NINAVYOJUA : Tutawamaliza waamuzi tukitaka kuwahukumu kwa kila kosa

Muktasari:

  • Ingawa siku ile binafsi niliutizama ule mchezo mara nyingi nikapata nafasi ya kurudia ule mkanda roho ikawa inanisuta tu, sikuona makosa ya makusudi kutoka kwa Mwamuzi huyo, maksi alizopata kuwa alichezesha chini ya kiwango ilinifanya nishangae zaidi sababu kuchezesha dakika tisini vizuri alafu ukahukumiwa kutokana na makosa mawili tu ni uonevu.

IMEPITA misimu kama minne hivi nakumbuka toka Mwamuzi, Abdalah Kambuzi ahukumiwe kusimama kuchezesha mechi kadhaa na kamati ya masaa 72 , hukumu ile ilitokana hasa na msukumo wa mashabiki na vyombo vya habari ambao kwa pamoja walishajigeuza wasaidizi au washauri wa Kamati inayotoa hukumu.

Ingawa siku ile binafsi niliutizama ule mchezo mara nyingi nikapata nafasi ya kurudia ule mkanda roho ikawa inanisuta tu, sikuona makosa ya makusudi kutoka kwa Mwamuzi huyo, maksi alizopata kuwa alichezesha chini ya kiwango ilinifanya nishangae zaidi sababu kuchezesha dakika tisini vizuri alafu ukahukumiwa kutokana na makosa mawili tu ni uonevu.

Bwana Kambuzi siku ile alihukumiwa kutokana na msukumo tu kutoka kwa wadau ambao kwanza walishaichoka Yanga ambayo ilikuwa inashinda tu unajua ukishinda sana nako watu huchukia, hivyo kwenye mchezo huo ambao Yanga iliwafunga Coastal Union mabao 2-0 na kuingia nusu fainali ya kombe la Azam Sports Federation Cup huku, Abdalah Kambuzi akionekana kwanza kulikubali goli la Hamis Tambwe aliyeonekana kufunga kwa Mkono huku Mwamuzi akiwa amezibwa bila kuona na hata zile kamera za Azam Tv zilishindwa kutusaidia kumuonyesha kweli Tambwe akishika na kufunga. Pili Mwamuzi huyo alionekana kumuacha, Oscar Joshua salama baada ya kumpiga mchezaji wa Coastal Union akiwa bila mpira, yote hayo yalimfanya Mwamuzi huyo kuhukumiwa tena haraka sana.

Msimu uliopita kwenye pambano la watani wa jadi Simba dhidi ya Yanga timu hizo zikimaliza kwa sare ya bao 1-1 na Mwamuzi wa kati, Elly Sasii alituhumiwa na upande wa Simba kuwa aliwanyima penati iliyoonekana kufanywa na Kelvin Yondani kuwa aliushika mpira huku Mwamuzi huyo akiwa karibu na mchezaji, tafsiri ya haraka haraka ya Mwamuzi ilikuwa mpira uliufuata Mkono lakini mashabiki na Wana habari wengi walisimamia kwenye makosa ya Mwamuzi kutoliona tukio hilo.

Hiyo iliwafanya wenye maamuzi kumuondoa kwenye listi ya waaamuzi msimu huo, licha ya kuwa ndiye Mwamuzi bora kwenye ligi yetu akiwa na begi ya Fifa, Mwamuzi aliyeonekana kufanya kosa moja tayari alibebeshwa mzigo, sababu tu anachezesha mchezo unazigusa timu tuzipendazo.

Juzi tu hapa tumeshuhudia makelele mengi kutoka kwa watu mbalimbali wadau wa soka waandishi wa habari na hasa wale wanaoishi ndani ya mitandao ya kijamii wakimzungumzia Mwamuzi aliyechezesha mchezo uliozikutanisha JKT Tanzania dhidi ya Simba kwenye uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga na Simba kushinda maboa 2-0, wameshaanza kumyoshea kidole Mwamuzi wa siku hiyo, Mbaraka Rashid kuwa aliwauma JKT na alishindwa kutoa penati iliyokuwa itokane na Mlinzi, Erasto Nyoni kuonekana kuushika mpira ndani ya eneo lake, lakini Mwamuzi hakuonekana kuliona kosa hilo, tayari tunataka kumuhukumu, Mbaraka kwa kosa hilo moja huku akifanya vizuri kwenye maeneo mengi ndani ya dakika 90.

Haitowezekana kabisa Mwamuzi kutofanya kosa au kuonekana kufanya kosa sababu ndani ya dakika 90 kuna matukio mengi huweza kutokea yapo yale ya kiufundi ambayo pengine hata wachezaji huyafanya wengine hufungisha, wengine hukosa kufunga kwenye nafasi zinazoonekana za wazi wakiwa wamebaki na goli tu lakini bado hawafungi lakini ikitokea kwa Mwamuzi kufanya kosa, tayari kila mshabiki mdau wa soka hukimbilia kumkosoa Mwamuzi na kutaka wafungiwe tutawafungia kila siku huku tukishindwa kuwarekebisha uwanjani, tunawaondoa na kuwapa adhabu bila kuwarekebisha.

Hawatakiwi kufundishwa kuchezesha kwa mapenzi ya Usimba na Uyanga walikuwa wakielimishwa kutoona Unyumbani na Ugenini, nilikuwa nikiwaona vijana hawa pindi wakichezesha kituoni mfano pale Twalipo hungeweza kuiona timu mwenyeji kama Transcamp ikicheza mechi ya kirafiki ndani ya ile kambi ikipendelewa na hawa vijana haikuwa rahisi zaidi wao ndio waliokuwa wakilalamika kuminywa na hao vijana wanafunzi wa Uamuzi hii ndiyo dhana ya usawa waliokuzwa nayo hadi hivi Leo sasa iwapo wanafanya makosa basi vizuri wakaelimishwa ili waendelee kuongeza ubora

Hivi sasa tuna kundi kubwa la waamuzi vijana wengi wakiwa wamelelewa kwenye vituo vya kukuza na kufanyia mazoezi kama kile cha Twalipo kile cha Azam na vinginevyo hawa wanahitaji kulelewa na kuendelezwa kwa kushauriwa kuelekezwa na kukosolewa kwa utaratibu siyo kulaaniwa na kunyoshewa vidole.