#WC2018: Unaanzaje kuzikosa hizi kwa mfano

Muktasari:

  • Kwenye mechi hizi kali kabisa kwenye fainali hizo za Kombe la Dunia huko Russia, kwenye hatua ya makundi tu, unataka nani apigwe?

MOSCOW, RUSSIA. WAPIGWE tu, hiyo ndiyo lugha ya mashabiki wa soka pale wanapokwenda kutazama mechi hasa ikiwa moja ya timu hizo wakiwa hawaipendi.

Kwenye mechi hizi kali kabisa kwenye fainali hizo za Kombe la Dunia huko Russia, kwenye hatua ya makundi tu, unataka nani apigwe?

Yote kwa yote hizo ndizo mechi ambacho hupaswi kabisa kuzikosa kwenye hatua ya makundi ya fainali hizo za Russia. Ukizikosa, umekosa utamu kamili wa Kombe la Dunia 2018.

Misri vs Uruguay, Juni 15

Mohamed Salah atatazamwa sana kwenye mchezo huu kama atakuwa kwenye ubora wake kuendeleza kile alichokianzisha cha kuwapeleka Misri kwenye fainali hizo za Kombe la Dunia huko Russia.

Mo Salah amekuwa na msimu bora kabisa huko Liverpool, akiweka rekodi ya kufunga mabao 44 kwa msimu na ilibaki kidogo tu wabebe ubingwa Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Lakini kwenye mechi hii atakutana na fundi mwenzake, Luis Suarez atakayekuwa upande wa Uruguay. Suarez naye aliwahi kuwa Liverpool na moto wake mashabiki wanaufahamu ukiweka kando yale anayofanya kwa sasa huko Barcelona.

Wachezaji wengine wa kuwatazama katika mechi hiyo ni Mohamed Elneny kwa upande wa Misri na Edinson Cavani kwenye timu ya Suarez.

Ureno vs Hispania, Juni 15

Ureno dhidi ya Hispania hakika ni moja kati ya mechi kali kabisa ambazo mashabiki watazishuhudia kwenye fainali hizi za Kombe la Dunia huko Russia.

Ureno ni tishio kwenye michuano hiyo hasa kutokana na kuwa na huduma ya Cristiano Ronaldo huku wakitokea kubeba ubingwa wa Ulaya miaka miwili iliyopita.

Lakini, Hispania kikosi chake kipya kina mchanganyiko wa wachezaji chipukizi na wenye uzofu ambapo kuna kundi la wakali kama Marco Asensio, David de Gea na Isco kwa upande wa vijana huku wakongwe ni Andres Iniesta, David Silva, Gerard Pique, Sergio Ramos, hivyo Ronaldo asitarajie kuwa na wakati mwepesi katika mechi hiyo hasa ukizingatia wanamfahamu vyema wakicheza wote pamoja La Liga na Real Madrid.

Argentina vs Iceland, Juni 16

Si unakumbuka yale maajabu ya Iceland kwenye fainali za Euro 2016 zilizofanyika Ufaransa, sasa kazi atakuwa nayo Lionel Messi na Argentina yake katika kuwakabili wakali hao.

Iceland ni taifa dogo kwenye soka, lakini asikwambie mtu, wachezaji wake wamesambaa sehemu mbalimbali kwenye klabu kubwa za Ulaya na hivyo Argentina ya Messi huenda ikakumbana na wakati mgumu kwenye mechi hiyo.

Hata hivyo, mechi hiyo ni suala la watu kusubiri tu kama kweli mende ataweza kuangusha kabati kwani kimsingi, Argentina ni taifa kubwa sana kisoka na lina wachezaji wengi mahiri ukilinganisha na waliopo kikosi cha Iceland

Brazil vs Uswisi, Juni 17

Mechi ya kwanza kabisa ya Brazil kwenye fainali za Kombe la Dunia tangu ilipochapwa zile 7-1 na Ujerumani miaka minne iliyopita, itacheza na Switzerland.

Hakuna ubishi, Brazil itataka kufanya tofauti katika mechi hiyo ili kuondoa machungu yale ya kupigwa nyingi kwenye Kombe la Dunia, lakini kwa bahati mbaya wanakumbana na timu ngumu.

Neymar na kundi la mastaa wengine Philippe Coutinho, Fred, Roberto Firmino na Willian watapambana kurejesha hadhi ya Brazil kwenye fainali hizo, lakini wakati mgumu unaowakabili ni kwamba watakutana na Xherdan Shaqiri na mwenzake Granit Xhaka, ambao wanaweza kuchafua hali ya hewa muda wowote mchezoni.

