Wale mashabiki wanaozima viwanjani wana tatizo hili

PINDI zinapokutana timu zenye upinzani wa jadi hutokea msongamano mkubwa na viwanjani.

Hali hii husababisha watu wengi kuzimia kutokana na matokeo ya uwanjani au nje ya uwanja kama siyo yote.

Unaweza ukadhani inatokea tu kwa mashabiki wa Simba na Yanga, hapana hata katika mechi za kimataifa hali hii hutokea.

Sababu za kuzimia

Kitabibu kuzimia hujulikana kama Syncrope kwa Kingereza Fainting, ni hali ya kupoteza fahamu kwa muda mfupi inayoweza kumpata mtu yeyote ikiwamo watu wenye afya njema.

Mara nyingi sababu huwa ni uchache wa hewa ya oksijeni katika ubongo. Mtu anapozimia mwili huruhusu kufanyika kwa shughuli za ndani huku shughuli za nje ya mwili ikiwamo kutembea, kusikia, kuongea na kuona zikisitishwa.

Ni tatizo la muda endapo tu hakuna tatizo lolote la kiafya lililochangia, mwili hutatua hatilafu hiyo na baadaye fahamu hurudi katika hali ya kawaida.

Vilevile tatizo hili linaweza kuwa ni ishara ya uwepo wa tatizo kubwa la kiafya mwilini na ndiyo maana inashauriwa anayezimia apewe huduma ya kwanza na uangalizi kama mgonjwa wa dharula.

Kawaida mwili ukiwa katika hali hiyo maeneo nyeti ikiwamo ubongo na moyo ndiyo yanayopewa kipaumbele kupata damu nyingi yenye oksjeni.

Mwili hubana matumizi ya damu kwa kuinyima misuli ambayo kipindi cha kuzimia huwa imetulia. Kipindi hiki mishipa ya pembezeni hujibana ili kuongeza msukumo wa damu na moyo hudunda kwa kasi ili kuhakikisha maeneo nyeti yanapata damu yenye oksijeni.

Unaweza kujiuliza kwanini wasisizimie wachezaji waliopo uwanjani? Lakini kumbe mashabiki ndiyo huwa katika shinikizo kubwa wakifuatilia kwa umakini kila kinachoendelea.

Kuwepo katika msongamano katika michezo ya wapinzani wa jadi ambayo huwa na idadi kubwa ya watu ambao ni kitu hatarishi kuweza kuzimia.

Tofauti na wachezaji wao wapo katika eneo la katikati ya uwanja wakiwa wanapata hewa ya kutosha. Hali ya hewa ya joto na kutokwa na jasho sana kunaweza kusababisha mtu kupoteza maji mengi mwili, hivyo kusababisha mtu kuzimia kutokana na upungufu wa maji na chumvi mwilini.

Upenzi wa timu uliokithiri huchangia kupatwa na mshtuko mkali pale timu inapofungwa hivyo kupata mabadiliko ya ghafla ya hisia.

Hali hii kuzalisha hasira inayoambatana na kutiririshwa kwa wingi kwa homoni ya Adrenalini ambayo nayo inaweza kuchangia kuzimia.

Baadhi ya watu miili yao hukosa ustahimilivu wa kukabiliana na uchache wa hewa hivyo kuzimia kirahisi. Maelfu ya mashabiki hupokonyana hewa kidogo iliyopo na huku miili yao huwa katika shinikizo kubwa kutokana na hali ya joto, makelele na hisia kali za ushabiki huweza kuchangia kuzimia.

Kutumia muda mwingi kusafiri na foleni barabarani mpaka kufika viwanjani, mihangaiko ya kupata tiketi na kuingia ndani ni mambo yanayouchosha mwili hivyo hatarini kuzimia huwa ni kubwa.

Dalili ni zipi?

Dalili za kuzimia zinaweza zisiwe za moja kwa moja kwani inawezekana mtu aliyezimia akakumbuka tu kuona giza au kizunguzungu kisha asikumbuke kitu. Pia mtu anaweza kuzimia na akakumbuka kila kitu ikiwamo dalili zilizompata mpaka alipoanguka na kugonga chini.

Wengi wanaozimia wanakumbuka tu dalili ya kuona mawimbi au giza giza na kizunguzungu kisha kuishiwa nguvu na kupoteza fahamu.

Mara nyingi dalili za jumla ni pamoja kuishiwa nguvu, kupumua kwa shida, kuona nyota na giza, kizunguzungu, mapigo ya moyo huwa ya juu, kuchanganyikiwa au kuweweseka, kuhisi miguu kukosa nguvu na kuwa mizito, joto kupanda au kutokwa jasho, kupata kichefuchefu au kutapika na kupiga miayo mingi.

Walio katika hatari ya kuzimia ni pamoja na wenye matatizo ya moyo, ubongo, upungufu wa damu, lishe duni, shinikizo la kushuka la damu, magonjwa ya mfumo wa hewa, upungufu wa maji, msongo wa mawazo na wasiofanya mazoezi.

Faida na hasara za kuzimia

Faida ya kuzimia ni mwili kusahihisha dosari iliyojitokeza kwani kipindi hiki mwili hulipa deni la upungufu wa hewa ya oksijeni kwa kuruhusu damu kwenda maeneo nyeti zaidi ili kulinda uhai.

Hasara ya kuzimia ni pamoja na majeraha ya kichwa, kuchubuka, kujeruhi tishu laini. Kifo huweza kutokea kama mwili utashindwa kurekebisha dosari iliyojitokeza na pia kama oksijeni ni chache sana na ubongo ukaendelea kukosa oksijeni muda mrefu.

Jinsi ya kutoa huduma

Kwanza ni kumtoa katika eneo hatarishi na kumweka eneo salama lililo na hewa ya kutosha, fungua au legeza nguo zote alizovaa. Kama huna ujuzi toa mwito haraka kwa watoa huduma ya kwanza wafike. Hakikisha njia ya hewa haina mikwamo, msaidie upumuaji kwa kumpepea au kumweka katika eneo lenye hewa. Mgonjwa hulazwa katika mtindo wa kunyanyuliwa kidogo eneo la miguu kuwa juu kuliko kiwiliwili ili damu nyingi ifike katika ubongo kirahisi.

Akipata nafuu mlaze mzuri unaosaidia mwili. Ili kukabiliana na tatizo la kuzimia ina shauriwa kudhibiti msongamano, viwanja viwe na hewa ya kutosha, kujidhibiti hisia kali za kishabiki, unywaji maji mengi na mlo kabla ya kwenda mchezoni, kuongeza watoa huduma ya kwanza viwanjani na kutoa elimu ya huduma ya kwanza kwa jamii.