Diamond: Ibra na Angela wa Konde Gang ni wajukuu zangu

Msanii Diamond Platnumz, amesema wasanii kutoka Konde Gang, Ibra na Angela ni wajukuu zake.
Diamond aliyasema hayo katika mahojiano na shirika la habari la Uingereza (BBC) ikiwa ni moja ya ziara yake katika kutangaza EP yake ya First if All (FOA) aliyoiachia Machi, 2022.
Katika mahojiano hayo, moja ya swali aliloulizwa ni kuhusu uhusiano wake na msanii Harmonize ulivyokuwa huko nyuma na ulivyo kwa sasa na kama anadhani wangekuja kuwa na tofauti.
“Mimi unajua napinga sana mikwaruzano na migongano kwa sababu mimi binafsi hainisadii, furaha yangu ni kuona kesho mtu anasema sababu ya Diamond nimekuwa mtu fulani au nimekuwa hapa au nimefanikiwa kwa sababu ya Diamond' Alisema Diamond na kuongeza;.
“Sio tu Harmonize, pengine kesho kutakuwa na wasanii wengine atatoka kutoka wasafi atakwenda kujitegemea iwe positive sio kwa ubaya mimi ndio kitu ninachokitarajia, iweje sasa iwe vita kwani vita itatusaidia nini haitusaidii kitu”.
“Leo unaona kuna watu kama wakina Ibra, Angela hao wote ukiangalia sasa hivi ni kama wajukuu zangu mimi kimuziki".
“Hivyo nafurahi kuona kuwa nimemtoa mtu kaenda kuwatoa watu na ninaamini atawashika wengine,” amesema Diamond.