Diamond, familia yake wanavyokata kiu za mashabiki wa kisasa

Wiki hii hakuna msanii atakayetoa wimbo utakaobamba kiasi cha kuipita stori ya mama Dangote kusema mzee Abdul sio baba mzazi wa Diamond. Narudia, hakuna hata ukiwa ni wimbo mzuri kama Iokote wa Maua Sama au Muziki wa Darassa.

Na hii sio kwa sababu eti stori hiyo inamhusu msanii mkubwa Tanzania, Diamond, hapana, bali ni kwa sababu stori hiyo imekuja kipindi ambacho watu wanahusudu maisha ya wasanii kuliko sanaa zao.

Kama huamini nakukumbusha hivi, wiki hii Nandy katoa bonge la ngoma na Joe Boy wa Nigeria, Chege kaachia EP, Ibrah wa Konde Boy naye ana EP yake tena kamshirikisha mpaka Skales na Lamata katoa bonge moja la tamthilia la kuitwa Jua Kali na vyote hivyo vinapatikana bure YouTube bila malipo (isipokuwa tamthhilia ya Jua Kali). Lakini ukienda YouTube leo hii usishangae kukuta kinachotrendi ni habari ya Daimond na baba zake badala ya miziki mizuri.

Labda Diamond anafahamu hili, labda alikuwa anatamani kila kitu kitokee namna hii na kwa sababu Mungu anasikilikiza vitu vinatokea kama alivyotamani.

Alipoanza muziki alikuwepo yeye na wasanii wengine wengi. Lakini wakati wenzake wanahangaika kuandika ngoma kali yeye alihangaika kuandika ngoma kali na kumtongoza Wema Sepetu.

Matokeo yake ni nini? Matokeo yake akawa msanii mwenye ngoma kali lakini pia mpenzi wa muigizaji maarufu zaidi Tanzania.

Kisha penzi lao likajaa drama, ikawa hata Diamond asipotoa wimbo miezi sita lakini drama zake na Wema Sepetu zinafanya aongelewe ile mbaya mitaani na kwenye kila chombo cha habari.

Hivyo ndivyo dunia ya sasa inavyotaka, uwe muigizaji mzuri wa filamu lakini maisha yako yawe na chumvichumvi, visavisa na vimbwanga. Uwe mwanamuziki mzuri lakini pia familia yako iwe na mazengwezengwe.

Familia ya Kardashian wanaishi hivyo, hawaimbi, hawaigizi kwenye filamu, lakini umaarufu wao mkubwa unatokana na mikasa ya familia yao. Na kitu kizuri ni kwamba kwa mikasa hiyohiyo wametengeneza mpaka mabilionea.

Hawafanyi sanaa yoyote ya kueleweka lakini ukiamka utasikia baba yao kabadilisha jinsia kuwa mwanamke. Utasikia mama yao anatembea na kijana mdogo umri sawa na mtoto wake wa mwisho. Hujakaa sawa utasikia huyu kaolewa na Kanye West, na sasa wanadaiana talaka kwa nguvu, na kweli wanatrendi hivyo.

Dunia nzima sasa hivi mashabiki ni walevi wa skendo kuliko kazi za sanaa. Hii ni kwa sababu mitandao ya kijamii inahitaji stori za kuzungumzwa, kwa hiyo watu wanajikuta tu wanatafuta stori za wasanii kuziongelea.

Nina uhakika Diamond na familia yake wanajua hilo ndiyo maana tangu imekuwa maarufu haiwajahi kutupumzisha hata mwezi. Yaani kila mwezi lazima kuwe na jambo kubwa wamefanya.