Christian Bella awachanganya Ruby na Nandy

Christian Bella awachanganya Ruby na Nandy

NI miongoni mwa waimbaji wachache wazuri tuliobahatika kuwasikia kipindi hiki, alianza kusikika ndani ya Bongofleva kupitia Tanzania House of Talent (THT) na ndipo alipopewa jina la Ruby.

Ameshiriki kwenye miradi mikubwa upande wa tasnia kama Coke Studio Africa, amefanya shoo na kolabo kubwa kwa kifupi amefanikisha mengi mazuri kwa kiasi chake. Bongo Music Facts inakujuza zaidi.

1. Wimbo wa kwanza kumtoa Ruby kimuziki, Na Yule umeandikwa na Barnaba, wakati anapewa wimbo huo na alitaka kuukata kutokana na kile alichosema unasikika (sound) kama wa Injili lakini ulipokuja kutoka ikawa ni habari nyingine.

2. Ruby alikuwa mchezaji soka mzuri tu akicheza namba nane uwanjani na aliwahi kuichezea Young Twiga Stars, hii ni sawa na Alikiba ambaye aliwahi hadi kucheza ngazi ya Ligi Kuu Bara akiwa na Coastal Union.

3. Director Kelvin Bosco kutoka nchini Kenya alijitolewa kufanya bure video ya wimbo wa Ruby, Na Yule baada kusikia ukali wake, video ilikuja kutoka Mei 16, 2015 na hadi sasa ndio video pekee ya Ruby iliyotazamwa zaidi YouTube ikiwa na views milioni 9.9.

4. Ruby alianza kuimba alipo maliza darasa la saba akiwa kanisani katika kikundi cha ‘Praise and Worship’, hakuwahi kujiona ndani ya Bongofleva ambayo kuna kipindi ilimvuruga hadi kufikiria kujiua.

5. Hadi sasa Ruby hajatokea kwenye video za nyimbo mbili alizoshirikishwa, nazo ni ‘Su’ ya Yamoto Band na ‘One Day’ yake Motra The Future, hii ni sawa na Belle 9 ambaye hajatokea kwenye video kama; ‘13’ ya Young Killer na ‘Tunasafisha’ ya Edu Boy.

6. Ruby ni ndugu na Prodyuza wa muziki, Mazuu upande wa Baba, Mazuu ameweza kufanya kazi na wasanii kama Shilole, Q Chief, Nuh Mziwanda, Abdukiba na wengineo.

7. Hadi anajiunga THT, Ruby alikuwa hamfahamu kabisa Ruge Mutahaba kiasi kwamba alifika ofisini na kumuulizia wakati naye alikuwepo hapo hapo jambo lilofanya waliokuwepo karibu kumcheka!.

8. Miongoni mwa malengo ya Ruby ni kuja kuanzisha Chuo cha Muziki kitakachofundisha kutengeneza muziki mzuri, kutengeneza na kukua chapa ya msanii na mengine mengi katika eneo hilo.

9. Katika wimbo wa Christian Bella, Ollah akimshirikisha Khalighraph Jones kutokea Kenya, kuna sauti za Ruby na Nandy mwishoni ambazo walizirekodi kwa nyakati tofauti, walikuja kugundua wamewekwa pamoja baada ya wimbo kutoka.

10. Ruby aliingia THT baada ya kushida shindano la uimbaji chini ya Fiesta, Super Nyota Diva ambapo zawadi ya mshindi ilikuwa ni kurekodi albamu na kufanyiwa promosheni ya muziki wake. Hii ni sawa la Lady Jaydee aliyeshinda shindano laVipaji Halisi kupitia Radio One na kupata nafasi ya kurekodi kwa mara ya kwanza MJ Records.