Wachezaji Singida United wajifunze kwa Chirwa , Bossou

Labda hadithi ya wachezaji Obrey Chirwa na sasa Vincent Bossou waliokuwa wakiichezea Yanga misimu miwili mmoja nyuma huko na kisha baada ya mikataba yao kumalizika waliamua kuondoka na kwenda nje kutafuta timu za kuchezea mbali na Yanga ambayo walikuwa pamoja, Obrey Chirwa akimkuta Vincent Bossou ndani ya klabu ya Yanga ambaye alidumu hapo kwa zaidi ya misimu miwili kisha akaondoka kwa madaha.

Haikuwa rahisi kuwaacha wachezaji hao kwa mkupuo kwa kuwa walikuwa muhimu ndani ya klabu hiyo, Vincent Bossou akicheza kama Mlinzi wa kati kwa muda mrefu akiunda ukuta wa pamoja yeye na ama Kelvin Yondani au Nadir Haroub na kuipa mafanikio klabu hiyo huku Obrey Chirwa akicheza nafasi ya Mbele na kwa nyakati tofauti tofauti akifanikiwa kufunga goli kadhaa ndani ya klabu hiyo, wachezaji wote hao wawili waliikuta Yanga ikiwa na neema kubwa huku wakilipwa mishahara mizuri chini ya ufadhili wa tajiri Yusuf Manji, kwa ujumla walifaidi sana maisha ya furaha ndani ya uwanja chini ya kocha Hans wakipata mafanikio makubwa kiasi na nje ya uwanja maisha yakiwa mazuri.

Ghafla matatizo yaliyompata tajiri na Kiongozi wao Mkuu bwana Yusuf Manji yaliyomfanya ashindwe kuihudumia klabu yalipelekea kubadili sura ya klabu kwa kila eneo, mishahara ikaanza kuchelewa au kutolipwa kabisa kwa kipindi kirefu na kuyafanya maisha ya wachezaji kuwa magumu, Obrey Chirwa na Vincent Bossou wakiwa kama wachezaji wa kulipwa kutoka nje hawakuweza kuvumilia kila mishahara ilipochelewa nao pia waligoma kucheza wakiwa wanashinikiza kulipwa mishahara yao hawakujali mchezo uliokuwa Mbele yao uliokuwa wa kimataifa au wa ligi, walifikia kugoma hata kucheza mchezo dhidi ya Simba hawakujari kabisa! Ni kweli walikuwa wanahaki ya kulipwa mshahara au mishahara lakini hawakutaka kukubaliana kwa muda na hali iliyotokea. Hali hii ndio iliyowapelekea viongozi wa Yanga kugoma kuwaongeza mikataba pindi ilipokuwa imekwisha licha ya kuwa walikuwa bado wanawahitaji na kutambua uwezo wao ndani ya klabu.

Wachezaji hao waliondoka ndani ya klabu kwanza kwa kiburi sana wakiwa na matarajio ya kupata timu nzuri nje ya Tanzania sababu walijiamini waliamini viwango vyao na hata kuwasikiliza washauri wao waliokuwa wakiwaambia ondokeni, tulilazimika kufuatilia nyendo za wachezaji hao ambao si watanzania ila kwa kuwa wamepita na kucheza kwenye ligi yetu kama ilivyokuwa kwa kina Nonda Shabani na wengine inafurahisha kusikia wakipata mafanikio.

Bahati mbaya kwa wachezaji hawa mambo yamekuwa tofauti sana yale mategemeo waliyokuwa nayo hayakwenda kama walivyotarajia, kwa Vincent Bossou siku nyingi tulishaanza kusikia habari zake za kutofanikiwa huko alikotaka kwenda na sasa akawa akisikika kuuomba uongozi wa Yanga ukubali kumpokea tena ingawa haijakuwa rahisi tena. Upande wa Obrey Chirwa mambo yake hayakukaa vizuri kabisa alikoenda huko nchini Misri matarajio yake yalikuwa kwenda kujiunga na Klabu inayocheza ligi kuu nchini Misri lakini akahangukia kwenye Klabu inayoshiriki ligi daraja la kwanza bila shaka hali hiyo ndio iliyomkatisha tamaa kuendelea kucheza na kuishi nchini Misri hadi kufikia kuomba kuvunja mkataba na kuamua kurudi Tanzania.