Ujerumani vs Mexico, Juni 18

Mabingwa watetezi Ujerumani wataingia uwanjani kutazama uwezekano wa kuanza kulitetea taji hilo, huku mechi yao ya kwanza ikiwa ngumu kweli kweli kwa kuwakabili Mexico.

Kikosi cha Ujerumani bado kipo vizuri, licha ya kumuweka kando mfungaji wa bao kilichoifanya kibebe ubingwa huo miaka minne iliyopita, Mario Gotze.

Lakini, wachezaji wengi waliopo karibu ni walewale waliokuwa kwenye fainali zile za Brazil kama vile Thomas Muller, Sami Khedira na Toni Kroos huku wakati huu ikiwaongeza Timo Werner na Marco Reus huku golini akitarajiwa kusimama kipa wake matata Manuel Neuer.

Lakini, watakwenda kukikabili Mexico ya Javier Hernandez maarufu kama Chicharito, mshambuliaji matata wa kutibulia watu.

Argentina vs Croatia, Juni 21

Argentina kundi lake kwenye fainali hizo za Russia si la mchezo mchezo kabisa kwa sababu ukiwaacha Iceland imepangwa pia na Croatia na kama unavyofahamu taifa hilo la Ulaya limesheheni mastaa wa maana ambao wanaweza kufanya chochote kwa muda wowote.

Croatia imesheheni vipaji vingi kwelikweli kuanzia kwa Luka Modric, Ivan Rakitic, Mario Mandzukic, Ivan Perisic na Dejan Lovren ambao watakuwa kwenye viwango bora vya kumkabili Lionel Messi na jeshi lake, ambalo pia kimsingi litakuwa limesheni mastaa wengi wa maana akiwamo Sergio Aguero, Paulo Dybala, Gonzalo Higuain na Angel Di Maria.

Denmark vs Ufaransa, Juni 26

Denmark si taifa dogo kwenye soka hasa zinapokuja fainali za Kombe la Dunia na kitendo cha kuwajumuisha mastaa wake wa maana kama Christian Eriksen na Andreas Christensen, hakuna ubishi kwamba mpinzani atakayekwenda kukabiliana nao, anapaswa kujipanga kwelikweli.

Moja ya mechi zake kwenye hatua ya makundi itakabiliana na Ufaransa, ambayo inapewa nafasi ya kufanya vizuri kutokana na kusheheni nyota wengi wa viwango vikubwa katika kikosi chao.

Ufaransa yenye mastaa makini kama Paul Pogba, Antoine Griezmann, Thomas Lemar, Kylian Mbappe, N’Golo Kante, Nabil Fekir na Ousmane Dembele wanatazamiwa kwenda kufanya makubwa huko Russia, lakini hilo haliwezi kuwa hadi kwanza waonyesha kiwango bora mbele ya Denmark hiyo Juni 26.

Senegal vs Colombia, Juni 28

Kwenye fainali hizo za Kombe la Dunia huko Russia, Simba wa Teranga yaani Senegal itakwenda kuongozwa na mshambuliaji wake matata kabisa, Sadio Mane, ambaye hakuna asiyemfahamu kutokana na kile alichokifanya huko kwenye kikosi cha Liverpool msimu uliomalizika karibuni.

Alifunga mabao 20 katika mechi 44. Hakika baada ya kushindwa kubeba taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya, Mane atakuwa na hasira ya kufanya vizuri kwenye Kombe la Dunia na hakika Colombia wajiandae kwenye mechi yao hiyo itakayofanyika uwanjani Samara Arena mwishoni mwa mwezi huu.

Colombia silaha yake kwenye fainali hizo atakuwa James Rodriguez, ambaye kwenye fainali zile zilizofanyika Brazil alifanya maajabu makubwa.

England vs Ubelgiji, Juni 28

England itakwenda kwenye fainali za Kombe la Dunia safari hii ikitaka kuondoa gundu lililoikabili kwenye fainali mbili za michuano hiyo zilizopita, Afrika Kusini na Brazil.

Lakini kasheshe kubwa la huko Russia ni kwamba Three Lions watakuwa na shughuli ya kuikabili Ubelgiji, timu iliyosheheni vipaji vya hali ya juu kwelikweli.

Timu hiyo na wakali kama Eden Hazard, Romelu Lukaku, Kevin de Bruyne, Thibault Courtois na wengineo kibao huku silaha ya England ikiwa ni straika Harry Kane.

Hakika hii ni mechi ambayo hata mashabiki wenyewe wa England wanaisubiri kwa hamu kwa sababu sehemu kubwa ya wachezaji wa timu watakaochuana nayo yaani Ubelgiji wanacheza kwenye Ligi Kuu England.