WINO MWEUSI : Uongozi Simba umtafakari upya Haji Manara

Wednesday May 15 2019

 

By Thobias Sebastian

HONGERA sana rafiki yangu Ofisa habari wa Simba Haji Manara. Hakika umeweza kutumia vizuri wafuasi wako katika mitandao ya kijamii kwenye kujitengenezea kipato. Unastahili pongezi.

Umeweza kutumia fursa hiyo kwa kufanya biashara ya kuuza pafyumu, lakini kama haitoshi kuna masilahi ambayo umeyapata kutoka katika kampuni mbalimbali kupitia umaarufu na ukubwa wa jina lako hapa nchini.

Jambo hilo ambalo umefanya lilikuwa lifanywe na uongozi wa Simba siku nyingi ili kujipatia kipato kutokana na wingi wa mashabiki wao waliokuwa nao ndani na nje ya nchi kwa kuuza bidhaa zao ambazo zingeweza kuwapatia vyanzo vingine vya mapato kipato kama zinavyofanya timu ambazo zimeendelea.

Siku moja tukiwa Zambia kabla ya mechi ya mzunguko wa kwanza Ligi ya Mabingwa Afrika ya Nkana Red Devils dhidi ya Simba nilikupongeza rafiki yangu Manara umeweza kuona fursa ndani ya Simba kutokana na wingi wa wafuasi wako kwenye mitandao ya kijamii na mashabiki wako ukawatumia kuwa chanzo cha kupata kipato.

Kingine ambacho umeweza kufanikiwa na kupewa pongezi ni ushawishi wako mkubwa ambao ulikuwa ukiufanya katika kuhamasisha mashabiki kujitokeza kwa wingi kwenda kuipa nguvu Simba katika mechi zake za Kimataifa zote ambazo waliweza kujitokeza mashabiki wa kutosha na kuujaza Uwanja wa Taifa.

Uongozi wa Simba naimani kwa hilo utakuwa umempa pongezi. Lakini unatakiwa kumwangalia Manara kipindi hiki kwani anaweza kuchangia ugumu wa timu hiyo katika kutimiza azma yao ya kutwaa ubingwa.

Advertisement

Iko hivi, Simba baada ya kurudi kutoka Mbeya, Manara alionekana kuzungumza kauli ambazo katika mechi zao tano ambazo watacheza jijini Dar es Salaam, hakuna timu itaweza kuwazuia na watatangaza ubingwa mapema kabla ya kuanza ratiba yao nyingine ya kusafiri katika mechi mbili za mwisho.

Manara alifika mbali na kuweka hadharani mpaka Mei 22, mchezo wao dhidi ya Sevilla watakuwa tayari wameshachukua ubingwa kwa hiyo kombe na zawadi zao wataomba wakabidhiwe siku ya mchezo huo wa kirafiki na timu hiyo kutoka Ligi Kuu Hispania.

Ikumbukwe msimu uliopita walipoteza mchezo mmoja dhidi ya Kagera Sugar mbali ya kuchukua ubingwa, lakini siku moja kabla ya mchezo huo Manara alipofanya mahojiano na chombo kimoja cha habari alitoa majibu ambayo ni kama Kagera hawataweza kuwafunga mbele ya Rais wa Tanzania Dkt, John Pombe Magufuli tena wakiwa wanacheza Uwanja wa nyumbani, Taifa.

Kilichotokea, Kagere waliweza kuvunja rekodi ya Simba kutopoteza mchezo wowote tangu kuanza kwa msimu uliopita kwa kuwazaba bao 1-0, lililofungwa na mchezaji wao za zamani Edward Cristopher.

Uongozi wa Simba unatakiwa kumtafakari Manara kwa namna mbili, kutokana na kauli zake ambazo zimesababisha hadi kutokuelewana na Kocha wa Yanga, Mkongomani Mwinyi Zahera.

Kauli zake ndizo zilizosababisha ugumu wa mchezo dhidi ya Kagera Sugar na Simba kufungwa bao 1-0, tena wakishindwa kuonekana kuwa na makali kama walivyokuwa dhidi ya Coastal Union.

Kauli hizi pia huenda zilichangia ugumu wa mchezo na Azam ambao ulimalizika kwa suluhu, lakini unaweza kuongeza ugumu wa michezo mitano waliyobaki nayo, kwani hakuna timu ambayo itataka kuonyesha unyonge kwa Simba jambo ambalo linaweza kuchelewesha safari ya timu hiyo kutwaa ubingwa msimu huu.

Manara anachotakiwa ni kuwa mpole hasa kipindi hiki na baada ya timu yake kutimiza malengo ya kupata pointi ambazo zitawafanya wao kutetea ubingwa wao ndio angeanza kutamba kwani hilo lina ruhusiwa katika soka.

Pia kauli hizo za Manara mbali ya kuwa zinaweka ugumu katika mechi zao lakini kwa upande mwingine zinaweza kuwa chachu kwa wachezaji na timu kwa jumla kuongezeka morali ya kushindana ili kufikia malengo ambayo yanasemwa mara kwa mara na msemaji wao.

Kwa hiyo rafiki yangu Manara hongera kwa yale ambayo ulikuwa unafanya na unaendelea kufanya kwa manufaa ya Simba lakini unatakiwa kuangalia kauli zako zinaweza kuwa na hasara katika timu kwa kuchelewesha malengo yenu ya kuchukua ubingwa, pia yanaweza kuwa chachu kwa wachezaji na timu yote kwa jumla kuongeza morali ya kupambana na kutwaa ubingwa.

Advertisement