Awilo, Harmonize waingia studio

Msanii wa muziki wa Bongofleva, Harmonize ameingia studio na Mwanamuziki kutoka Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo, Awilo Longomba.
Awilo  yupo nchini kwa takribani siku ya nane sasa na  anatarajiwa kuwepo mwezi mzima kwa ajili ya shughuli ya kurekodi filamu ya ‘A life to Regret'.
Msanii huyo nguli amewahi kutesa na vibao mbalimbali ikiwemo Gate Le Coin, Coupe Bibamba, Porokondo, Bibala na Caroline, alipotua nchini pamoja na kuzungumza mambo mbalimbali,alisema kipindi ambacho atakuwepo ana mpango wa kuingia studio na baadhi ya wasanii wa Bongo ambao hakuwa tayari kuwataja majina na kuwakaribisha wengine watakaopenda kufanya naye kazi.
Jana kupitia Instastory kwenye mtandao wa Instagram, Harmonize aliweka video ikiwaonyesha akiwa na mwanamuziki huyo katika maongezi na nyingine akiwa studio anaimba katika kipazasauti kinachotumika kurekodia.
Katika video hiyo, Harmonize anaandika "Waoooo this is big night I ever had, lover legend ,respect the legend lets do this,” akimaanisha ni moja ya siku nzuri maishani mwake na anamuheshimu mkongwe huyo.
Wakati akizungumza na waandishi wa habari muda mchache baada ya kutua Uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mwalimu Nyerere Dar es Salaam Aprili 8, Awilo alikiri kuwa husikiliza muziki wa wasanii wa Bongo na kuwataja baadhi anaowapenda kuwa ni pamoja na Diamond Platnumz, Alikiba, Harmonize na Rosaree.