Chuchu Hans: Alichofanya Shilole ni kupokezana vijiti

Chuchu Hans: Alichofanya Shilole ni kupokezana vijiti

Muktasari:

  • Ronze alisainiwa rasmi Shishi Gang Novemba 26, 2020 na kutambulishwa mbele ya waandishi wa habari, ambapo anakuwa msanii wa kwanza kusainiwa katika lebo hiyo.

Zikiwa zimepita siku tano tangu msanii Ronze asajiliwe  kwenye lebo ya Shishi Gang, Chuchu Hans afunguka.

Kabla ya kujiunga na Shishi Gang, lebo inayomilikiwa na msanii Shilole, Ronze ambaye jina lake halisi ni Rajah Mkufya , alikuwa akisimamiwa kazi zake  na Chuchu ambaye ni  msanii wa filamu nchini Tanzania.

Ronze alisainiwa rasmi Novemba 26, 2020 na kutambulishwa mbele ya waandishi wa habari ambapo Shilole alisema mpaka wamemsajili wamejiridhisha kuwa ana kipaji ambapo anakuwa msanii wa kwanza kusajiliwa katika lebo hiyo mpya nchini.

Akizungumzia hatua hiyo, leo Jumatano Desemba 2, 2020 Chuchu katika mahojiano yake na Mwanaspoti Digital, amesema kwake ni faraja kwa kuwa tangu awali wakati anamsimamia msanii huyo malengo yake ilikuwa afike mbali kimuziki na sasa anaona dalili za ndoto hizo kutimia.

Amefafanua kwamba kitendo cha Shilole kumchukua msanii huyo kitampa faida nyingi ikiwemo kukutana na wasanii mbalimbali wakubwa ambao Shishi ana koneksheni nao.

“Shishi anajuana na wasanii wakubwa, na ndio maana akiwa bado mgeni, wiki iliyopita Ronze aliweza kupanda jukwaa la wasafi mkoani Shinyanga, jambo ambalo wasanii wengi wanalitamani hata wale waliomtangulia katika muziki muda mrefu,”amesema Chuchu.

Mbali na hilo, Chuchu  amesema sasa msanii huyo katua katika mikono ambayo angestahili kuwa ya wanamuziki wenzake, tofauti na yeye ambaye anafanya kazi za filamu ambazo wakati mwingine zinamuweka busy kwa kuwa zinahitaji muda mwingi kuziandaa.

Alipoulizwa kama wana mawasiliano mazuri na msanii huyo baada ya kujiondoa kwake, mcheza filamu huyo amesema wapo vizuri hata juzi walizungumza na kuongeza kwamba hakuna ugomvi wala tofauti yoyote baina yao na kuahidi kuendelea kumsaidia pale atakapomuhitaji kama jambo lenyewe litakuwa ndani ya uwezo wake.

Mpaka anatua Shishi Gang, Ronze tayari alishaachia vibao mbalimbali ikiwemo  Sawa, Chereko, Nikokote, Huruma na Alivyo.

...........................................

Na Nasra Abdallah