Ziara ya Infantino itufumbue macho Waafrika

Muktasari:

Hiyo ni baada ya kuona kuwa nchi nyingi za Afrika zimekuwa na viwanja, lakini vilivyo vingi kati ya viwanja hivyo havikidhi viwango vya Fifa, hivyo kushindwa kutumika kwenye mechi za Fifa hata za kirafiki na baadhi ya mataifa yaliyoendelea kutoka Ulaya, Marekani na Asia.

Wiki iliyopita Rais wa Shirikisho la Soka duniani (Fifa), Gianni Infantino alikuwa na ziara nchini Gabon ambako alikwenda kuonana na Rais wa nchi hiyo, Ali Bongo Ondimba.

Katika zira hiyo Infantino alizuru maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutembelea ofisi za shirikisho la soka la nchi hiyo na kukutana na rais wa shirikisho hilo.

Infantino alisema kuwa Bara la Afrika lina vipaji vya mchezo wa soka vya kutosha isipokuwa changamoto iliyopo kwa nchi hizo zinafanana na siku Afrika ikifanikiwa kutatua changmoto hizo, basi ina uwezekano mkubwa wa kutawala soka la dunia.

Katika mipango aliyoizungumzia, alisema kuwa Fifa imepanga kutekeleza kusaidia maendeleo ya soka kwa Afrika ni pamoja na utekelezaji wa sheria namba moja kati ya sheria 17 za mchezo huo.

Alisema kuwa Fifa imepanga kutenga kiasi cha dola bilioni moja kwa ajili ya miundombinu yaani viwanja vya soka vyenye kuzingatia viwango vya shirikisho hilo katika kila nchi mwanachama barani Afrika.

Hiyo ni baada ya kuona kuwa nchi nyingi za Afrika zimekuwa na viwanja, lakini vilivyo vingi kati ya viwanja hivyo havikidhi viwango vya Fifa, hivyo kushindwa kutumika kwenye mechi za Fifa hata za kirafiki na baadhi ya mataifa yaliyoendelea kutoka Ulaya, Marekani na Asia.

Hivyo Fifa itatumia kiasi hicho cha fedha ambazo ni sawa na zaidi ya shilingi trilion mbili kwa ajili ya ujenzi wa viwanja vya soka katika Afrika.

Lakini kitu cha cha pili alichokizungumzia ni eneo la waamuzi katika mchezo wa soka ambalo linatakiwa kutengenezewa mpango mkakati maalumu wa kuzalisha waamuzi wa kulipwa vijana kutoka katika kila nchi.

Alisema lengo ni kuwa na kundi la waamuzi watakaokuwa wanafanya kazi ya uamuzi wa mchezo wa soka tu na si kazi nyingine kama walivyo wachezaji au makocha ambao wanafanya kazi moja pekee na si nyingine ambayo inawaingizia kipato kinachowafanya waishi, hivyo kuwa na waamuzi wa wa kulipwa kama walivyo wachezaji .

Utaratibu huu wa waamuzi wa kulipwa kwa mara ya kwanza ulianzia nchini Uingereza mwaka 2001 ambapo waamuzi wote wanasimamiwa na kulipwa kwa kazi wanayofanya na kampuni ya Proffesional Game Match Officials Limited (PGMOL) ambayo iliundwa kwa lengo la kuwaajiri na kuwasimamia.

PGMOL vilevile inasimamia utekelezaji wa majukumu yao na maslahi kutokana na kazi ya uamuzi wa soka wanayoifanya, hivyo rasmi kuanza kutambuliwa kama ni waamuzi wa kulipwa.

Eneo hilo la waamuzi ni moja kati ya maeneo yenye changamoto kubwa hasa kwa Afrika ikizingatiwa kwamba kazi hiyo si rasmi ya kulipwa kama ilivyo kwa wachezaji wa kulipwa, makocha na madaktari wa timu.

Hivyo waamuzi hujikuta wakiwasimamia watu wanaofanya kazi yao kwa kulipwa huku wao wakifanya kazi hiyo kwa kutolipwa, yaani hufanya kazi ya hiari licha ya ukweli kwamba mchezo huo kwa sasa umekuwa ukiingiza fedha nyingi ambazo hutumika katika kulipia gharama nyingine.

Hili eneo la waamuzi inaonekana limetoka katika ripoti ya Katibu Mkuu wa Fifa, Fatma Samoura ambaye kwa zaidi ya miezi sita amekuwa akisimamia utendaji wa shughuli za kila siku za Shirikisho la Soka barani Afrika (Caf), baada ya kuona kuwa kunahitajika mabadiliko ili kuboresha ushindani utakaozingatia misingi ya haki na uungwana (fair play).

Kwa hakika kama Fifa itatekeleza hayo katika soka la Afrika inaweza kutawala mchezo huu siku zijazo kama ilivyo Amerika Kusini hasa Brazil kwa miaka ya nyuma kwani Afrika siku zote haijawahi kukosa vipaji.

Hivyo kwa kuwa Fifa imekwisha sema kuwa ina mpango wa maendeleo kwa Bara la Afrika ukizingatia maeneo hayo mawili, nasi kama nchi tunaweza kuanza kufanya maandalizi katika maeneo hayo ili pale Fifa itakapokuja kwa ajili ya utekelezaji wa mipango hiyo, basi tuwe tumekwishaanza iwe rahisi kuendelea na hata sisi pengine kuwa ndio mradi wa mfano kwa mataifa mengine.

Lakini kingine alichokizungumza Inafantino katika mazungumzo yake na Rais wa Gabon ni kuwa, Afrika kutokuwa na mpango wa pamoja kama bara au hata mipango ya kikanda kama ilivyo Cecafa, Cosafa, Wafu na kanda nyingine.

Alisema inatakiwa kuwa na makubaliano ya kimaandishi ya ushirikiano ambapo wanachama wanao wajibu na si hiari kama ilivyo kwa sasa kushiriki katika mashindano yoyote yale ya ukanda huu wa Cecafa ni hiari na sio wajibu.