Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Akili kubwa Bongo iliyoajiriwa na muziki

Muziki Pict
Muziki Pict

Muktasari:

  • Hata hivyo, baba yake ambaye alikuwa akifanya kazi Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) hakutaka awe mtayarishaji muziki bali afanye kazi aliyoisomea ila Master J akashikilia msimamo wake wa kuendelea na muziki hadi kuondoka nyumbani.

Mwanzilishi wa MJ Production, MJ Records kwa sasa, Master J baada ya kuhitimu shahada ya uhandisi wa umeme Chuo Kikuu cha London aliamua kuweka vyeti kabatini na kugeukia sanaa kama mtayarishaji muziki na sasa ni mmoja wa wengi waliofanya hivyo licha ya kuwa kwa sasa amerudi kwenye taaluma yake.

Hata hivyo, baba yake ambaye alikuwa akifanya kazi Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) hakutaka awe mtayarishaji muziki bali afanye kazi aliyoisomea ila Master J akashikilia msimamo wake wa kuendelea na muziki hadi kuondoka nyumbani.

Kwa mujibu wa Master J, Sugu ndiye msanii wa kwanza kumlipa vizuri katika kazi hiyo, awali alikuwa anarekodi kwa Sh50,000 ila Sugu akamlipa Sh100,000 na walianza kufanya kazi kwenye albamu yake pili, Ndani ya Bongo (1996). 

Mwaka 1997, akanunua gari lake la kwanza na ndipo baba yake akaanza kukubali kazi yake na sasa Master J anaheshimika na wengi kwa mchango wake mkubwa wa kuikuza Bongo Fleva huku studio yake ikirekodi albamu zaidi ya 500 kati ya mwaka 1996 hadi 2010.

Miongoni mwa nyimbo zilizorekodiwa MJ Records ni ule wa Mwana FA akimshirikisha Vanessa Mdee, Dume Suruali (2016) ambao ulitayarishwa na Daxo Chali, wasanii hao wawili nao shule ipo ila muda mwingi wameutumia katika muziki.

Hamis Mwinjuma ‘Mwana FA’ ambaye kwa sasa ni Naibu Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo na Mbunge wa Muheza, ni mhitimu wa Chuo Kikuu cha Coventry, Uingereza alipopata shahada ya uzamili katika usimamizi wa fedha.

Lakini Mwana FA aliyetoka na kibao chake, Ingekuwa Vipi (2002), yeye baada ya kupata umaarufu katika sanaa ndipo masomo ya chuo yakaanza akijiunga na Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) mwaka 2003 hadi 2007, kisha Coventry 2009 hadi 2010.

Hadi anateuliwa na Rais Samia kuwa Naibu Waziri hapo Februari 2023, Mwana FA alikuwa ametoa albamu mbili, Mwanafalsafani (2002), Toleo Lijalo (2003) na moja ya ushirikiano, Habari Ndio Hiyo (2008) akiwa na AY.

Kwa upande wake Vanessa Mdee aliyetoka na wimbo, Closer (2013) ulioshinda Tuzo za Muziki Tanzania (TMA) 2014 kama Wimbo Bora wa RnB, yeye alipata shahada ya sheria kutoka Chuo Kikuu cha Catholic University of Easterm Africa nchini Kenya.

Utakumbuka Vanessa alipambana sana kuipeleka Bongo Fleva kimataifa, mathalani mwaka 2013 alishiriki mradi wa The African Queens ulioandaliwa na aliyekuwa Rais Gabon, Ali Bongo, kisha mwaka uliofuatia akasaini dili na Universal Music Group (UMG).

Mtayarishaji muziki kutoka studio ya The Industry, Nahreel amefanya kazi na wasanii hao wawili, alishiriki kutengeneza wimbo wa Mwana FA, Mfalme (2014), na nyingi za Vanessa kama Come Over (2014), Nobody But Me (2015), Never Ever (2015) n.k.

Huyu Nahreel ana shahada ya sayansi ya kompyuta, elimu aliyoipata katika Chuo cha Punjab College nchini India ila hata baada ya kuhitimu masomo yake mwaka 2011 aliendelea kuwatengenezea wasanii midundo mizuri na mikali. 

