WINO MWEUSI : Simba walikwenda Algeria wakiwa wameshafungwa

Thobias  Sebastian

Muktasari:

  • Kabla ya Simba kucheza mechi ya Jumamosi walikuwa nafasi ya pili Kundi D wakiwa na pointi sita, vinara wakiwa Al Ahly waliokuwa na saba huku nafasi ya tatu ni JSS waliokuwa na pointi tano na AS Vita wao ndio walikuwa wakiburuza mkia na pointi nne.

KWANZA nianze kuwapa pole wananchi wa Afrika Mashariki kwa msiba mzito baada ya Ndege aina ya Boeing 727 ya Shirika la Ndege la Ethiopia iliyokuwa inawenda Nairobi, Kenya kutokea nchini Ethiopia kupata ajali na kuanguka juzi Jumapili ambapo abiria na wahudumu waliokuwa humo kupoteza maisha.

Siku moja nyuma yaani Jumamosi kabla ya kutokea tukio hilo kulikuwa na mechi za hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika na ukanda huu wa Afrika Mashariki kulikuwa na mwakilishi wao ambaye anacheza hatua hiyo ya makundi.

Simba ndiye mwakilishi pekee wa Afrika Mashariki ambao walicheza dhidi ya JS Saoura, mechi ilichezwa Algeria katika Mji wa Bechor ambapo walifungwa mabao 2-0.

Simba waliwasili jana Jumanne saa 9:00, alasiri kwa Shirika la Ndege ya Emarates wakitokea nchi Algeria kupitia Dubai ambako walionekana kwenda kuwavaa Saoura wakiwa tayari wamefungwa.

Kabla ya Simba kucheza mechi ya Jumamosi walikuwa nafasi ya pili Kundi D wakiwa na pointi sita, vinara wakiwa Al Ahly waliokuwa na saba huku nafasi ya tatu ni JSS waliokuwa na pointi tano na AS Vita wao ndio walikuwa wakiburuza mkia na pointi nne.

Simba walikuwa ugenini dhidi ya JSS walikuwa na nafasi ya kushinda na kufikisha pointi tisa ambazo zingewafanya kuongoza kundi na kutafuta pointi moja tu mchezo ambao wamebaki nao dhidi ya AS Vita.

Kulingana na mchezo huo ulivyokuwa mbali ya Simba kushindwa kupata pointi tatu walikuwa na uwezo wa kupata suluhu ambayo ingewafanya wafikishe pointi saba na kuwa katika mazingira mazuri ya kupata ushindi mechi ya mwisho hapa nyumbani na kufuzu hatua ya robo fainali.

Lakini msafara wote wa Simba kuanzia wachezaji, benchi la ufundi waliamini kuwa wanakwenda kucheza mechi hiyo ya ugenini huku wakiwa na matokeo kufungwa kwani hata mechi walikuwa wanacheza kwa aina hiyo.

Mara baada ya Simba kufungwa bao moja kipa wa Simba, Aishi Manula alionekana kupooza mpira, muda mwingine alianguka na kuonekana kama ameumia lakini si pekee yake aliyefanya hivyo hata Pascal Wawa na Jonas Mkude.

Katika mechi mbili ambazo Simba wamecheza ugenini msimu huu dhidi ya JSS ni miongoni mwa mechi pekee ambayo walicheza kiwango kizuri na kufanyia kazi makosa mengi ambayo waliyafanya mechi zilizopita.

Si kama Simba hawakufanya makosa, hapana walifanya, lakini mechi na JSS walikuwa katika kiwango kizuri ambacho kama akili za wachezaji zingekuwa ni kupata ushindi katika mchezo huo walikuwa na uwezo lakini si kirahisi.

Ukweli usiopingika wachezaji, viongozi na mashabiki wa Simba akili zao imejengeka zana ya kila timu kushinda mechi zake za nyumbani jambo ambalo si sahihi kwani hata ugenini wana uwezo wa kupata matokeo tofauti na kufungwa.

Kulingana na dakika 90 za mchezo huo haikuwa mechi ngumu mno kwa Simba kama ilivyokuwa dhidi ya AS Vita na Al Ahly kwani wawakilishi hao walicheza vizuri na kama wasingekuwa na akili ya wao wanahaki ya kushinda nyumbani wangepata hata matokeo ya sare.

Simba mbali ya kwenda Algeria wakiwa wamefungwa kisaikolojia kwa kuamini wao wanaweza kupata matokeo mazuri uwanja wa nyumbani tu bado wana nafasi ya kufuzu na kusonga mbele kundi hilo.

Kama watashinda mechi ya mwisho dhidi ya AS Vita ambayo watacheza hapa nyumbani siku ya Jumamosi, watafikisha pointi tisa ambazo moja kwa moja zitawapeleka hatua inayofuata.

Simba kwenda hatua inayofuata kwangu si tatizo kwani wanaweza kufanya hivyo kulingana na matokeo ambayo wamekuwa wakiyapata uwanja wa nyumbani lakini tatizo ni mechi mbili ambazo watacheza hatua ya robo fainali.

Kama Simba watakwenda hatua ya robo fainali timu ambayo watakutana nayo watacheza nayo mechi mbili nyumbani na ugenini shida ni kwamba kama watashindwa kucheza vizuri mechi ya ugenini na kufungwa idadi kubwa ya mabao uwanja wao wa nyumbani utakuwa hauna faida tena.

Wachezaji, viongozi na mashabiki watambue ili timu yao ifaye viuri wanatakiwa kuwa na uwezo wa kupata matokeo mazuri hata kama wakicheza ugenini ili kujirahisishia kazi katika mechi ya nyumbani. Endapo Simba watafanya hivyo watafika mbali lakini wakifanya tofauti itakuwa kazi sana.

Wino mweusi inawakumbusha Simba ili kufanya vizuri katika mchezo huo wanatakiwa kuyaboresha haya ili kutimiza malengo yao, lakini kama wakiyarudia tena halitakuwa jambo la kushangaza kuona wanacheza kipigo kingine ugenini kwa mara ya tatu.