JAMVI LA KISPOTI : Zahera alivyojiingiza katika kitanzi kizito Yanga

Friday October 11 2019

 

By Khatimu Naheka

Yanga hawana raha na timu yao kwasasa kila wakifikiria kiwango chao akili yao haikai sawa wanafikiria mbali sana wapi wataangukia msimu huu na lawama zinazidi kuongezeka kila siku mpya inapoanza.

Kupoteza mechi moja na kupata sare moja kisha ushindi mmoja sio kitu kinachowaumiza Yanga kwani matokeo ya namna hii walishayapata huko nyuma, kisha wakarudi katika mstari wa ushindi kama ilivyokuwa enzi za makocha Torm Saintffiet na hata Marcio Maximo.

Kinachowanyima raha mashabiki wa Yanga ni jinsi kiwango cha timu yao na yale ambayo waliyatarajia wakati wa usajili wao kuelekea msimu mpya na Imani ambayo walijengewa hapo kabla na kufanya juhudi kubwa kujenga timu yao.

Inawezekana ikawa kila timu ndogo sasa inataka kukutana na Yanga haraka wakiwa katika hali hii kuliko ikija kubadilika, Yanga imekuwa haitishi tena.

Timu imekuwa ya kawaida na kinachowaumiza zaidi mashabiki na wanachama wao ni kwamba yanatokea katika msimu ambao unaanza huku wakiwa waliweka nguvu kubwa katika kujenga timu yao kwa muamko mkubwa wa kuchangia usajili wao kwa ile kauli yao ya kwamba timu ya wananchi inajengwa na wananchi.

Mambo haya yanapotokea hakuna mtu mwingine ataangaliwa kwa jicho la tatu zaidi ya kocha Mwinyi Zahera ambaye ndiye alikuwa injini kuu katika kuhakikisha Yanga inajengwa kwa kuhamasisha wanachama kuchangia usajili na ukafanyika ambao uligharimu fedha nyingi.

Advertisement

Zahera anaumia na kinachomtesa ni kwamba waliomuona shujaa ghafla wameanza kubadilika na kuona katika wachezaji aliowaleta inawezekana wakawa bora lakini bado wameshindwa kuonyesha uwezo.

Niliwahi kusema huko nyuma bahati mbaya inayomtokea Zahera ni kwamba anafanya kazi Tanzania katika nchi ambayo mashabiki wake wanapenda sana mpira, lakini hapohapo hawana uvumilivu mkubwa mambo yanapokwenda tofauti kama vile wanavyofanya wazungu kule Ulaya.

Hapa Tanzania unaposajili straika mashabiki wanataka matokeo kama ya Meddie Kagere anakuja anapiga mabao kama hana akili bila kutafuta sababu za kuzoea hali ya hewa wala kupungua mwili.

Hapa kwetu wanataka ukisema unasajili beki basi awe kama Lamine Moro yule aliyemleta haraka azoeane na wenzake kisha kazi ya kuzuia washambuliaji na kutoa mabao katika mstari wa goli kama alivyofanya kule jijini Gaborone nchini Botswana wakati Yanga ikiwatoa Township Rollers ya huko katika Ligi ya Mabingwa Afrika.Hawa ndio mashabiki wetu wanaweza wakakupenda lakini baadaye mambo kama hayaendi hawachelewi kubadilika haraka hawatakuwa na wewe.

Kwasasa watu wachache wameanza kubadilika wakiona kuna mambo hayako sawa baadhi wakiona usajili wao haukuwa wa umakini lakini wapo wengine wanaona ubora wa mbinu za uwanja kiufundi haziko sawa lakini wengine wanamini Yanga inahujumiwa. Soka ni mchezo wa wazi Yanga imepoteza ubora wake wa uwanjani kwasasa hawana tena ubora wa kutisha na sasa hata timu ndogo ambazo zilikuwa zikija Uwanja wa Uhuru au Taifa wanakula nane, sasa wanatafuta ushindi au sare hii sio ishara nzuri.

Hatua mbaya zaidi kwa Zahera uongozi huu hautakuwa na kazi katika kumuangushia jumba bovu kwa kusema tu kikosi chao walikisajili kwa matakwa ya mkocha na hata mbinu zi za makocha na wachezaji tunawalipa vizuri mpaka sasa tunanunua ushindi kwa sh 10 milioni,wakishasema hivyo shabiki yoyote hatakuwa na la kuongeza kwa Dk Mshindo Msola,Fredrick Mwakalebela au Frank Kamugisha ambaye ndiye mwenyekiti wa kamati ya usajili.

Moto utarudi kwa Zahera ambaye kunusuru hali hii ya sasa anatakiwa kuwa makini kuhakikisha anabadilisha haraka mwenendo wa timu hiyo sasa vinginevyo presha kubwa na hata kupoteza kazi kunaweza kuwa mgongoni kwake na kufuatana nalo kama vile binadamu anavyoongozana na kivuli chake wakati wa jua kali.

Kitakachomuandama Zahera ni ile ahadi yake kwamba ataleta wachezaji bora na wafungaji bora, mabeki bora na mpira mkubwa utapigwa kisha Yanga itatangaza ubingwa mapema ambapo sasa hali inakuwa tofauti katika ahadi hizo za awali.

Ahadi hizi ndizo ziliwafanya watu kuchanga fedha nyingi ili usajili ufanyike masikini Zahera hakujua kama anajiingiza katika janga kubwa ambalo waliomuona shujaa hawataweza kuvumilia kusikia Yanga inaendelea kuhesabu dakika mpira uishe, kwa kiwango duni anachotakiwa ni kuhakikisha mambo hayatokei kama yalivyotokea DC Motema Pembe mara ya mwisho alipokuwa bosi wa klabu hiyo kisha akapoteza kazi kwa matokeo mabaya.

Advertisement