STRAIKA WA MWANASPOTI : United impe tu Solskjær ukocha wa kudumu

Muktasari:

  • Leo namzungumzia kocha wa muda pale, Manchester United, Ole Gunnar Solskjær. Kocha mchanga aliyepewa mikoba baada ya Kocha Jose Mourinho kupigwa kalamu kufuatia msururu wa matokeo mabaya tangu msimu uanze.

LIGI Kuu England inazidi kushika kasi timu zikitoana jasho hasa kwenye timu sita Bora zikiwemo Liverpool, Manchester City, Tottenham, Chelsea, Arsenal na Manchester United.

Kuna vita kali sana katika mbio za kuwania nafasi za nne bora kwani timu nne za mwanzo hupata uwakilishi wa Ligi ya Mabingwa barani Ulaya.

Leo namzungumzia kocha wa muda pale, Manchester United, Ole Gunnar Solskjær. Kocha mchanga aliyepewa mikoba baada ya Kocha Jose Mourinho kupigwa kalamu kufuatia msururu wa matokeo mabaya tangu msimu uanze.

Ole Gunnar alipewa jukumu hilo na kufikia sasa kwa kweli yale ambayo ameyafanya ni makubwa. Kocha huyo amepiga ushindi wa mechi sita mfululizo.

Ndani ya mechi hizo ambazo amekuwa kocha wa muda ameshinda zote jambo ambalo limewashangaza wengi sana.

Hakuna mtu aliyetarajia. Juzi Jumapili angeweza kuipiga Tottenham nyumbani kwao katika Uwanja wa Wembley bao 1-0. Wakati Ole Gunnar akichukua mikoba hiyo Man United ilikuwa zaidi ya alama nane nyuma ya Arsenali ambayo ipo katika nafasi ya tano.

Lakini sasa timu hiyo iko alama sawa na Arsenali. Alama 41. Alama sita tu nyuma ya Chelsea na alama 16 nyuma na viongozi wa ligi hiyo, Liverpool.

Mechi ambazo zimechezwa kufikia sasa ni 22. Zimebaki 16 kumaliza ligi na kumpata bingwa. Hapa naamini chochote kinaweza kutokea kwa kasi hii ambayo Ole Gunnar Solskjaer. Iwapo Ole Gunnar ataendelea na mziki huu, basi kazi ipo kwa hizo timu tano zinazoongoza ligi hiyo.

Wachezaji wa Man United wamejituma vilivyo. Paul Pogba kiungo hodari mno anakipiga bila presha tofauti na siku za nyuma.

Kila mchezaji pale anafanya kazi yake vilivyo. Katika mechi ya Tottenham Pogba alipiga pande la pasi lililo zalisha bao safi likufungwa na kinda Rashford. Kipa De Gea alilinda lango wa Man United akiokoa mabao zaidi ya 10. Kazi aliyofanya katika mechi hiyo kwa kweli inazidi kupaisha nyota yake.

Kipa huyo anabakia kuwa bora duniani. Alikuwa katika kila tukio katika eneo lake la kazi. Aliokoa mipira ambayo kila mtu alikuwa anajua Man United inafungwa. Aisee kipindi cha pili Tottenham iliwasha moto lakini De Gea alikuwa anauzima kila kukicha.

Harry Kane hakuamini De Gea alipopangua mikwaju yake yote minne. Alibaki tu akitabasamu. Man United ni kama ndio imeanza msimu sasa. Kuondoka kwa Mourinho kumechangapia pa kubwa. Alikuwa kocha mkali kwa wachezaji wake.

Hakutaka kuwapa muda wa kupiga kazi na kujibamba. Man United ilikuwa imebaki timu ya kupigwa na kila mtu. Haikuwa inashambulia.

Kazi kubwa ilikuwa ni kuzuia tu. Katika soka sisi husema njia safi ya kuzuia ni kushambulia.

Usipofanya hivyo, basi unabaki kuwa bwege tu. Utapigwa mafuriko hadi ukose la kufanya. Ole Gunnar Jambo ambalo amelifanya ni kuwapa nguvu vijana wake wacheze soka. Washambulie.

Kuzuia kupo katika soka lakini lazima uzuie pia ukisaka ushindi. Utashindaje bila kuzuia. kwa sasa timu bora ndani ya mwezi ambao umepita nadhani ni Man United. Tuzo la Kocha Bora lazima imuendee Ole Gunner. Ningekuwa na uwezo ningemkabidhi kabisa kmikoba ili awe kocha mkuu wa Man United. Hamna haja ya kuleta kocha mwingine. Sioni haja kwani Ole ameshazoeana na wachezaji.

Wachezaji bila uelewano kazi haitafanyika. Lazima kocha awe na uhusiano mzuri nao. Sidhani Kuna kocha mwingine atakayewezana na klabu hii. Ole amekuwa mchezaji pale akiwa chini ya Sir Alex Ferguson. Anaelewa nini klabu hiyo inahitaji. Mashabiki kote duniani niko na uhakika wana imani na Ole Gunnar. Kwa mda mfupi tu amebadilisha kikosi cha klabu hiyo kutoka kwa wazoefu wa kufungwa hadi kwa wazoefu wa kushinda. Mziki unaendelea.

Wakati huo huo natuma pongezi zangu kwa Klabu za Gor Mahia (Kenya), Simba Sports Club ( Tanzania) kwa ushindi wao katika mechi za kuwania ushindi barani Afrika.

Ushindi wa Gor Mahia katika Kombe le Shirikisho na Simba kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika unatueka vizuri kwenye chati la soka barani Afrika. Lazima tuzidi kuziombea zizidi kufanya vizuri.