TASWIRA YA MLANGABOY : Tunataka wachezaji wenye viwango bora CHAN 2020

Muktasari:

Hilo ndiyo jambo la msingi zaidi kwa sababu unapokuwa umekaa nje ya mashindano kwa zaidi ya miaka 10 tangu iliposhiriki kwa mara ya kwanza mashindano ya CHAN yaliyofanyika Ivory Coast mwaka 2009, ambapo DR Congo ilitwaa ubingwa, ni wazi tunahitaji utayari wanajeshi zaidi kwa ajili ya kupambana.

KOCHA Mkuu wa Timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, Ettiene Ndayiragije amesema wachezaji waliosaidia timu hiyo kufuzu kwa fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wanaocheza Ligi za Ndani (CHAN2020) kazi yao ilikwisha.

Tanzania itashiriki Mashindano CHAN2020 yanayotarajia kuanza Aprili 4-25 mwaka huu Cameroon ikiwa Kundi D pamoja na Namibia, Zambia na Guinea.

Ndayiragije alisema kikosi chake kitakuwa na mabadiliko makubwa ya wachezaji kwa kuwa waliosaidia timu kufuzu, kazi yao iliisha. Ndayiragije alisema anaamini Stars itafanya vizuri na muda upo wa kujiandaa na kufafanua hata wiki moja au mbili zinatosha.

Ameeleza kikubwa ni wachezaji wenyewe kuwa tayari na kwamba mkakati wanaoufanya timu hiyo itafanya vizuri na kubainisha kuwa wapinzani watakuwa na ushindani, lakini hawaogopi kitu.

Naungana na Ndayiragije anaposema wachezaji waliowezesha timu hiyo kufuzu kazi yao imekwisha, na kubwa zaidi ni kuwataka wachezaji wenyewe kuwa tayari kwa fainali hizo.

Hilo ndiyo jambo la msingi zaidi kwa sababu unapokuwa umekaa nje ya mashindano kwa zaidi ya miaka 10 tangu iliposhiriki kwa mara ya kwanza mashindano ya CHAN yaliyofanyika Ivory Coast mwaka 2009, ambapo DR Congo ilitwaa ubingwa, ni wazi tunahitaji utayari wanajeshi zaidi kwa ajili ya kupambana.

Ukisoma kwa makini kauli ya Ndayiragije kuhusu wachezaji walioivusha Stars kazi yao ilikwisha ni wazi anatoa ishara ya kujiandaa kisaikolojia kwa wachezaji wake.

Kwa sababu kuna wachezaji waliofanikisha timu hiyo kufuzu wanaweza kuwa na mawazo kwamba wao ni lazima wataenda Cameroon bila ya kutunza viwango vyao.

Ukweli Mrundi huyo anawaambia wale waliopoteza ubora wao kwa sasa hawatakuwa na nafasi kwa sababu katika mashindano unahitaji wachezaji waliokuwa katika viwango bora zaidi kwa sasa kuliko historia yao. Naamini ni wachezaji wengi walikuwa tegemeo wakati ule mechi za kufuzu leo wamepoteza ubora wao kwa sababu moja au nyingine, jambo la msingi ni kocha kuchagua wachezaji bora si majina bora ya kufurahisha watu.

Unaweza kuziona Namibia, Guinea na Zambia ni timu nyepesi kwa majina yao, lakini ligi zao ni nzuri na zimefanikiwa kutengeza mabingwa na wachezaji wenye ushindani. Tofauti kubwa ya wachezaji wetu na wenzetu ni kwamba wao wanapata wachezaji waotokana na ushindani wa ndani ya uwanja si wa hapa kwetu ambako kila siku tunapeana lawama za kuhongo waamuzi na timu pinzani.

Naamini Kocha Ndayiragije atatumia muda wa sasa kutangaza kikosi cha awali ili kuwapa muda wachezaji wetu kutambua jukumu lao na kujiandaa katika kuelekea kupata kikosi cha mwisho.

Morocco, Rwanda tayari zimeweka bayana vikosi vyao ya awali mapema ili kuonyesha umuhimu wa mashindano haya kwao, hivyo ni bora na sisi tukafanya hivyo kwa sababu tunajua ukweli kuhusu viwango vya wachezaji wetu ni kama homa za vipindi.

Pia, sina tatizo la kutumia muda wa wiki mbili kuandaa timu kwa ajili ya mashindano haya kwa kuzingatia ugumu wa ratiba ulivyokuwa kwa sasa.

Kwa sababu mwishoni mwa mwezi ujao kutakuwa na mechi mbili za kusaka kufuzu kwa Afcon2021 dhidi ya Tunisia, pia Ligi Kuu Tanzania Bara inakimbizana kabla ya kusimama ili kupisha mashindano ya CHAN2020.

Hata hivyo, bado nadhani TFF na wadhamini pamoja na Kocha Ndayiragije watakuwa wamefanya kosa la kiufundi kwa kushindwa kuipatia Taifa Stars ya Chan kwenda katika mashindano haya bila ya kupata muda wa kucheza mechi japo mbili za kirafiki.

Najua sehemu kubwa ya wachezaji watakaocheza dhidi ya Tunisia ndio watakwenda Cameoon, lakini bado timu ya Chan ilipaswa kucheza mechi na kujua ubora wake ikiwa bila ya nahodha Mbwana Samatta, Saimon Msuva mbele.

Majirani zetu Rwanda watacheza mechi mbili za kirafiki mwisho wa mwezi Februari 24 watakuwa ugenini kuivaa Cameroon na Februari 28 watacheza nyumbani dhidi ya Congo-Brazzaville yote ikiwa ni sehemu ya maandalizi yao kwa CHAN.

Hakuna ubishi timu inapojianda na mashindano ni vizuri kupata mechi za kirafiki ikiwa ni sehemu ya maandalizi hii itasaidia kuijenga kiushindani na kujua kombinesheni za wachezaji.

Mwisho natamani TFF iweke wazi mapema wachezaji wakifanikiwa kufuzu kwa hatua ya pili watapewa Dola 175,000 zile ambazo timu zinapewa kwa kushiriki tu mashindano haya.

Hiyo iwe kwa hatua ya awali, lakini huko mbele watakavyokuwa wakifanya watapewa kulingana na mafanikio yao kwa sababu timu ikiingia nusu fainali itajihakikishia kupata Dola 400,000 hivyo ni vema mambo haya yakawekwa sawa mapema.

Tunahitaji kuona Tanzania ikifanya vizuri zaidi katika mashindano ya mwaka huu kwa kuwa na maandalizi ya aina zote ndani na nje ya uwanja.