Van Der Sar amfuata Mbappe wa Bongo

Muktasari:

  • Uamuzi wa Ajax inayoshiriki Ligi Kuu ya Uholanzi kumtuma Van Der Sar umekuja baada ya kukoshwa na kiwango bora kilichoonyeshwa na mshambuliaji huyo katika majaribio ya wiki moja aliyoyafanya kwenye timu ya vijana ya Ajax Cape Town ya Afrika Kusini ambayo ni tawi la klabu hiyo ya Uholanzi.

NYOTA wa Serengeti Boys, Kelvin John ‘Mbappe’ inazidi kung’aa baada ya uongozi wa klabu ya Ajax Amsterdam ya Uholanzi kumtuma kipa wa zamani wa Manchester United na Uholanzi, Edwin Van Der Sar kuja kufanya mazungumzo na wakala anayemsimamia mchezaji huyo.

Uamuzi wa Ajax inayoshiriki Ligi Kuu ya Uholanzi kumtuma Van Der Sar umekuja baada ya kukoshwa na kiwango bora kilichoonyeshwa na mshambuliaji huyo katika majaribio ya wiki moja aliyoyafanya kwenye timu ya vijana ya Ajax Cape Town ya Afrika Kusini ambayo ni tawi la klabu hiyo ya Uholanzi.

Katika majaribio hayo, Kelvin John (15) ambaye ndiye mshambuliaji nyota na tegemezi wa Serengeti Boys alifunga mabao mawili katika ushindi wa mabao 3-1 wa kikosi cha vijana cha Ajax Cape Town dhidi ya timu ya vijana Mamelodi Sundowns.

Kelvin aliliambia gazeti hili Ajax Amsterdam wanataka kumsajili moja kwa moja baada ya kukoshwa na kipaji chake ingawa atalazimika kucheza kwa muda kwenye kikosi cha vijana cha Ajax Cape Town.

“Kwenye yale majaribio niliyofanya wiki hii, nilifunga mabao mawili kwenye mechi yetu dhidi ya kikosi cha vijana cha Mamelodi, sasa nimeambiwa nitacheza hapa Afrika Kusini hadi pale nitakapofikisha miaka 17 na baada ya hapo ndipo nitaenda Uholanzi kwa sababu wanataka niimarike zaidi.

Hata hivyo, wiki ijayo wamemtuma Van Der Sar akutane na wakala wangu huku Afrika Kusini kwa ajili ya kuingia makubaliano kwani wamesikia pia nimeshafuzu kule Denmark,” alisema straika huyo.

Kelvin aliyechukua tuzo ya mchezaji bora wa mashindano ya kuwania kufuzu fainali za mataifa ya Afrika kwa vijana wenye umri usiozidi miaka 17 mwakani kwa upande wa Kanda ya Afrika Mashariki na Kati, alisema pia ametumiwa tiketi na timu za Lazio na Napoli ili kwenda kufanya majaribio kwenye vikosi vyao vya vijana.