CPwaa 'King of Bongo Crank' afariki dunia

Msanii wa muziki wa kizazi kipya kutoka Tanzania, Ilunga Khalifa maarufu Cpwaa amefariki dunia usiku wa kuamka leo Januari 17.

Kifo cha Cpwaa ambaye enzi za uhai wake alitamba kupitia kundi la Park Lane na nyimbo zake binafsi kama Action aliomshirikisha Dully Sykes, marehemu Ngwair na msanii kutoka Jamaica Ms.Triniti kimetokea hospitali ya Muhimbili ambapo alilazwa kwa siku nne.

Akizungumza na Mwanaspoti muaandaji wa muziki P Funk Majani ambaye alikuwa mtu wa karibu wa msanii huyo ikiwa ni pamoja na kufanya naye kazi na hata kipindi cha ugonjwa wake amethibitisha msiba huo, hata hivyo amegoma kuweka wazi chanzo cha kifo cha Cpwaa.

"Ni kweli amefariki lakini mengine mtayafahamu zaidi kutoka kwenye familia baadae," amesema Majani.

Cpwaa atakumbukwa kama moja ya wasanii waliwekeza katika kufanya mapinduzi kwenye upande wa video za muziki kwani video za nyimbo zake kama Problems, Action na Mhhh! zinatajwa kuwa moja ya video za muziki za mwanzoni zenye ubora kutoka Tanzania. Na zaidi ziliwahi kumpa tuzo mfulilizo za Kilimanjaro Tanzania Music Award mwaka 2010 na 2011 kama video bora za mwaka.

Aidha wasanii wengi wameoneshwa kugusa kwa msiba huo na wametoa heshima zao kupitia 'kupost' picha zake kwenye mitadano ya kijamii.

Kupitia akaunti zao Instagram za wasanii Shilole, Adili, waandaji wa muziki Marco Chali, J Murder na wengine wote wameachia ujumbe w wa kuonesha kuguswa na msiba huo.

Aliyekuwa msanii mwenzake, Suma Lee ameandika kwenye ukurasa wake wa Instagram kuwa msiba upo Magomeni Mikumi na atazikwa leo saa 10 jioni.

Taarifa zaidi kuhusu msiba huu zitakujia hivi karibuni kwenye mitandao yetu...