#WC2018: Hazard bana! Eti kajitaja mwenyewe

Muktasari:

  • Hazard alisema: "Unaniuliza nani apewe tuzo...ninasema ni mimi lakini sitaki kusema nani, mimi pia ninastahili kupata tuzo, lakini ninadhani watatoa tuzo kwa mchezaji atakayecheza fainali."

Mshambuliaji wa Ubelgiji hakutaka kupindisha wala kuwaza sijui nani, alipoulizwa tu na waandishi wa habari kuwa anadhani nani anafaa kuwa mchezaji bora wa Fainali za Kombe la Dunia 2018, akajitaja mwenyewe.
Eden Hazard alisema yeye anafaa kuwa mchezaji bora wa Tuzo ya Golden Ball kwani aliiwezesha Ubelgiji kuishinda England na kushika nafasi ya tatu katika fainali za mwaka huu. England ilipigwa mabao 2-0 huku Hazard akifunga bao la pili.
Hazard alikuwa roho ya Ubelgiji huko Russia, akichochea mashambulizi, kufunga na akitoa asisti mbili.
Fifa imepanga kumtangaza mchezaji bora wa fainali za mwaka huu baada ya mchezo kati ya Ufaransa na Croatia.
Hazard alisema: "Unaniuliza nani apewe tuzo...ninasema ni mimi lakini sitaki kusema nani, mimi pia ninastahili kupata tuzo, lakini ninadhani watatoa tuzo kwa mchezaji atakayecheza fainali."

Inaonekana kama Kylian Mbappe na Luka Modric wanastahiki kupata tuzo ya Golden Ball na atakayetwaa kombe basi tuzo yake.
Croatia haijawahi kucheza fainali za Kombe la Dunia wakati Ufaransa imeshaingia mara kadhaa na inataka kutwaa ubingwa kama ilivyokuwa mwaka 1998 fainali zilizofanyika Ufaransa
Modric aliisaidia Croatia kuweka historia, wakati Mbappe ni chipukizi wa tatu kucheza fainali za Kombe la Dunia mwaka huu. Hazard sasa anajipanga kwa mapumziko kabla ya kuanza majukumu yake Chelsea.