Udanganyifu kama huu usifumbie macho ili kuliepushia aibu taifa

Thursday May 10 2018

 

KUNA baadhi ya mambo yamekuwa yakifanyika kwenye michezo na kutia doa sekta hiyo, kiasi cha kuchangia kuwakimbiza wadhamini na wafadhili wenye nia ya kujitolea.

Bahati mbaya ni kwamba matukio mengi yamekuwa yakijiri kwenye soka na kusababisha wakati mwingine kuupa wakati mgumu mchezo huo na hasa klabu shiriki katika kufanikiwa malengo yao.

Migogoro ya kiuongozi, mkanganyiko wa katiba na hata malumbano na vita baina ya wanachama kwa wanachama ama viongozi kwa viongozi ni baadhi ya sababu zilizofanya baadhi ya klabu na vyama kushindwa kusonga mbele katika soka.

Ubabaishaji na tabia ya mazoea waliyonayo nayo wadau wa soka yalikwamisha mambo mengi, ikiwamo kuwakimbiza wadhamini na wafadhili wengine kama ambavyo hivi karibuni tu, kampuni ya Acacia iliyokuwa wadhamini wa Stand United walivyokimbia.

Hata hivyo vimbwanga kama hivi vilimekuwa vikileta athari kwa klabu husika na wadau wake na wakati mwingine kwa chama husika kinachotokea klabu husika, hali ni tofauti kwa michezo mingine jambo lolote humgusa moja kwa moja mchezaji husika.

Kwa mfano, bondia yeyote akifanya udanganyifu wowote ama kuharibu katika mchezo huo, anayeumia ni mhusika moja kwa moja kama ilivyowatokea baadhi ya mabondia wenye majina makubwa kukwama kusafiri kwa sababu hizi na zile za kibabaishaji.

Wanariadha nao wamekujikuta wakiadhibiwa kwa udanganyifu wanaoufanya kwenye mashindano mbalimbali, kama ilivyowahi kushuhudiwa kwa nyota kadhaa nchini akiwamo Sarah Ramadhani na wenzake wawili kufungiwa kwa tuhuma za kutumia dawa zilizopigwa marufuku michezoni.

Sarah alishamaliza adhabu yake, wakati wenzake wawili, Eliah Daud na Msandeki Mohammed wakiendelea kutumikia adhabu yao ya miaka minne kila mmoja waliyopewa mwishoni mwa mwaka jana kwa kosa hilo.

Hata hivyo, wakati Watanzania na hasa wadau wa riadha wakianza kusahau matukio hayo mwishoni mwa wiki hii, mwanariadha mwingine wa Tanzania, John Leonard amegeuka kituko baada ya kufanya udanganyifu wa aina yake.

Inadaiwa kuwa, mwanariadha huyo alifanya hila ya kudandia bodaboda na kuibuka mshindi wa pili kabla ya kushtukiwa na wanariadha wenzake hususani Wakenya na kujikuta akipokwa nafasi yake ya pili aliyoshinda na kupewa ya nne.

Wakati mwingine unaweza kudhani hii ni hadithi ya kubuni ya kuchangamsha baraza, mwanariadha anayeiwakilisha nchi katika Mashindano ya kimataifa ya Mbeya Tulia Marathoni anapoamua kurahisisha mbio kwa kupanda pikipiki ni kituko cha mwaka. Udanganyifu huu sio tu umekuwa ni aibu kwa mhusika, lakini pia ameliaibisha taifa mbele ya wanariadha wa kigeni na washiriki wengine wa mbio hizo za Tulia.

Mwanaspoti mpaka sasa limeshindwa kuamini, ilikuwaje mwanariadha huyo aliamua kufanya udanganyifu huo, ilihali anatambua kuwa ni rahisi kubainika hata kwa wanariadha wenzake.

Awali ilidhaniwa ni ulalamishi wa Wakenya tu katika kutaka kujihakikishia ushindi wa pili wa mbio hizo, lakini ilibainika ni kweli Leonard alifanya faulo ambayo haikubaliki michezoni na bila shaka amejikweka katika hatari ya kuadhibiwa bila kupenda. Tunaamini, hiki kilichotokea Mbeya hakitaweza kutokea tena katika mchezo huo wa riadha na hata michezo mingine. Hii ni aibu kubwa na haikubaliki michezoni.

Unaweza kujiuliza kama mwanariadha huyo hakushtukiwa ina maana zawadi ya ushindi wa pili aliyokuwa amepewa awali angeibeba bila kustahili na huu ni udanganyifu mbaya pengine kuliko ule unaotokea kwenye soka wa wachezaji kujisajili mara mbili katika msimu mmoja.

Tunaamini Shirikisho la Riadha Tanzania (RT) litachukua hatua stahiki kwa mhusika ili kutoa fundisho kwa wanariadha wengine wenye kulazimisha ushindi kwa njia za hila na mambo hayo pengine ndiyo yanayokwamisha wanariadha wetu kutamba kimataifa.

Kama mwanariadha anaamua kudanganya nyumbani tena katika mbio zisizo na ushindani mkubwa kama hizo za Tulia ambazo ndizo zinaanza kuchanganya na kupata umaarufu, vipi angeshiriki mashindano makubwa na kufanya udanganyifu huo?

Hatuna nia ya kumhukumu Leonard kwa tuhuma hizo, lakini maadamu imebainika aomba radhi Watanzania na RT imuonye kwa kosa hilo.