Baba Levo aitikia wito wa Basata

Msanii wa vichekesho na muziki, Clayton Chipando maarufu baba Levo, amewasili Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) akiwa ndani ya gari la Wasafi kwa ajili ya wito wa baraza hilo.

Baba levo aliwasili katika ofisi hizo leo Alhamisi Aprili 15, 2021 saa 4:00 asubuhi hii ikiwa ni kuitikia wito baada ya kupokea simu kutoka kwa mmoja wa maofisa kutoka baraza hilo jana kumtaka afike hapo saa 5:00.

Hata hivyo ikitegemewa labda angewasili na gari yake lakini mambo yamekuwa tofauti kwani alifika katika ofisi hizo akiwa na gari la kampuni ya Wasafi akiwa ameingozana na baadhi ya watangazaji wa kituo cha Wasafi Tv.

Msanii huyu anafanya hivyo ikiwa imepita siku moja tangu onekane akiwa kwenye pikipiki ilihali alishazawadiwa gari na bosi wake Diamond Platnumz aina ya Harrier.

Baada ya kuwasili alikaa ndani ya gari hiyo takribani nusu saa kwenye maegesho ya magari kabla ya saa 4:30 kuelekea ofisi za uongozi za Basata ikiwa ni dakika 30 kabla ya muda aliotakiwa kufika.

Alipofika ndani ya ofisi hizo alifika dirisha la mapokezi la ofisi ya Katibu Mtendaji, na kujieleza kuwa amefika hapo kuitikia wito.

Mmoja wa wafanyakazi aliyekuwa akimsikiliza alimuagiza akakae kwenye kiti ili amuitie muhusika na ndipo alipofika baba mmoja na kumueleza asubiri kwanza na kuwataka waandishi wa habari waliokuwepo eneo hilo waliokuwa wakitimuza majukumu yao kuondoka kwa kile alichoelezwa hakuruhusiwi kuchukua picha wala kufanya mahojiano yoyote.