STRAIKA WA MWANASPOTI : Waamuzi hawa huwa wanabeti au hawajui sheria?

Muktasari:

  • Hapa nitatoa mfano wa mcchezo wa wa Kombe la Shirikisho Afrika kati ya Gor Mahia na Hussein Dey ya Algeria. Gor Mahia ilifunga bao safi tu la kusawazisha. Refa akalikataa.

NDANI ya wiki mbili hivi nimeshuhudia visanga vingi vya kutofurahisha kutokana na maamuzi ya marefa wengi waliyoyafanya uwanjani.

Tatizo hili sio la Kenya, Tanzania au Uganda na Afrika peke yake, la hasha hili ni tatizo la dunia nzima.

Waamuzi (marefarii) wengi maamuzi yao yamekuwa si mazuri sana kwa baadhi ya timu. Yanaacha maswali mengi yanayokosa majibu.

Makosa ambayo yanazidi kufanywa kila kukicha na yanaua soka letu hususan Afrika Mashariki.

Hapa nitatoa mfano wa mcchezo wa wa Kombe la Shirikisho Afrika kati ya Gor Mahia na Hussein Dey ya Algeria. Gor Mahia ilifunga bao safi tu la kusawazisha. Refa akalikataa.

Sababu za kumfanya alikatae wala hazieleweka kwa sababu hazikuwa wazi. Hebu fikiria wakati mwamuzi anapokataa bao zuri tu na kuwaacha na maswali mengi wachezaji. Inaudhi sana.

Kumbuka timu imetayarishwa kwa muda mrefu. Kikosi kimetayarishwa kimawazo, kisaikolojia, kwa kutumia pesa nyingi, muda. Watu wamejinyima vitu vingi tu halafu refa na kipyenga chake ndani ya sekunde chache anabadilisha matokeo kwa njia isiyo ya halali. Inauma sana.

Tatizo hili limeharibu sana ligi zetu katika Ukanda wa Afrika Mashariki, inaonekana wazi timu yenye nguvu ndio inayoshinda Ligi Kuu.

Mfano Gor Mahia, AFC Leopards (enzi zake) za hapa Kenya na Simba na Yanga za Tanzania.

Kila siku timu hizi ndio zinawakilisha nchi zetu. Je, waamuzi wanatenda haki? Maana kama kweli tunataka kufanya vizuri ni lazima tuanze na kwenye ligi zetu za ndani, Afrika Mashariki. Tuhakikishe waamuzi wanafanya vizuri kwenye ligi zetu.

Nilisema tatizo hili ni la dunia, hebu angalia kwenye Ligi Kuu England, katika mechi ya Manchester United na Arsenal wa juzi Jumapili.

Mwamuzi alitoa penalti ambayo haikuwa sahihi. Hapo ndipo mechi iliharibika. Nina uhakika kama mechi ile ingeendelea ikiwa 1-0 na ile presha ya Manchester United ilivyokuwa kwa kweli ingesawazisha bao lile. Lakini upuzi kidogo tu wa yule refa alibadilisha mechi nzima.

Tazama mechi ya siku hiyohiyo ya Liverpool na Burlney, ambapo Burlney walianza kupata bao la kuongoza. Halikuwa bao sahisi kwa kuwa kipa wa Liverpool, Allison alikandamizwa chini na wachezaji wa Burnley wakati kona ikipigwa. Halikuwa bao sahihi.

Tazama pia mechi ya Jumamosi Manchester City dhidi ya Watford. Katika kipindi cha Kwanza mechi iliishia kwa sare ya 0-0.

Watford ilikuwa imejipanga kupata alama moja. Lakini punde tu kipindi cha pili, Raheem Sterling alifunga bao akiwa ameshaotea. Msaidizi wa refa aliinua kibendera kuonyesha ishara ya kuotea, lakini refa akasema ni bao.

Kuanzia hapo wachezaji wote wa Watford nyoyo zao zikafa, ndipo mvua wa mabao ikawashukia. Katika soka watu hawaelewi nyakati kama hizi, huwasononesha sana wachezaji na kuwakatisha tamaa.

Na hapo ndio huanza kupoteza umakini. Wanabaki wakijuiliza maswali mengi. Jambo ambalo huwafanyawaamini hata wakifanya nini watafungwa tu.

Wanalegeza kamba. Marefaa siku hizi ni kama pia wao wako kwa biashara za kubeti ama vipi? Tangu kuibuke na kampuni nyingi za kubeti soka letu linabadilika kila kukicha. Sheria zinabadilishwa kila wakati , hadi sasa tunaletewa VAR, chombo cha kusaidia marefa kutoa uamuzi.

Haileti furaha hata kidogo. Kama ningekuwa mimi ningerudisha soka letu palepale na kuondoa hizi kampuni za kamari katika soka letu. Soka tumewaachia maharamia sasa.

Hatuelewi chochote sasa, refa atatoa penalti ambayo wala siyo. Atawanyimana penalti dunia yote itaona. Refa atakataa bao safi, refa atahesabu bao la kuotea (off-side) bila kujali.

Sheria zinawazunguka, hakuna chochote ambacho wachezaji na benchi la ufundi wataweza kumfanya.

Imefika wakati sasa hawa waamuzi ni lazima waanze kuchunguzwa kwa undani. Nakumbuka kulikuwa na refa Pierluigi Collina. Alikuwa hana mchezo. Alikuwa anajua kazi yake. Kila wakati alikuwa katika tukio lolote uwanjani. Usingeweza kumdanganya. Hakufanya makosa ya kizembe.

Hata kama alikosea, hayakuwa makosa ya kijinga kama tunayoyashuhudia sasa. Alikuwa anaifahamu vizuri kazi yake.

Marefa kama hawa walienda wapi? Marefa bandia wamejaa kila kona. Inaudhi kuwaona wanaofaa kuongoza mechi ndio wanaharibu. Mashirikisho ya Soka ya Kenya (FKF), la Tanzania (TFF), la Uganda (FUFA) na CAF na FIFA lazima yafuatilie masuala haya kwa undani.

Marefa wa sasa ni kama wanatumiwa kuharibu mechi. Hata mtoto ambaye hafahamu sheria vizuri anabaki kushangaa mbona refa ameamua hivi wala sio vile. Je, wanakula mlungula ama shida iko wapi? Popote ulipo niko na uhakika ushawahi kushuhudia tukio ambalo linaudhi kutokana na maamuzi ya refa.

Nayaomba mashirikisho yote duniani yaungane kuangamiza ujinga huu wa marefa. Nashukuru Mungu baadhi yao wameanza kupigwa marufuku kukaribia mechi zetu.

Juzi tu refa Oden Mbaga wa Tanzania alifungiwa maisha. Kenya Aden Marwa vile vile. Nadhani iwapo wengi watafungiwa. Kwa sasa lazima tuokoe soka letu kutoka kwa mikononi mwa wacheza kamari Wakati ndio huu kabla ya kuua soka letu kabisa kwa faida ya watu wengine.