#WC2018: Kane abeba kiatu cha dhahabu

Muktasari:

  • Kane, 24, amemaliza fainali hizo akiwa na mabao sita licha ya kushindwa kufunga katika pambano la kutafuta mshindi wa tatu juzi Jumamosi dhidi ya Ubelgiji, ambapo walichapwa mabao 2-0. Katika pambano hilo pia mpinzani wake wa karibu, Romelu Lukaku alishindwa kutumia nafasi hiyo kumpiku.

STAA wa England na Tottenham, Harry Kane amethibitisha ufalme wake katika ufungaji wa mabao soka la England, baada ya kuibuka kuwa Mfungaji Bora wa fainali za Kombe la Dunia zilizomalizika jana Jumapili kule Russia.

Kane, 24, amemaliza fainali hizo akiwa na mabao sita licha ya kushindwa kufunga katika pambano la kutafuta mshindi wa tatu juzi Jumamosi dhidi ya Ubelgiji, ambapo walichapwa mabao 2-0. Katika pambano hilo pia mpinzani wake wa karibu, Romelu Lukaku alishindwa kutumia nafasi hiyo kumpiku.

Katika pambano la jana, Kane alitazamiwa kupata upinzani kutoka kwa mastaa wawili wa Ufaransa, Antoine Griezmann na Kylian Mbappe ambao walifunga na kufikisha mabao manne kila mmoja.

Kane, ambaye ameibuka kuwa mfungaji bora wa England mara mbili katika misimu mitatu iliyopita huku akipitwa na Mohamed Salah msimu uliopita ingawa alifikisha mabao 30, kwa kuibuka kuwa mfungaji bora ameifikia rekodi ya Muingereza mwenzake, Gary Lineker ambaye aliibuka kuwa mfungaji bora wa Kombe la Dunia mwaka 1986 zilizofanyika nchini Mexico.

Kane pia ameweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza Muingereza kufunga katika mechi sita mfululizo za kimataifa tangu Tommy Lawton alipofanya hivyo mwaka 1939.

Mabao yote ya Kane yalikuja katika mechi nne za kwanza za England huku matatu kati ya hayo akifunga kwa njia ya penalti. Ni bao moja tu la Kane alifunga katika njia ya kawaida ya muvu ya uwanjani. Mengine alifunga kwa mipira ya adhabu ndogo ambayo ni mahiri.

Katika michuano hiyo, bao lake la kwanza alilifunga katika pambano dhidi ya Tunisia akimalizia kwa urahisi mpira uliotemwa na kipa wa Tunisia baada ya John Stones kupiga kichwa kufuatia mpira wa kona uliochongwa na beki wa kushoto, Ashley Young.

Bao lake la pili alifunga katika mechi hiyo hiyo kirahisi baada ya kumalizia mpira wa kichwa uliopigwa na beki, Harry Maguire kufuatia kona ya beki wa kulia, Kieran Trippier. Lilikuwa bao rahisi kama bao lake la kwanza.

Bao lake la tatu alilifunga kwa penalti katika pambano dhidi ya Panama na akafunga tena bao lake la nne kwa njia hiyo hiyo katika pambano hilo hilo. Alikamilisha ‘hat trick’ yake katika pambano hilo baada ya kuugusa kwa bahati mbaya mpira uliopigwa na kiungo, Ruben Loftus-Cheek. Bao hili linahesabika kuwa bao pekee la Kane katika muvu ya kawaida.

Kwa kufanya hivyo, alikuwa Muingereza wa pili kufunga hat trick katika Kombe la Dunia. Muingereza wa kwanza kufanya hivyo ni Sir Geoff Hurst aliyepiga hat-trick katika pambano la fainali Kombe la Dunia Wembley dhidi ya Ujerumani Magharibi ambapo, England ilishinda 4-2 na kutwaa taji hilo kwa mara ya kwanza na ya mwisho.

Bao lake la sita lilikuja tena kwa njia ya penalti katika pambano muhimu la robo fainali dhidi ya Colombia huku England ikishinda kwa penalti 3-4 baada ya Colombia kurudisha bao la Kane katika dakika za majeruhi.

Kwa jumla katika michuano hii, Kane angefunga mabao 14 kama mashuti yake yote sita yaliyolenga yangetinga wavuni. Mabao yake yote ameyafunga akiwa ndani ya boksi la adui huku matano akiyafunga kwa mguu wa kulia na moja akifunga kwa kichwa. Nusu ya mabao yake amefunga kwa penalti.

Katika michuano iliyopita ya Kombe la Dunia, staa wa kimataifa wa Colombia, James Rodriguez naye aliibuka kuwa mfungaji bora kwa idadi hiyo hiyo ya mabao akifunga mabao sita. Mabao hayo yalisaidia apate uhamisho wa pesa nyingi kutoka Monaco kwenda Real Madrid. kabla ya kupelekwa Bayern Munich.