Uchaguzi Leopards uwe darasa soka Afrika Mashariki

Wednesday June 5 2019

By Boniface Ambani

NIMEKUWA nikishuhudia mengi kwa viongozi wa soka hapa nchini. Ni kama wengi wao wameugeuza mchezo wa soka kuwa mali zao binafsi pale tu wanapoingia madarakani.

Wamekuwa hawazingatii sheria za ofisi walizoingia na hata sheria za nchi kwa jumla. Hii inaonyesha wazi hawajui nini maana ya uongozi.

Ngoja niwaambie. Kiongozi mzuri ni yule ambaye awapo uongozini anahakikisha mambo yanakwenda vizuriri. Anayeepuka mambo kama vurumai kuanzia anapoingia madarakani hadi anatoka. Hata hivyo, kwenye soka la nchi za Ukanda wa Mashariki kumekuwa na shida kubwa.

Kwa mfano ni klabu ya Kenya ya AFC Leopards. Kwa muda mrefu imekuwa na matatizo makubwa katika uongozi wake na kumekuwa na msururu wa kesi mahakamani.

Hata hivyo, kumekuwa na mambo yasiyoeleweka kutokana na uongozi kutokuzingatia sheria za uendeshaji klabu.

Wakati wapo mamlakani hawataki kufanya vitu kwa njia nzuri. Shida nii kwamba hawajui siku za usoni, sheria ambazo walipaswa kuweka ofisini kusaidia klabu ndizo hizo zitakuja kuwaponza baadaye.

Kesi ambazo zipo kortini zote hazijawahi kufuatiliwa na viongozi ambao wapo mamlakani. Wamezipuuzilia mbali. Ni vyema wakati wowote ule, ukiwa uongozini uwaambie wananchi ukweli, wabaki wakijua kiongozi wetu alituambia jambo hili na lile halikufanyika kwa sababu ya kitu fulani kilituzuia kutekeleza majukumu yetu.

Uchaguzi wa klabu hiyo umeshawadia. Uchaguzi ambao umekuwa gumzo kila kona ya nchi kama ulivyokuwa ule wa Yanga ya Tanzania.

Kubwa zaidi linaloumiza wengi hasa mashabiki wa timu hiyo na wanachama ni katiba ya klabu hiyo. Katiba imekuwa kizungumkuti na ilitakiwa ifanyiwe marekebisho na hadi sasa katiba hiyo ya mkwaka 2017 haijapitishwa.

Kuna baadhi ya vipengele viongozi waliambiwa warekebishe lakini ni kama hawakuigusa kabisa. Inashangaza kidogo. Sasa wanachama hawajui ni katiba gani itatumika huku kisheria ikijulikana wazi, huwezi kutumia katiba ambayo haijaidhinishwa kufanya uchaguzi.

Ni vyema sheria ikafuata mkondo wake ili kuepuka malumbano na siasa zisizo na tija tunazozishuhudia kwa sasa kwenye soka letu. Soka sio siasa. Viongozi wetu wote wameingiza siasa katika soka letu. Wanaendesha hizi klabu kama mali yao binafsi.

Naamini viongozi bora huacha misingi mizuri nyuma wakati wanapostaafu ama wakati wapo mamlakani.

Ukipata kiongozi ambaye ameondoka mamlakani na baada ya siku mbili tu ama mwezi mmoja yanajitokeza matatizo, jua huyo kiongozi sio mzuri hata kidogo.

Haifai ukiacha uongozi ama hata usafiri tu kwa muda kila kona iko shida. Hapo Sasa ndipo unapo jua uongozi wako ni mbovu.

Kukiwa na mikakati na misingi imara kwenye uongozi pamoja na miundombinu ni wazi9 utakuwa kiongozi bora wa kujivunia miaka nenda miaka rudi. Kiongozi mzuri ni yule anayekumbukwa na wengi wakipendelea laba angerudi tena madarakani baada ya muda wake kuisha kutokana na uongozi wake imara.

Hata hivyo, huwa najiuliza, ni nani anayewachagua haoi viongozi? Ni sisi wenyewe. Hivyo, ni wazi wa kulauiwa ni wananchi wenyewe kwani wengi wao wamekuwa wakipewa hongo ili tu kuwapitisha na matokeo yake ni hushuhudia madudu yanayofanya na hao viongozi.

Hapa sasa wananchi wanabaki wakilia na kumlaumu kiongozi. Haya sasa mashabiki na wanachama wa Leopards, uchaguzi ndio huo, wakufanya maamuzi ni nyie yatakayosaidia klabu yenu.

Baada ya kukwama kwa muda, ni wakati sasa wa kusonga mbele. Wewe kama mpigakura, chagua kiongozi ambaye unajua atapiga kazi na kuangalia masilahi ya klabu na si ya kwake.

Kiongozi ambaye ataangalia masilahi ya wachezaji kwani wao ndio hasa wanaoifanya klabu kuwa klabu na kazi wanaoifanya ni kubwa kuliko hao viongozi katika kuiangaza klabu.

Usije ukajilaumu baadaye ndugu yangu. Chagua kiongozi sahihi ufikapo kupiga kura. Piga kura kwa kutumia akili yako na ueledi wako wa kisoka. Siku njema ndugu zangu.

Advertisement