Alicia Keys awafunda Zari na Hamisa Mobetto!

Kabla ya kukutana na Alicia Keys aliyefanikiwa kumthibiti, Swizz Beatz alikuwa kijogoo kweli kweli, kuanzia Bara la Amerika Kusini hadi Ulaya kote aliweka chapa yake na kuumiza moyo wa mrembo asiye na hatia, Mashonda Tifrere.

Mfululizo wa visa, mikasa na maridhiano kati ya Swizz Beatz, Mashonda hadi Alicia Keys ni darasa lingine huru kwa Mastaa maarufu Afrika Mashariki, Zari The Bosslady na Hamisa Mobetto ambao wamezaa na Diamond Platnumz.

Swizz Beatz ni Prodyuza wa Marekani, alianza kutambulika kupitia lebo ya familia yake, Ruff Ryders na kufanya kazi na DMX, ametengeneza nyimbo maarufu kama; Jigga My Nigga, Girl's Best Friend za Jay Z, Upgrade U, Chek on It, Ring the Alarm za Beyonce, Touch IT ya Busta Rhymes na Ultralight Beam ya Kanye West.

Basi Swizz Beatz na Mashonda walianza kuwa na uhusiano mwaka 1998, ujauzito wa kwanza wa Mashonda uliharibika mwaka 2000, wakati huo Swizz akiwa na mchepuko wake, Nichole Levy ambaye walijaliwa kupata mtoto wao, Nasir Dior mwaka huo.

Mwaka 2004 Swizz Beatz na Mashonda walifuna ndoa, Desemba 2006 Mashonda akajifungua mtoto wake, Kasseem Dean, hata hivyo, ndani ya ndoa Swizz akampiga tena tukio lingine Mashonda.

Nalo ni kuzaa nje na mwimbaji wa Uingereza, Jahna Sabastia ambaye alikutana mwaka 2007, wawili hao walijaliwa mtoto wao, Nicole Mei 2008 ila Swizz aligundua kuhusu uwepo wa binti huyo mwaka mmoja baada ya kuzaliwa.

Mwaka 2008, Mashonda akapigwa tena tukio ila hili ni zito zaidi, Swizz Beatz akaanzisha uhusiano na Alicia Keys, Mashonda alidai wakati hilo linatokea bado ndoa yao ilikuwepo na si kama ambavyo Swizz alidai kuwa walikuwa wameshatengana.

Alicia Keys huyu ni mwimbaji wa Marekani, akiwa na umri wa miaka 15 alichukuliwa na Columbia Records, baadaye alisaini Arista Records kisha J Records, mwaka 2004 wimbo wake 'My Boo' akimshirikisha Usher Raymond ulimpatia umaarufu mkubwa duniani.

Kwa ujumla Alicia Keys ameuza zaidi ya rekodi milioni 90 duniani kote, alitajwa na Billboard kama Msanii wa R&B/Hip Hop wa Muongo (2000) na alishika nafasi ya 10 kwenye orodha ya wasanii 50 Bora wa R&B/Hip Hop wa miaka 25 iliyopita, huku akiwa ameshinda tuzo 15 za Grammy.

Kwa mujibu wa Mashonda, aliwahi kukutana na Alicia Keys na aliyewakutanisha ni Swizz Beatz, hakujua mambo yanaweza kuwa hivyo, ila Swizz alidai wakati anaanzisha uhusiano na Alicia, tayari walikuwa wameachana kwa talaka miezi tisa au 10 iliyopita kufikia Juni 2008 na talaka yao ilikamilishwa Mei 2010.

Jambo hilo lilileta uhasama mkubwa kati ya Mashonda na Alicia Keys, walitupiana vijembe na maneno mitandao na moto uliwaka kweli kweli, Mashonda alidai kuwa Alicia Keys ndiye aliyeivunja ndoa yake.

Ikumbukwe Mashonda naye ni mwimbaji, aliwahi kusainiwa na lebo ya Full Surface chini ya uangalizi wa J Records ambapo pia Alicia Keys alisainiwa, Mashonda alitoa albamu yake ya kwanza 'January Joy' mwaka 2005 iliyotayarishwa na Swizz Beatz, Kanye West na Raphael Saadiq.

Mashonda ameshiriki kwenye ngoma kubwa kama; Girl's Best Friend ya Jay Z, Get No Better ya Cassidy na Listen Baby ya Fat Joe kutoka kwenye albamu yake, All or Nothing (2005).

Alicia Keys na Swizz Beats walifunga ndoa Julai 31, 2010 katika sherehe ya faragha iliyofanyika karibu na Bahari ya Mediterania, Alicia alijifungua mtoto wao wa kwanza wa kiume, Egypt Daoud Dean, Oktoba 2010 na wa pili, Genesis Ali Dean Desemba 2014.

