Mitano tena kwa Profesa Jay

KABLA ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 kumpeleka bungeni, Joseph Haule a.k.a Profesa Jay alikuwa akiwatumikia Watanzania kupitia sanaa. Sauti na mashairi yake konki ikikutana na midundo mikali ya prodyuza kama vile P Funk Majani ilikuwa ni mazishi.

Lakini alipoingia bungeni kama mbunge wa Mikumi kupitia Chadema, licha ya kwamba aliendelea kufanya muziki, lakini haikuwa kwa kasi na nguvu kama ilivyokuwa zamani. Alikuwa akiachia ngoma taratibu na hata alipofanya hivyo hakupata muda wa kuzitangaza kama ambavyo wasanii wa sasa wanafanya — na unaweza kusema hiyo iliwaacha mashabiki wa muziki wake na kiu kubwa.

Hata hivyo, matokeo ya uchaguzi mkuu 2020 yaliamua kuwa Profesa mwana Msolopaganzi asirudi tena bungeni baada ya kushindwa kutetea nafasi yake ya ubunge.

Na baada ya matokeo hayo, Profesa alijifungia kwa muda akiwa mbali na vyombo vya habari, kabla ya hivi karibuni kurudi uraiani kupitia wimbo mpya unaoitwa Baba ambao ameshirikishwa na rapa Stamina.

Mwanaspoti limepiga stori na Heavy Weight MC huyu aliyeimba nyimbo za kukumbukwa kama vile Ntakusaidiaje na Bongo Dar es Salaam na amefunguka mengi yakiwemo maisha nje ya ubunge, pia ameongelea kuhusu kurudi kwenye muziki pamoja na kujaribu tena siasa.


MAISHA NJE YA UBUNGE

Akijibu swali la kwa sasa hayupo tena bungeni anayaonaje maisha, anadhani ni mazuri zaidi ya alivyokuwa bungeni au anapendelea zaidi maisha ya ubunge, Profesa anaeleza kuwa kwa upande wake hakuna kigeni kwani kabla ya kuwa mbunge alikuwa ni mwanamuziki.

“Kabla ya kuwa mbunge nilikuwa mwanamuziki tu, kwa hiyo maisha ninayoishi sasa hayana utofauti sana na nilivyokuwa naishi zamani,” anasema.

Anao-ngeza kuwa hata hivyo anadhani maisha ya nje ya Bunge yanawapendeza zaidi watu wa familia yake kama vile mke na watoto kwa sababu muda mwingi anapata wa kuwa nao karibu.

“Unajua kuwa mbunge ni shughuli inayokula muda mwingi sana. Unatakiwa uwe jimboni kwako mara kwa mara jumlisha vikao vya chama, vikao vya Bunge na kadhalika. Inakufanya upate muda kiduchu sana wa kuwa na familia yako. Mimi binafsi nachukulia hata watu wa jimbo langu ni familia yangu, lakini naamini kwa upande wa mke wangu na watoto hawaichukulii hivyo, nadhani wao wanatamani niwe na muda zaidi kuwa karibu nao, kwa hiyo nadhani labda wanapenda zaidi maisha ya Profesa Jay msanii kuliko Profesa mbunge,” anasema.


KURUDIA MUZIKI

Profesa ametaka kuwathibitishia ma-shabiki wake kupitia Mwanaspoti kwamba amepanga kuitumia miaka mitano ambayo atakuwa nje ya Bunge kufanya muziki. “Nataka kuhakikisha kuwa miaka hii mitano ni kwa ajili ya kuwapa raha mashabiki wa muziki wangu kwa sababu moja ya vitu nilivyogundua ni kwamba bado wananihitaji. Kwa hiyo nitafanya muziki tu mpaka 2025,” anasema.

Anaongeza kuwa hata wimbo mpya alioshirikishwa na Stamina ulitakiwa uwe umetengenezwa muda mrefu, lakini imewezekana mwaka huu kwa sababu yupo nje ya Bunge.

“Hata huu wimbo wa Stamina alinipigia simu kunielezea wazo muda mrefu sana, lakini kutokana na ratiba zangu kila siku nikawa namsubirisha. Lakini kwa sasa niko huru, ndiyo tukapata nafasi ya kufanya.”

Kuhusu ratiba ya kuachia ngoma itakavyokuwa, Profesa anasema kwa sasa anakesha studio akitengeneza ngoma na pindi atakapokuwa tayari kuachia makombora atatoa taarifa.


KURUDIA SIASA

Ikumbukwe 2025 utafanyika uchaguzi mkuu mwingine na hiyo itakuwa ni fursa ya kumuona Profesa Jay kwenye majukwaa akiomba kura, lakini hilo litawezekana ikiwa tu mwenyewe atakuwa na mpango huo.

Alipoulizwa kama ana mpango wa kurudi kwenye ulingo wa siasa kwenye uchaguzi mkuu ujao, Profesa alijibu NDIYO kubwa huku akiainisha kwamba anaweza kurudi kugombea nafasi ya juu zaidi ya ile ya mwanzo, yaani kugombea urais.

“Nina malengo makubwa sana ya kuwatumikia wananchi, kwa hiyo kurudi kwenye uchaguzi ni jambo la lazima nikiwa hai. Lakini pia, msishangae nikarudi kugombea nafasi ya juu zaidi, ya urais,” anasema Mzee wa Mitulinga.

“Mikumi ni sehemu ndogo sana ya Tanzania, na Watanzania wengi wana matatizo kama waliyowahi kuwa nayo watu wa Mikumi. Na ukiangalia mimi nimesaidia kutatua matatizo mengi ya Mikumi, kwa hiyo natamani siku moja nifanyie hivyo Tanzania.”