Diamond na rekodi zake katika uchawi wa namba - 3

Diamond na rekodi zake katika uchawi wa namba - 3

Summary

  • Kwa kipindi cha zaidi ya miaka 12 katika muziki, Diamond ameweza kutoa albamu tatu, Kamwambie (2010), Lala Salama (2012), A Boy From Tandale (2018), pamoja na Extended Playlist (EP) moja, First of All (FOA) (2022) yenye nyimbo 10.

TOLEO lililopita tuliangazia wasanii wa DR Congo na Nigeria walivyofanikisha Diamond Platnumz kuandika rekodi ya kuwa na video nne zenye views zaidi ya milioni 100 YouTube na kumfanya kuwa msanii pekee Afrika Mashariki mwenye rekodi hiyo. Leo tunatazama upande mwingine. Endelea...!

Kwa kipindi cha zaidi ya miaka 12 katika muziki, Diamond ameweza kutoa albamu tatu, Kamwambie (2010), Lala Salama (2012), A Boy From Tandale (2018), pamoja na Extended Playlist (EP) moja, First of All (FOA) (2022) yenye nyimbo 10.

Albamu yake ya tatu, A Boy From Tandale ndio albamu namba moja ya Bongofleva iliyosikilizwa zaidi (most streamed) kwenye mtandao wa Spotify ikiwa na streams zaidi ya milioni 30 tangu itoke Machi 14, 2018.

Kwa mujibu calcutor ya tovuti ya Dittomusic.com, streams milioni 1 katika mtandao wa Spotify ni sawa na Dola4,370, wastani wa Tsh10.1 milioni, hivyo katengeneza kiasi kikubwa cha fedha kupitia albamu huyo. Kwa ujumla, Diamond ana streams zaidi ya milioni 175 Spotify.

Ikumbukwe baada ya video ya wimbo wake, Waah! kufikisha views milioni 100 YouTube, Diamond alisema ameingiza zaidi ya Euro80,665, wastani wa Tsh192.3 milioni, na kumbuka ana jumla ya views bilioni 1.9 YouTube.

Upande wa Boomplay Music ana streams zaidi ya milioni 170 akiwa ndiye anaongoza Tanzania na Afrika Mashariki, EP yake ya kwanza, First of All (FOA) imefikisha streams milioni 66.1.

Anafuatiwa na wasanii ambao kawatoa yeye chini ya WCB Wasafi ambao ni Rayvanny, streams milioni 138.4, kisha Zuchu, streams milioni 95.4, huyu anatarajiwa kuwa msanii wa kwanza wa kike Afrika Mashariki kufikisha streams milioni 100 (Golden Club) Boomplay.

Ikumbukwe katika mtandao huo Zuchu ana nyimbo nne zenye streams zaidi ya milioni 10 sawa na Diamond Platnumz, anafuatiwa na Jovial (Kenya) mwenye tatu, kisha Rayvanyy na Otile Brown (Kenya) ambao wote wana mbili.

Mwaka 2018 Diamond alitambulika kama msanii wa kwanza nchini Tanzania kumiliki vyombo vya habari baada ya kuanzisha Wasafi Radio na TV, anatajwa kuwa msanii wa pili barani Afrika kufanya hivyo baada ya Youssou N’Dour wa Senegal.

Diamond ndiye msanii wa kwanza Tanzania kununua gari la kifahari aina Rolls-Royce Cullinan ambalo ametaja bei yake ni Tsh2.2 bilioni, huku akidai kuililipia ushuru wa takribabi Tsh700 milioni.

Staa huyu anaungana na mastaa wengine wa Afrika kama Burna Boy, D’Banj, Phyno, Mr. P, J Martins, DJ Cuppy na Davido kumiliki Rolls-Royce, gari linalotengenzwa na Kampuni ya Rolls-Royce Holdings iliyoanzishwa mwaka 1904 huko Manchester, England.

Jarida la Forbes limeripoti kuwa, kampuni Rolls-Royce Holdings yenye Makao Makuu London ambayo kwa sasa ipo chini ya Mkurugenzi Mtendaji, Warren Authur East, imeajiri watu 48,200, na kufikia mauzo ya Dola 15.1 bilioni zaidi ya Tsh34 trilioni.

Ikumbukwe utajiri wa Diamond unakadiriwa ni Dola 10 milioni, wastani wa Sh23.3 bilioni baada ya mwaka jana kuikataa ripoti iliyotolewa na moja ya Blog nchini Nigeria na kutaja utajiri wake ni Dola5 milioni, wastani wa Tsh11.6 bilioni.

Hadi kufikia mwaka 2017 Diamond Platnumz alitangaza kutoza Tsh100 milioni kwa shoo, jambo hilo lililosababisha kutofanya shoo nyingi Tanzania, huku mapromota wa ndani wakimlalamikia fedha hizo ni nyingi sana.

Julai 2021 Meneja wa Diamond na WCB Wasafi kwa ujumla, Sallam SK alitangaza kuwa Diamond anatoza Dola70,000, wastani wa Sh163. 2.5 milioni kwa shoo za nje ambazo ndizo hasa msanii huyo amekuwa akizifanya mara nyingi.

Utakumbuka kwa mujibu wa WCB Wasafi, malipo ya Zuchu kwa shoo za nje ni Dola20,000, wastani wa Sh46.3 milioni, huku shoo za ndani ikiwa ni Dola 15,000 kama Sh34.8 milioni.

Akiongea na kipindi cha The Switch cha Wasafi FM, Januari 2021, Diamond alidai kwa mwezi anapokea Sh200 milioni kutokana na dili zake za ubalozi kutoka kwa kampuni mbalimbali, hiyo ni sawa na Sh55 milioni kwa wiki, Sh7 milioni kwa siku, Sh300,000 kwa saa na Sh6,000 kwa sekunde! Alieleza.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram Diamond aliweka wazi kuwa cheni anazovaa zinagharimu Dola177,000 wastani wa Sh422.0 milioni, pete zinagharimu Dola100,000, wastani wa Sh238.4 milioni, hivyo cheni na pete ni jumla ya Dola 277,000, wastani wa Sh645.7 milioni.

Na umaarufu wa kazi zake umemfanya Diamond kujizolea mamilioni ya wafuasi (followers) katika mitandao ya kijamii, ndiye msanii namba moja Tanzania na Afrika Mashariki upande huo katika mitandao minne mikubwa duniani, Instagram ana followers milioni 15.4, Facebook milioni 6.8, TikTok milioni 1.7 na Twitter milioni 1.1. Anayemkaribia kwa ushawishi kwenye mitandao ni mzazi mwenzie, Zari The Bosslady aliyemzalia watoto wawili, Tiffah na Nillan.