Chungu tamu miaka 23 ya JB kwenye Filamu

Monday October 25 2021
jb pic
By Charity James

UKIAMBIWA utaje waigizaji maarufu na bora kwenye tasnia ya filamu za kibongo huwezi kuacha kutaja jina la Jacob Steven (JB) kutokana na ubora wa kazi zake.

Ni bora na ni bora tena. Amekuwa mwigizaji ambaye mara nyingi anaigiza uhalisia wa maisha ya wabongo. Mkongwe huyo aliyeigiza kwa miaka 23 ametangaza kutundika daluga kutokana na kuridhika na alichokifanya.

“Nimefanya kazi ya uigizaji miaka 23 ni umri wa mtu mzima. Naomba kupumzika sasa kuigiza nitakuwa nyuma ya kamera kufanya kazi nyingine inayohusiana na tasnia hiyo kama mwongozaji na si muigizaji,” anasema.

Mwanaspoti linakuletea makala ya nyota huyo aliyefunguka mambo mbalimbali huku akilizwa na Riyama Ally kwa kukosa nafasi ya kuigiza naye akimtaja kuwa ni msanii bora.


RIYAMA AMTESA

Advertisement

Siku chache baada ya kutangaza kustaafu kuigiza, JB alisema ameumizwa kukosa nafasi ya kuigiza na mwanadada anayefanya vizuri kwenye tasnia hiyo, Riyama Ally.

“Huwa napenda sana sana kuigiza na waigizaji wanaojua kuigiza. Napendelea zaidi kuwaita mafundi. Kuna mafundi wachache sikupata bahati ya kuigiza nao, lakini Riyama ameniuma zaidi. Yupo kwenye wanawake watano bora wanaojua kufanya kazi hii. Huyo pamoja na kumkosa yupo kwenye nyota wa muda wote,” anasema JB.


MTAJI MDOGO

JB hajawahi kufanya kazi mbovu, lakini akikueleza mtaji alioanza nao utashangaa, kwani Sh1.5 milioni aliyochanga na mwenzake akatoa kiasi kama hicho ndiyo iliyomfikisha alipo.

“Sikuwa nazo, kwani ndio kwanza nilikuwa natoka kufilisika kwenye biashara ya uuzaji wa sembe. Rafiki yangu Hayati Mpakanjia alinipa pesa kiasi nilichotakiwa kuchanga huku akisema anaamini ninaweza, baadae Mjomba Fujo aliacha uigizaji nikabaki mwenyewe, lakini bado alikuwa akitoa nyumba yake, magari na hakukosa kuhudhuria ‘shooting’ zetu huku akinipa moyo. Moja ya watu ambao ningependa waone nilipofika ila Mungu alimpenda zaidi,” anasema.


FILAMU YAKE BORA

Mzee wa Swagga ni filamu ambayo kwa upande wa JB anataja kuwa ni bora huku akiweka wazi kuwa anaamini tangu ameanza kuigiza hiyo ndiyo bora, huku akitaja nyingine tano ambazo ndizo zimekuwa bora kwa mashabiki wake.

“Hadi nasimama kuigiza filamu Mzee wa Swagga ndio bora kwangu ingawa kupitia maoni ya wadau na mashabiki zangu DJ Ben ndio iliongoza ilifuatiwa na Senior Bachelor,” anasema.

“Filamu zangu tano bora ni 14 days, Nakwenda kwa Mwanangu, Regina, Senior Bachelor na Mzee wa Swagga, kitu kimoja kinachonifurahisha kwenye hili karibu kila mtu namba moja yake ni tofauti na mwenzake.”


ZILIZOMPA TUZO

JB anataja filamu tatu ambazo zilimpa tuzo za mwigizaji bora na mwaka aliopata tuzo ya kwanza kuwa ni 2008 kwenye Ukumbi wa Diamond Jubilee. “Tuzo zilikuwa zinaitwa Vinara Awards nilishinda tuzo ya mwigizaji bora wa mwaka kupitia The Stranger 2011 pale Zanzibar kupitia tamasha la Zanzibar International Film Festival (Ziff) nilishinda tena Best Actor kupitia Senior Bachelor 2013 nilishinda Best Actor kupitia Shikamoo Mzee,( Steps Awards),” anasema.

“Filamu ya Shikamoo Mzee ilishinda tena tuzo ya Movie bora ya mwaka ZIFF Awards pale Zanzibar, filamu yangu ya Mikono Salama iliwahi pia kutoa Best Actress wa mwaka (Mh Jokate Mwengelo) kwenye Ziff Awards pale Zanzibar.”


FILAMU ILIYOMPA ULAJI

Wakati wasanii wa filamu wakiendelea kulia kudhurumiwa mkongwe huyo anaweka wazi kuwa anataja filamu iliyomuingizia pesa nyingi kuwa ni Hukumu ya Ndoa Yangu.

“Filamu yangu ya Hukumu ya Ndoa Yangu ndiyo niliyouza kwa bei kubwa zaidi kuliko zote ikifuatiwa na Mikono Salama, sababu ni kuwa Hukumu ya Ndoa Yangu ilikuwa na sehemu tatu na Mikono Salama ilikusanya mastaa wengi. Hata hivyo Mikono Salama ilishinda tuzo ya Best Actress (Ziff Awards) kupitia Main Actress wa sinema hiyo Jokate,” anasema. “Pia ndiyo filamu yangu ya kwanza kutumia HD toka kwenye mfumo wa DIV, mageuzi haya yalisaidia bei kupanda.”


ALIYEMFANYA AIGIZE

Akizungumza kwa nini aliiingia kwenye uigizaji, JB anasema: “Nakumbuka mwaka 1997/98 nikiwa Dodoma Hoteli Inn nilikuwa nasubiri malori ili nikapakie mzigo wangu Kibaigwa kuangalia kwenye TV nikamuona Single Mtambalike nikashangaa vipi huyu nilivyofuatilia nikagundua ni igizo.

“Niliporudi Dar es Salaam siku moja tukakutana wote tulikuwa maskani yetu Sinza Mori aliponiona tu aliniambia eeh nilikuwa nakutafuta tukaigize nikamwambia sifanyi utoto huo. Baada ya kunibembeleza sana nikakubali wakati huo nilikuwa ‘check bob’ halafu na hela za mahindi.

“Nikawa nawasumbua sana wananifuata na basi la ‘shooting’ la ITV hadi Manzese mashine halafu wanirudishe Mori kuchukua nguo. Kiukweli nilikuwa sitaki nilifanya sanaa kumridhisha Rich,” anasema na kutaja mchezo wake wa kwanza ni ‘Kuvuja kwa Mitihani.

Advertisement