Akizungumza na gazeti hili, Nahreel amesema baadhi ya wasanii kuonekana kutofanya kazi ya taaluma walizonazo, ni kutokana na mfumo wa tasnia ulivyo ila kuna baadhi baadaye huachana na muziki na kuamua kuajiriwa au kujiajiri. 

“Baadhi wameendelea kutoajiriwa kutokana muziki unachukua muda, kuajiriwa na kufanya muziki kwa wakati mmoja ni ngumu kidogo. Sawa muziki una fedha ila kuipata inachukua muda, huwezi kuanza muziki kesho na ukapata fedha, hamna hilo,” amesema.

Nahreel ambaye akiwa masomoni alitengeneza wimbo wa Joh Makini, Stimu Zimelipiwa (2009) ulioshinda TMA 2010, kama Wimbo Bora wa Hip Hop, anasema anatumia taaaluma yake kwa mambo binafsi ila bado hajafikiria kuajiriwa kutokana na ufinyu wa muda.

“Nafanya muziki, nasimamia akademi yangu ya mpira, nafanya biashara zangu nyingine mbili tatu, kwa hiyo muda wa kuajiriwa nisingepata kwa sababu muziki umechukua nafasi kubwa,” amesema Nahreel.

Ikumbukwe Nahreel anaimba pia akiunda kundi la Navy Kenzo na mwenzake Aika ambaye naye ana shahada ya uongozi wa biashara kutoka Chuo cha Punjab na huko ndipo walipokutana kisha mwaka 2013 kuunda kundi lao ambalo limetoa albamu tatu hadi sasa.

Nahreel sio msanii pekee Bongo aliyesomea sayansi ya kompyuta, kuna Roma - Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Nikki Mbishi - Chuo Kikuu cha Sayansi Mbeya (MUST) na Jux - Chuo Kikuu cha Guangdong, China.

Kipindi Roma anapata shahada yake UDSM ndipo wimbo uliompatia umaarufu zaidi ulitoka, Mathematics (2012) ambao ulimwezesha kushinda tuzo mbili za TMA 2013, alishinda vipengele vya Wimbo Bora wa Hip Hop na Msanii Bora wa Hip Hop.

Ikumbukwe wimbo uliomtoa Roma kimuziki, Tanzania (2007), awali aliurekodi M Lab (Music Laboratory) kisha baadaye akaenda kuurudia Tongwe Records, studio ambayo imetoa wasanii wengi wa Hip Hop akiwemo Moni Centrozone.

Centrozone ambaye alishirikiana na Roma katika ngoma, Usimsahau Mchizi (2017), ni msomi kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) alipopata shahada ya jiografia na mazingira mwaka 2015, na yeye hadi sasa anafanya muziki tu.

Huyu alikuwa katika kundi la Centrozone liloanzishwa mwaka 2009 mkoani Dodoma, mwaka mmoja baadaye wakaanza kurekodi Tongwe Records ambapo walisainiwa na lebo hiyo, kisha mwaka 2015 akaanza kutoa kazi zake binafsi.

“Tangu nakua ndoto yangu ilikuwa ni muziki, kwa hiyo kwanza nilihakikisha natimiza ndoto zangu kama msanii lakini pia kufuata mfumo wa kielimu kama kijana na sio kwa ajili ya kuajiriwa tu bali kwa maisha ya kila siku,” anasema Moni. 

“Hivyo kipaumbele haikuwa ajira kwa sababu wakati nasoma tayari nilikuwa natengeneza njia za kuja kuwa mwanamuziki. Kwa hiyo nilianza kurekodi siku za nyuma na kutafuta nafasi nikijua kabisa nitakapomaliza chuo hiki kitu ndicho nitakachokifanya,” anasema. 

Kwa sasa Moni yupo katika mradi wa Serikali Kuu ya Mizuka ambao una wasanii wengine kama Country Wizzy, Young Lunya, Conboi na Salmin Swaggz ambaye ana shahada ya teknolojia na mawasiliano na hata katika wimbo wao wa kwanza, Serikali Kuu ya Mizuka (2020) ameeleza kujivunia hilo.