TUONGEE KIUME: Godzilla alikuwa anatupigisha pindi Waandishi wa Habari

Godzilla alikuwa anatupigisha pindi Waandishi wa Habari

UKINIULIZA ngoma zangu bora za wakati wote lazima utasikia nimeitaja Kila Wakati ya Golden Jacob Mbunda maarufu Godzilla akimshirikisha G Nako. Ile ngoma ilikuwa ya moto nadhani inawezekana ndiyo ngoma pekee ambayo Godzilla alianza kuitengeneza kwa kuandika mashairi kwa sababu kama unavyojua King Zilla alikuwa ni mfalme wa freestyle. Kwa hiyo hit song zake nyingi alikuwa anapiga kwa mitindo huru.

Ukisikiliza ‘Kila Wakati’ mashairi yametulia sana imeandikwa kiutu uzima mno, lakini mbali na hivyo ukiisikiliza utagundua ni kama vile anaimba kumdisi au kumchana mtu fulani ambaye ni msanii mwenzake.

Ngoma inaanza kwa mistari hii “kujua mziki homie that’s not enough, Ukishindwa rudi matawi ya chini omba upigwe tough, discipline kuwa nayo maintain yourself, lete kiburi upewe kiburi yaani u-burial-we safe...”

Na wakati ngoma inatoka Godzilla hakuwa katika wakati mzuri alikuwa kwenye kipindi kigumu. Kipindi ambacho anatoa ngoma haziendi tofauti na ilivyokuwa awali ambapo kila akiachia ngoma inatoboa. Kila msanii anataka kumshirikisha Godzilla.

Na pia alikuwa kwenye kipindi ambacho tayari vyombo vya habari vilishaanza kumtengenezea taswira mbaya. Baadhi ya media zilikuwa zinamchukulia kama mvuta bangi tu au mhuni aliyepoteza mwelekeo wa muziki na sanaa yake.

Wengine walikuwa wanampa sifa ya kiburi, jeuri, eti hana nidhamu, hana ile professinalism. Unajua tena media zinavyofanya kwa baadhi ya wasanii kuwachoresha na sifa ambazo zinaweza kuwa kweli au sio kweli.

Sifa ambazo baadaye zilitajwa kama moja ya sababu ya kuporomoka kwa muziki wa Godzilla. Mtaani walikuwa wanasema anajua muziki, lakini hana nidhamu.

Na kubwa zaidi wakati wimbo wa ‘Kila Wakati’ unatoka Billnass naye alikuwa ndiyo anafanya vizuri kwenye gemu na uimbaji wake ulikuwa unafananishwa sana wa Godzilla. Na siyo uimbaji wa Billnass pekee uliokuwa unafananishwa na Godzilla, mambo yalikwenda mbali hadi wakasema uwepo wa Billnass ndiyo umesababisha kufulia kwa Godzilla.

Kwa hiyo, wimbo wa Kila Wakati ulipotoka watu wengi mtaani na hata vyombo vya habari vilikuwa vinadhani Godzilla ameandika kama dongo kwa Billnass.

Lakini juzi nilikuwa nausikiliza tena huo wimbo mara kuna ‘kitu kikanambia’ vipi kama ni kweli Godzilla alimuimbia mtu ule wimbo na vipi kama huyo mtu mwenyewe alikuwa ni yeye mwenyewe. Yaani vipi kama Godzilla alikuwa anajiongelesha mwenyewe kwenye ule wimbo? Kwamba labda alikuwa amegundua sababu zilizomshusha na sasa alikuwa anajipa taarifa kupitia wimbo, yaani ni kama vile Godzilla kutoka miaka ya mbele anarudi kumtahadhalisha Godzilla wa miaka ya nyuma kuhusu kutatufa dawa ya muziki wake kushuka.

Labda kwenye mistari yake wakati anasema “kujua muziki pekee haitoshi, ukishindwa jishushe uombe msaada”... labda hakuwa anamwambia Billnass wala msanii yeyote. Labda alikuwa anajiambia mwenyewe kutokana na zile sifa mbaya alizopewa na vyombo vya habari.

Labda wakati anasema “kuwa na heshima, ukishindwa ukiwa na kiburi, watu watakuzika na hautosikika”.. vipi kama hakuwa anamwambia Billnass au msanii yeyote yule? Vipi alikuwa anajiambia mwenyewe kutoka na namna watu walivyokuwa wanamzungumzia?

Nimegundua, muda mwingine mashabiki na vyombo vya habari tunalazimisha watu wawe na ugomvi wakati pengine kinachohitajika ni kutulia na kusikiliza kwa makini na kuelewa tu. Kwaheri Godzilla, utakumbukwa!