukijumlisha na wengine watano aliowapata katika ndoa zake mbili za awali na Marianne na Stephanie.

Hata hivyo, baada ya miaka 27 ya kuwa pamoja, Aliane aliwasilisha kesi ya talaka mahakamani na kufikia 2022 wakatalikiana, Koffi alikuwa akituhumiwa kuwa na uhusiano nje ya ndoa na mwimbaji wa bendi yake Le Coeur tangu 2013.
Hiyo ni simulizi nyingine ya familia yao ila kwa leo tukamtazame binti yao, Didi Stone ambaye alizaliwa Julai 17, 1999 huko, Marseille, jiji la tatu kwa ukubwa na umaarufu nchini Ufaransa baada ya Paris na Lyon.
Didi na mdogo wake Del Pirlo walikulia Ufaransa na DR Congo ambako waliishi na ndugu zao wengine wa kambo ambao ni Aristotle na Minou, hawa ni watoto wa Marianne, pia walikuwepo Rocky, Diego na Karine ambao ni watoto Stephanie.

Baada ya masomo ya sekondari, Didi alijiunga na chuo cha biashara, EBS Paris - European Business School ili kusomea biashara na mitindo ambapo mwaka 2021 alihitimu ngazi ya shahada ya kwanza.
Tangu akiwa mdogo alionyesha nia ya kufuata nyayo za mama yake Aliane upande wa mitindo na alipofikisha umri wa miaka 15 tu mawakala mbalimbali wa mitindo kimataifa walianza kupigania saini yake.
Kwa mara ya kwanza alisainiwa na Next Management, Metropolitan Models Group kisha baadaye akachukuliwa na Elite Modeling Management, mawakala wote hawa waliisimamia chapa ya Didi na kuikuza vizuri kama mwanamitindo anayechipukia.

Akiwa na umri wa miaka 16, Didi alitokea katika jarida la Vogue na tangu wakati huo ameonekana na kuhojiwa na majarida makubwa ya mitindo na maisha kama vile Vanity Fair, Paris Match, Grazia, The New York Times, Forbes n.k.
Machi 2016, Didi akizungumza na Vogue alisema baba yake Koffi amekuwa akimfundisha jinsi ya kuvaa kwa kuzingatia asili yao ya miaka mingi kutoka DR Congo kitu ambacho kimemjenga kama mwanamitindo.
"Baba yangu ni Mkongo, utamaduni wao ni kuvaa kila wakati kwa njia bora zaidi, umaridadi na ustaarabu. Kwa hiyo, siku zote baba yangu hunifundisha jinsi ya kuvaa vizuri na kutunza sura yangu," alisema Didi.

Hadi sasa amejizolea umaarufu na wafuasi wengi kutokana na utamaduni wake kuchapisha maudhui ya mitindo, safari na mitindo ya maisha ya kila siku katika mitandao ya TikTok na Instagram ambako ana wafuasi zaidi ya milioni 2.
Katika mahojiano yake na Forbes yaliyochapishwa Agosti 2, 2023, Didi alizungumzia safari yake ya mitindo na kusema hakupendezwa na baadhi ya mawakala waliosema ana uzito uliozidi wakati huo akiwa na miaka 15 pekee.
Hata hivyo, kigezo cha uzito hakukiona kama changamoto ya kumzuia kusonga mbele, hivyo aliamua kuvunja baadhi ya kanuni za kimitindo kama anavyofanya Rihanna ili tu kufikia lengo lake.
"Hii ndio sababu nampenda Rihanna, ananihamasisha kwa asilimia 100 na kunitia moyo sana. Yeye ni mwanamke anayepindua kanuni, haogopi watu wanavyomfikiria. Nilipata nafasi ya kukutana naye na kuzungumza naye, ni baada ya kupiga picha kwa ajili ya chapa zake za Fenty Beauty na Fenty Skin," alisema.
Didi alisema mara zote mwazoni alipopata changamoto katika kazi yake kama kutokukubalika na kutupiwa maneno ya kashfa katika mitandao, alikuwa anakumbuka ushauri aliopewa na wazazi wake.

"Baba yangu aliniambia kila mara kuwa 'hakuna kitu kizuri ambacho ni rahisi', na mama aliniambia 'kila kitu kinapita', ni maneno ambayo yaliambatana nami katika nyakati zote ngumu na kunisukuma kushinda," alisema Didi.
Machi 2020 alichaguliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa Linalohudumia Watoto (UNICEF) kuwa balozi wa kupinga unyanyasaji kwa wasichana hasa ndoa za utotoni huko DR Congo, kazi aliyoifanya kwa mikono miwili.
"Siku zote nimekuwa nikifanya shughuli za kibinadamu Congo, huenda huko kuwaona watoto na kuzungumza nao. Tunajua nchini humo kuwa mwanamke mmoja kati ya watatu huolewa kabla ya umri wa miaka 18," alisema na kuongeza:
"Vita dhidi ya aina zote za ukatili dhidi ya wanawake na wasichana ikiwa ni pamoja na ndoa za utotoni, ndilo lengu kuu. Ni muhimu kuhimiza upatikanaji wa elimu hasa katika kuzuia ndoa za kulazimishwa," Didi aliliambia jarida la Forbes.
Na kwa mujibu wa Stark Times na TG Time, utajiri wa Didi unakadiriwa kuwa kati ya Dola 3 milioni hadi Dola 3.25 milioni kwa mwaka 2024, huku sehemu kubwa ya utajiri wake ikitokana na kazi yake ya mitindo, ushawishi katika mitando na balozi wa chapa kubwa.