Hata hivyo, baadaye mambo yalikuja kubadilika, Mashonda na Alicia Keys wakawa marafiki na kuwakutanisha watoto wao waliozaa na Swizz Beats pamoja, hapa ndipo Zari na Hamisa wanafundwa.  

Miaka 10 uliopita, ikiwa mtu angemwambia kuna siku moja Mashonda angesherehekea siku ya kina Mama duniani pamoja na mume wake wa zamani, Swizz Beatz na mke wake wa sasa Alicia Keys, labda angecheka sana.

Lakini ndivyo ilivyotokea siku ya kina Mama duniani Oktoba 2018 wakati Mashonda, Swizz Beatz na Alicia Keys, pamoja na watoto wao, wote walikusanyika na kuonyesha upendo kama familia moja.

Mashonda anasema licha ya talaka yake uliyomuacha na uchungu mkubwa mwaka 2010, maelewano waliyonayo sasa ni matokeo ya bidii ya miaka mingi.

Hata hivyo, kwa mara ya kwanza baada ya sakata hilo, Mashonda na Alicia Keys walikutana pekee yao mwaka 2012, katika siku ya kuzaliwa Kasseem (mtoto wa Mashonda) alipotimiza umri wa miaka sita.  

"Nikiwa na Alicia, hakuna njia ambayo ningeweza kumsukuma kando kwa sababu ndiye mwanamke katika maisha ya mwanangu, nilitaka kumjua kwa sababu mwanangu alikuwa akiniambia mambo ya ajabu." alisema Mashonda.

Linapokuja suala la uhusiano wake na Alicia Keys, Mashonda anasema hakuna hasira wala wivu, hawajawahi kuruhusu hilo kwenye mazungumzo yao.

"Ni urafiki mkubwa kuliko, kuna udada, tunapata chai pamoja, tuna mazungumzo kama wanawake; anataka kujua nina chumbiana na nani, ana ukarimu sana." alisema Mashonda.

Oktoba 2018 Mashonda aliachia kitabu alichoandika na kukiita, Blend: The Secret to Co-Parenting and Creating a Balanced Family (Siri ya Uzazi Wenza na Kuunda Familia Yenye Usawa), ambapo ameeleza mengi.

Mashonda ametoa uzoefu wake katika safari yake ya ulezi pamoja na mume wa zamani, Swizz Beatz na mkewe Alicia Keys, na kuonyesha jinsi familia iliyogawanyika inavyoweza kuundwa upya kwa upendo.

“Miaka sita iliyopita, mtoto wangu mwenye umri wa miaka mitano wakati huo aliniuliza kwa nini mimi na baba yake hatukupendana tena, nilitambua kwamba alikuwa akihoji ukosefu wetu wa mawasiliano na umoja tukiwa kama wazazi," Mashonda aliliambia Jarida la People.

"Uzazi mwenza ni mada ya ulimwengu mzima na wengi hawajui wapi pa kuanzia, kitabu hiki kitatumika kama msukumo na mwongozo unaohitajika kuwalea watoto wenye afya ya kihisia na kiakili." alisema Mashonda.

Hata hivyo, Mashonda hajaandika kitabu hicho pekee yake, bali Swizz Beatz na Alicia Keys nao wameshiriki kwa sehemu.

Kuna sura maalum ya kina baba iliyoandikwa na Swizz, pia kuna dibaji ya dhati iliyoandikwa na Alicia, watatu hao wanapaza sauti zao kusaidia vizazi vya familia duniani kote. Ni hakika kwamba kitabu hicho kitakuwa sanduku la vifaa kwa ajili ya wazazi waangalifu ulimwenguni kote.

Na kwa muda mrefu mashabiki wengi Bongo wanatamani walichofanya Alicia Keys, Mashonda na Swizz Beatz kitokee kwa Zari na Hamisa; kukutanisha watoto waliojaliwa na Diamond, na pengine kuwa kitu kimoja.

Utakumbuka wawili hao waliigia kwenye ugomvi mkubwa sana baada ya Hamisa kuzaa na Diamond wakati anajua alikuwa na uhusiano na Zari, ni kama mtu aliyemzunguka shoga yake maana katika sherehe ya 40 ya Tiffah, Hamisa alimzawadi sana kwa mbwembwe Zari.

Baada ya Hamisa kuonekana kuwa na ukaribu na Tanasha Donna na kukutana mara kwa mara, aliulizwa iwapo wana mpango wa kukutanisha watoto wao waliojaliwa na Diamond na kusema hilo linawezekana. Ila kufanya hivyo na Zari haijajulikana lini hasa na kwa namna gani, lakini Mashonda na Alicia Keys tayari wameshawafunda, kazi kwao!.