#WC2018: Hili ndio chama kamili

Muktasari:

  • Lakini, kwa staa wa zamani wa Jamhuri ya Ireland, aliyewahi kucheza fainali mbili za Kombe la Dunia 1990 na 1994, Tony Cascarino, aliyewahi kuzichezea pia klabu za Chelsea na Olympique Marseille, amechagua kikosi chake cha kwanza kinachoundwa na mastaa waliocheza kwenye fainali hizo za Russia zilizotia nanga jana Jumapili.

PANGA chama lako la Kombe la Dunia 2018. Nani atakaa golini na staa gani atakuwa kwenye nafasi ya straika. Kila mtu atakuwa na chaguo lake kutokana na shughuli ilivyokuwa.

Lakini, kwa staa wa zamani wa Jamhuri ya Ireland, aliyewahi kucheza fainali mbili za Kombe la Dunia 1990 na 1994, Tony Cascarino, aliyewahi kuzichezea pia klabu za Chelsea na Olympique Marseille, amechagua kikosi chake cha kwanza kinachoundwa na mastaa waliocheza kwenye fainali hizo za Russia zilizotia nanga jana Jumapili.

Kwenye kikosi chake hicho, Cascarino amechagua mchezaji mmoja tu wa England, huku Ufaransa ikiwa na mastaa kibao na Croatia ikiingiza pia wakali wake.

Kikosi cha Cascarino kimewahusu nyota wote waliokuwa wakipewa nafasi ya kunyakua tuzo ya mchezaji bora wa fainali hizo za Russia, Luka Modric na Kylian Mbappe.

Uteuzi wa Cascarino, golini atasimama, Hugo Lloris, kipa nambari moja wa timu ya Taifa ya Ufaransa, wakati mabeki wake kulia ni Kieran Trippier wa England, kushoto ni Diego Laxalt wa Uruguay na kati ni Dejan Lovren wa Croatia na Raphael Varane wa Ufaransa.

Kwenye safu ya viungo, N’golo Kante wa Ufaransa atasimama kwenye kiungo ya kukaba, akisaidia na kiungo mwenzake wa kati, Paul Pogba wa Ufaransa pia, huku fundi wa mpira, Luka Modric wa Croatia atasimama kwenye kiungo ya kushambulia. Kiungo wa kushoto ni Eden Hazard wa Ubelgiji, wakati kiungo ya kulia ni Ivan Perisic wa Croatia.

Kwenye kikosi chake, Cascarino amemchagua, Kylian Mbappe wa Ufaransa kuwa ndiye straika wake.

Kwenye chama hilo, hakuna Neymar, Cristiano Ronaldo wala Lionel Messi, hiyo ikiwa na maana pia kutakuwa na mabadiliko makubwa kwenye Ballon d’Or ya mwaka huu.