Yanga isifanye masihara na Kombe la Shirikisho Afrika

Friday May 11 2018

 

WAWAKILISHI pekee wa Tanzania waliosalia katika michuano ya kimataifa, Yanga, wamerejea kutoka Algeria walikokumbana na kipigo katika mchezo wa kwanza wa makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Yanga imeanza vibaya ilipolala mabao 4-0 mbele ya wenyeji, USM Alger na kujikuta ikishika mkia wa Kundi D baada ya mechi za kwanza tu.

Kundi lake pia lina timu za Gor Mahia ya Kenya na Rayon Sports ya Rwanda zilitoka sare ya bao 1-1 katika mechi yao.

Matokeo ya Yanga hayajapokewa vema na mashabiki wake, ingawa kwa wajuzi wa mambo walishajua timu hiyo itakumbana na nini huko kwa jinsi ilivyowaacha nyota wake kadhaa nyumbani.

Karibu wachezaji nyota watano wa kikosi cha kwanza hawakusafiri na timu kwa sababu mbalimbali, huku pia kukiwapo na tetesi za mgomo kushinikiza kulipwa malimbikizo ya mishahara.

Mwanaspoti haina haja ya kujikita sana kuhusu undani wa jambo hilo ikiamini lipo ndani ya uwezo wa klabu kulimamliza.

Lakini tunachukua nafasi hii kuwakumbusha wachezaji na wana Yanga kwa ujumla, kuwa wakumbuke Yanga ipo Kombe la Shirikisho kuiwakilisha nchi, hivyo nafasi waliyonayo si ya kuifanyia mzaha.

Pia wanapaswa kuzingatia ukweli kuwa katika hatua hii ya makundi, kama wakizichanga vyema karata zao, watajitengenezea mamilioni ya fedha zinazotolewa na Shirikisho la Soka la Afrika (CAF). Ni fedha zitakazoisaidia klabu hiyo ukizingatia ukweli kwamba Jangwani sasa kuna ukame mkubwa fedha.

Hivyo kama watakaza kiume na kufanya kweli, mbali ya kusaidia kuipaisha nchi, lakini pia kama klabu watakuwa na nafasi ya kufanya miamala izunguke klabuni humo.

Kwa kaunzia walipo sasa, kila hatua ya michuano hiyo ina thamani yake na klabu shiriki inanufaika kwa fedha taslimu.

Ni kama ilivyo sasa ambapo Yanga imeshajihakikishia Sh600 milioni kwa kutinga tu kwao hatua ya makundi, wakifanya vyema zaidi watavuna zaidi fedha.

Tena si kwamba fedha zitamiminika Jangwani tu, bali zitaenda pia hadi Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF).

Hii ina maana kwamba kuanzia viongozi wa klabu hiyo hadi wale wa TFF, wana wajibu mkubwa wa kushirikiana kuhakikisha timu inapata matokeo mazuri ili kuweza kuvuna fedha zaidi.

Hakuna siri, hata TFF inakabiliwa na hali mbaya ya kifedha kiasi cha kudaiwa watendaji wake walikuwa wakipiga miayo ya njaa kwa kutolipwa mishahara hivi karibuni, huku Yanga yenyewe ikiwa na hali tete ya kifedha kiasi cha kupunguza morali ya wachezaji.

Kutokana na hali hiyo, lazima viongozi hao wakae na wachezaji na kuwaeleza jinsi hatua waliyofikia ilivyo na umuhimu kwao na wanapaswa kuitumia vyema ili kuvuna fedha na kuwapunguza matatizo waliyonayo kiuchumi.

Pia ni lazima wachezaji wenyewe watambue kuwa hatua waliyofikia ya ushiriki wao katika makundi, inatoa fursa kwao ya kujitangaza na kujiuza katika soko la kimataifa kwa sababu mechi zote sita watakazocheza hatua hiyo zinarushwa hewani.

Mawakala na maskauti wa wachezaji wa klabu mbalimbali wanafuatilia mechi hizo na kama wachezaji wataonyesha vipaji vyao wakati wakiipigania Yanga, ni wazi watakuwa pia wakijiuza katika soko hilo.

Hata Mbwana Samatta, Simon Msuva na nyota wengine wa kimataifa wa Tanzania wanaotamba nje ya nchi kwa sasa, walionwa kupitia michuano ya kimataifa na leo wanakula matunda wakiwa mifano ya kuigwa na wenzao waliosalia nchini.

Hivi ni kweli wachezaji wa Yanga hawapendi kupata timu nje ya Tanzania? Kwanini wanataka kuichezea bahati ya klabu yao kushiriki michuano hiyo ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika?

Ni kweli kuwa kama binadamu wengine, wachezaji nao wanayo mahitaji yao na lazima mabosi wao wayatekeleze, lakini vile vile watambue kuwa kwa sasa Yanga imeyumba sana tangu aliyekuwa Mwenyekiti na mfadhili wake, Yusuf Manji, kujiengua klabuni.

Lakini pamoja na hayo, Yanga itambue hakuna njia ya mkato katika kuyafikia mafanikio bila ya kuweka nia na kuifanyia kazi nia hiyo kwa kufuata misingi ya kusaka mafanikio yaani nidhamu. Yanga isifanye masihara na nafasi iliyonayo.