Tusiishie kuburudika tu, tujifunze kwa wenzetu

Friday June 22 2018

 

SAFARI ya Kombe la Dunia ikiwa ni makala ya 21 imeanza siku tisa zilizopita na vigogo 32 wanaendelea kujaribu kufanya kile walichokusudia japo timu za Afrika zimewaangusha Waafrika.

Macho na masikio ya wapenda soka duniani yapo Russia, kwa kipindi kisichopungua mwezi mzima kitaendelea kuwa na agenda moja kubwa kila sehemu kuhusiana na yanayotokea kwenye fainali hizi za Fifa.

Tangu kuanzishwa kwa michuano hii rasmi na yakaitwa Kombe la Dunia la Fifa (Fifa World Cup) mwaka 1930 ni takribani miaka 88 iliyopita, hongera kwake muasisi wa michuano hii Rais wa awamu ya nne wa Fifa raia wa Ufaransa, Jules Rimet aliyekaa madarakani kwa muda mrefu kuliko marais wote waliohudumu kwenye shirikisho hilo tangu kuanzishwa kwake mwaka 1904.

Kiongozi huyu aliiongoza Fifa kwa miaka 33 na siku 297, hatujui huenda atakuja kutokea mwingine lakini mpaka sasa kati ya marais 11 waliopita haijatokea.

Mawazo ya Rais huyu kwa wakati ule yametuwezesha sote ambao hatukumuona au kumfahamu tuendelee kukiona kivuli chake katika njia bora na sahihi kama tunavyoshuhudia kipindi chote hiki cha fainali hizi.

Wakati michuano ikiendelea kushika kasi tunazidi kuyaona mabadiliko na maendeleo yanayokuja kwa kasi katika kuleta mapinduzi katika mchezo huu maarufu wa soka.

Licha ya kuongezeka kwa matumizi ya tekinolojia katika kufanya mambo mfano teknolojia ya kumsaidia mwamuzi ( VAR ), lakini pia timu zikizidi kuongezeka kutokana na maendeleo makubwa katika maisha ya kila siku ya binadamu,idadi ya watu na hivyo kuwafanya wakuu wa shirikisho hili kulazimika kubuni na kufikiri mambo mapya yatakayolandana na wakati uliopo, matahalani fainali za kwanza za Kombe la Dunia zilishirikisha timu 14 na sasa kuna timu 32.

Kama vile haitoshi, Fifa chini ya uongozi wa rais wa 12 aliyeko madarakani, Gianni Infatino, tutashuhudia fainali za 2026 timu zikiwa 48.

Katika kila jambo duniani, huwa kuna kipimo kwa ajili ya kubaini kiwango cha juu au cha chini cha mafanikio, katika soka kipimo sahihi na cha mwisho kabisa kwa nchi kupima kiwango cha mafanikio ni kushiriki fainali za Kombe la Dunia na kwa wachezaji siku zote wana ndoto za kushiriki fainali hizi.

Kwa jumla huwa ni historia isiyosahaulika,bila kujali ni lini kila mtu au mashirikisho ya soka kwa kushirikiana na serikali zao daima wanaendelea kupata taabu kwa kupanga mipango, kufanya mambo mbali mbali kwa imani kwamba ipo siku watatimiza ndoto zao. Kwa hapa nyumbani watanzania hawako nyuma katika kufuatilia michuano hii mikubwa kabisa inayowakutanisha wababe wa soka waliofanikiwa kukata tiketi zao mapema kwenda Russia kutoka mabara yote sita.

Msisimko mkubwa katika michuano hii kwa miaka yote mara nyingi unatokana na mkusanyiko mkubwa wa nyota wa kandanda wanaounda vikosi vyao vya taifa, ni jumuiko ambalo kwa wakati mmoja linasababisha kuwaona wachezaji nguli na mahiri duniani wakionyesha uwezo kupitia mechi mbali mbali kuanzia hatua ya makundi hadi fainali.

Hali hii inazua mijadala kwa wapenda mijadala na ubishi mwingi miongoni mwa mashabiki wakitaka kufahamu nani ni zaidi ya mwingine, mfano mwaka huu nani bora kati ya Messi, Cristiano Ronaldo na Neymar Jr na wengineo. Kwa ujumla hiyo ni miongoni mwa burani iliyopo kwenye michezo.

