Bei elekezi uuzaji filamu yaja

Katika kuhakikisha wasanii wa filamu wanafaidika na jasho lao, Serikali ipo katika mpango wa kuja na bei elekezi ya kuuza kazi hizo.
Hayo yamesema jana Jumapili Mei 9, 2021 na Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania, Dk Kiagho Kilonzo katika hafla ya uzinduzi wa tamthilia ya ‘We Men’.
Dk Kilonzo amesema wamekuja na wazo hilo baada ya muda mrefu wasanii hao kila mmoja kuwalipa anavyojisikia, ambapo malipo mengine hayaendani na kazi husika.
“Ifike mahali wasanii wetu wafaidike na jasho la kazi zao, kwani kuna watu wanawalipa hela ambayo ukipiga gharama za uandaaji wa filamu hazifiki hata robo, kama serikali tumeona hili halikubaliki na sasa tunakuja na bei elekezi ambayo haitaumiza upande wowote,” amesema Katibu huyo.
Akielezea hali ilivyo ya sasa katika tasnia hiyo, amesema wadau wa filamu wamekuwa matarajio makubwa kuliko hali halisi ilivyo hasa kwenye masoko na mahitaji.

Ni kutokana na hilo , wameona kuna haja ya kuboresha maisha ya wadau hawa kwa kuboresha masoko na kuimarisha vyama vyao ambapo tayari viashiria vya kuelekea huko vimeanza kuonekana.

Moja ya viashiria hivyo Dk Kilonzo amesema ni pamoja na ongezeko la watazamaji wa kazi za filamu na kutolea mfano tamthiliya ya Juakali imepata tuzo ya tamthiliya bora nchini Zambia, jambo linaloonyesha namna gani  tamthiliya za kitanzania zinatazamwa.

Pia ameeleza kumekuwa na Tv za nje zinakuja kuchukua filamu, ikiwemo Novela ya nchini Uholanzi ambayo mpaka sasa imeshachukua filamu tatu za Kiswahili, hatua ambayo ni nzuri.
Pia suala la kuongezeka kwa kumbi za sinema zinazofika 11 ambazo zimekuwa zikionyesha filamu hizo za Kiswahili tofauti na ilivyozoeleka huko nyuma kumbi hizi kuonyesha filamu za nchi za nje tu.
Wakati kwa tamthilia ya ‘We Men’ amesema inatarajia kuzalisha ajira  zaidi ya 100 hadi pale itakapomalizika.