Chirwa hakukumbuka yale mabaya aliyofanya huko nyuma ndani ya Klabu ya Yanga, ilikuwa rahisi yeye kuona alichokuwa akikifanya huko nyuma kilikuwa halali na haki kwake, kwa soka la kidunia ni sawa ila si kwa watanzania, ingekuwa rahisi kwake kuwa kila alipokuwa akigoma na kisha kurudi anafanya makubwa kwa klabu yake bila shaka hakuna mwana Yanga ambaye angemkataa lakini alikuwa akifanya kinyume kwani licha ya migomo yake mingi lakini pale alipofanikiwa kurudi ndio kwanza alikuwa akianza upya, Chirwa aliomba kwa dhati kurudi hapo Yanga lakini alikataliwa na bahati bado anayo kwani amesajiliwa na Azam na bila shaka atakuwa akilipwa vizuri.

Haya niliyoyaeleza yakifanywa na kina Chirwa ndio ambayo baadhi ya wachezaji wa Singida Utd wameshayafanya na wengine wanategemea kuyaendeleza, kibaya zaidi wachezaji hao ndio inavyosemekana kuwa wanachukua kipengere cha kutolipwa mishahara ya miezi kadhaa kuvunja mikataba yao, ni kweli wanahaki kabisa ya kudai haki zao na kulipwa lakini kwangu Mimi naona ni kama wanaharaka sana ya kufanya maamuzi wanayoyafanya na wengine wanaelekea kufanya hivyo.

Tayari tumeshawashuhudia wachezaji watatu muhimu waliokuwa ndani ya kikosi hicho msimu uliopita wakivunja mikataba na kuondoka, ameondoka Mlinda mlango Manyika Jr akaondoka Mlinzi wa kushoto Shafik Batambuze na Mshambuliaji mzambia Mundia Lubinda sasa inasemekana Mlinzi wa kushoto Salum Chuku, Mlinzi wa kulia Miraj Adam, Jamal Mwambeleko na wengineo wanaelekea kufuata.

Bila Shaka wachezaji hawa hasa wazawa waliishi ndani ya klabu ya Singida Utd hasa waliokuwapo msimu wa kwanza toka kupanda kwa timu wakifaidi maisha mazuri kabisa yaliyofanana na ya vilabu vikubwa vya Simba,Yanga na Azam huku wakiiona Singida tofauti na timu nyingine ndogo za Stand Utd, Ndanda nk, hawajataka hata kidogo kuichukulia Singida sawa na timu nyingine, hawajataka kukubali hali halisi kuwa maisha ndani ya Klabu hiyo yamebadilika kutokana na sababu zinazoeleweka za kupungua kwa wadhamini nk

 Inasikitisha kuwaona hata baadhi ya wachezaji ambao ndio kwanza walihamia huko wakitokea kwenye timu za kawaida kabisa wanashindwa Kukumbuka kama kuna sehemu walitoka hakuna huduma za kulinganisha na hapo Singida Utd. Binafsi sina lengo la kuwashauri kuvumilia shida lakini kwa wachezaji wetu wa kitanzania hii ndio kasumba inayotufelisha hata wakienda nje ya nchi siyo wavumilivu, wanashindwa kuitumia Singida au Klabu yoyote hapa nchini kama daraja la kupitia tu kuelekea kwenye mafanikio hawawezi, hawajui kuwa leo wanaweza kuikimbia Singida Utd kesho wakataka kurudi kuitumikia hapo timu ikiwa tofauti na waonavyo leo.