Wakati hayo yote yakiwa yanaendelea Watanzania tunajifunza nini? Nina hakika kwa wachezaji, viongozi wa shirikisho, wapenzi na mashabiki wanayo mengi watakayoyaona na kuyachukua kama njia na sehemu ya kupata mabadliko chanya ili na sisi siku moja tuwe wawakilishi wa bara la Afrika, hili ni jambo linalowezekana iwapo tutayatumia mashindano haya makubwa duniani kama darasa ama shule kwetu. Ni wazi kwamba walio wengi wanaofuatilia michuano hii ni kwa ajili ya kupata burudani hivyo mapokeo yao na jinsi wanavyoutazama mpira ni kwa ajili ya kufurahi na kuburudika, lakini ninadhani wakati umefika tusiendelee kuwa watazamaji wa burudani, bali watazamaji wenye macho ya kutaka kupata maarifa ili tuone jinsi ya kuujenge mpira wetu.

Yapo mengi sana ya kujifunza yanayohitaji utaalamu hivyo wale wote wenye dhamana ya maendeleo ya soka hapa nchini wawe makini kuyaona hayo ili wayapatie tafsiri ya kitaalamu kwa lengo la kuyajengea hoja za kitaalamu kwa ajili ya kuyafanyia kazi kwa muktadha (context) wa mazingira na mahitaji ya Kitanzania.

Kwa idadi yetu na wingi wetu kama wapenzi wa mpira tuanao wajibu wa kujaribu kuyaona yale mengine ya kawaida ambayo kwa macho na kwa akili ya kawaida tukiyaona tunapata majibu ya moja kwa moja kutoka kwenye luninga ambayo katika maisha ya kawaida ya mpira ni mambo muhimu sana kwa faida na maendeleo ya mchezo hapa nchini.

Tunaelewa mengi ambayo katika soka letu hayapo lakini leo hii wakati kombe la dunia likiendelea tunayaona,kwa kuyataja machache tu ni haya yafuatayo; nidhamu ya kiwango cha juu ya wachezaji inayowafanya waamuzi kufanya kazi yao vizuri, moyo wa uzalendo wa kuzipigania nchi zao mfano (Tunisia, Iceland, Russia, Mexico),kufanya kazi kama timu na kwa kujituma na hizi ni tabia za wachezaji ambazo hazihitaji nchi kuwa na uwezo mkubwa kiuchumi ni matokeo ya wachezaji kujitambua na kujua wajibu wao,kazi yao na dhamana waliyopewa na wananchi wao.

Wajibu wetu na jukumu letu kubwa liwe ni kutamani kupata maendeleo katika soka, hakika inasikitisha kuona nchi ndogo kama Iceland yenye idadi ya watu wasiozidi laki tatu na nusu wamefanikiwa kucheza fainali za kombe la dunia kwa mara ya kwanza na siyo kwa kubahatisha bali kwa mipango kabambe, na hata kwenye michezo ya kufuzu waliwachapa wakongwe wengi,kwa kuthibitisha kwamba wana nia ya kuwa miongoni mwa mataifa makubwa kisoka kadiri siku zinavyokwenda, wameustaajabisha ulimwengu kwa kutoka sare ya bao 1-1 na mabingwa wa dunia mara mbili Argentina nchi yenye idadi ya watu zaidi ya million arobaini na nne na laki sita lakini pia timu ilyosheheni nyota wengi wa kimataifa na mchezaji bora wa dunia mara 5 Lionel Messi,hii ni changamoto kwetu.

Kwa kiwango tulicho nacho sasa bado kipo chini,kwa vyovyote vile hatuna uwezo wa kucheza Kombe la Dunia lakini tuwaze kucheza Afcon, bahati nzuri mwakani tutakuwa wenyeji wa michuano ya vijana chini ya miaka 17.

Itakuwa vizuri iwapo tutaanzia hapo kujenga misingi ya weledi na kupata uzoefu mkubwa wa kuandaa michuano mikubwa pia kuziandaa timu zetu kwa ajili ya michezo mikubwa ya kimataifa.

Tukiwekeza kwa nguvu na tukawa na nia ya kuona kile tulichowekeza kinafanyika, ni wazi kila jambo linawezekana.

Advertisement