WINO MWEUSI : Simba kujikwaa si kuanguka, ijipange kwa mwakani

Muktasari:

  • Msemo huu upo katika maisha yetu ya kila siku ukiwa na maana ukikutana na changamoto ambayo imesababisha wewe kushindwa kufikia malengo hutakiwi kukata tamaa bali unatakiwa kujipanga upya uli kulifanya tena hilo jambo.

WAZEE wa zamani walikuwa na maneno na misemo mingi sana ambayo ilikuwa ikitunika katika kuelimisha jamaa au kufikisha jumbe bila ya kulitamka neno lenyewe kwa lugha ya ufasaha.

Baadhi ya misemo hiyo ilikuwa kama Simba kwenda pole ndio mla nyama, mvumilivu hula mbivu, misemo yote miwili hiyo ilikuwa na maana kuwa, ambaye anapenda kufanya kitu kwa utaratibu au kufanya kitu huku akiwa anavumilia huyo ndio mwishowe anafanikiwa. Miongoni mwa misemo mingine ya Wahenga ambao unaishi mpaka leo katika maisha yetu ya kawaida ni ‘Kujikwaa si kuanguka’.

Msemo huu upo katika maisha yetu ya kila siku ukiwa na maana ukikutana na changamoto ambayo imesababisha wewe kushindwa kufikia malengo hutakiwi kukata tamaa bali unatakiwa kujipanga upya uli kulifanya tena hilo jambo.

Msemo huo mbali ya kuwa nao katika maisha ya kila siku, kikosi cha Simba nacho kinatakiwa kuufanyia kazi ili kuweza kufanikiwa katika Ligi Mabingwa Afrika msimu ujao.

Iko hivi, Simba waliondolewa kwenye robo fainali katika Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu na TP Mazembe kwa kufungwa mabao 4-1, katika mechi zote mbili.

Simba hawatakiwi kujilaumu na kumtafuta mchawi nani kwa wao kushindwa kuwaondoa Mazembe ili kwenda kucheza hatua na nusu fainali dhidi Esperence de Tunis.

Awali malengo ya Simba Ligi ya Mabingwa Afrika ilikuwa ni kufika hatua ya makundi ambayo walifanikiwa zaidi na kilichokuwa mbele yao ni malengo ya matamanio, lakini mpango wao wa mwisho ukikuwa ni kutwaa tena ubingwa wa Ligi Kuu Bara. Hapa Simba ndio wanatakiwa kufahamu kujikwaa si kuanguka, kwa maana wanatakiwa kwanza kufanya vizuri mechi zao za ligi ili kuweza kutwaa ubingwa ili kupata nafasi ya kucheza mashindano hayo ya Kimataifa msimu ujao.

Wakishafanikiwa hilo watakuwa na uhakika wa kucheza Ligi ya Mabingwa Afrika kwa maana hiyo wanatakiwa kujipanga na kufanya yale mambo muhimu ili kuvuka hatua ya mbele zaidi ya walipoishia msimu huu. Jambo la kwanza ambalo Simba wanatakiwa kulifanya ni kumwongezea mkataba mpya kocha wao Patrick Aussems ambao mwisho wa msimu huu unamalizika.

Linaweza kuwa jambo la kushangaza kuona Simba inafanya mabadiliko ya Kocha Aussems licha ya kufikia malengo ya timu.

Jambo lingine Simba wanatakiwa kuboresha benchi la ufundi mbali ya kuwepo na kocha mkuu lakini wanatakiwa makocha wengine wa kumsaidia Aussems, Mkurugenzi wa Ufundi na hata wataalamu wa saikolojia. Kama wakiweza kuboresha benchi hilo la ufundi kuwa na wataalamu wa kiufundi zaidi ya saba waliokuwepo sasa nguvu na uimara wa timu hiyo utaongezeka msimu ujao katika Ligi ya Mabingwa Afrika na mashindano yote ya ndani.

Baada ya kuwa na benchi la ufundi pana zaidi na Aussems kupewa mkataba mpya wanatakiwa kufanyia kazi marekebisho ya kikosi kwa kufanya usajili wachezaji wenye uwezo. Aussema ndio atakuwa wa kwanza kueleza kutokana na Simba alivyo msimu ataka wachezaji wa maeneo gani na wenye sifa zipi na hata muda mwingine anaweza kuwaweka majina yao na kuwapa viongozi ili wasajiliwe.

Kwa maana hiyo usajili wa Simba ambao wanatakiwa kufanya msimu huu ni ule wa mahitaji ya timu kulingana na kocha alivyosema lakini si kufanya usajili wa sifa au kuwakomoa timu nyingine kwa kuwa wao wanamtaka mchezaji fulani. Simba hawatakiwi kufanya hivyo wameshapita katika aina hiyo ya kufanya usajili.

Binafsi Simba msimu huu mbali ya kuonyesha makali katika ligi ya ndani lakini kikosi hicho kinatakiwa kusajili kulingana na eneo husika kuanzia mabeki, viungo na washambuliaji wa viwango vya juu wanaocheza vikosi vya kwanza kama klabu za TP Mazembe, As Vita. Mamemod Sandowns na nyingine kunwa hapa Afrika.

Simba kama wanashindwa kuwa na maskauti kama zilivyo timu za nje au hapa Afrika zilizoendelea wawatumie hata makocha na wachezaji waliopita katika timu hiyo zamani kuwafatilia hao wachezaji na kuwapa taarifa kuwa kweli anafaa ua hafai.

Suala lingine Simba wanatakiwa kufanya uwekezaji kwa maana ya kutafuta chanzo vingine vya pesa ili timu yao kuwa na nguvu ya kulipa mishara, bonansi mambo muhimu ndani ya klabu kwenda vizuri.

Kama Simba wataweza kuyafanya hayo mambo kwa ufasaha ndio wataweza kuelewa maana ya kujikwaa si kuanguka yaani mbali ya kuondolewa katika hatua ya nusu fainali Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu msimu ujao watafanya vizuri lakini ikiwa tofauti na hapo kwa kufanya mambo ambayo hayakuwa na ulazima mafanikio watayasikia kwenye bomba katika mashindano yote.