Tulimmisi Special One wa Turf Moor

Thursday September 6 2018Said Pendeza

Said Pendeza 

By SAID PENDEZA

HUYU sasa ndiye Jose Mourinho, The Special One tunayemfahamu. Jose Mourinho tuliyemmisi siku za karibuni.

Kiboko wa kutumia mbinu kupata matokeo. Kimsingi Mourinho hajawahi kucheza mpira wa kuukosha moyo wa yeyote yule, ila amekuwa akiwapa furaha mashabiki wake kwa kuwapata matokeo.

Huko Turf Moor, Mourinho aliwakumbushia mashabiki kwanini alijipachika jina la The Special One miaka kadhaa iliyopita. Dhidi ya Burnley ilikuwa mechi ya matokeo ya aina moja tu, ushindi kwa Man United ili kibarua cha Mreno kuwa salama.

Kama inavyofahamika, Turf Moor hapajawahi kuwa mahali pazuri kwa Man United kwa miaka ya karibuni.

Lakini, Mourinho ndipo hapo alipokwenda na mbinu zake na kupata matokeo. Alichokifanya Mourinho, si kwama hakuwa na mabeki wa kati watatu kwenye kikosi chake, la alikuwa nao, lakini alichokitaka ni kuwa na viungo wawili wa kukaba ndani ya uwanja, lakini akiwa na wachezaji wa ziada kwenye safu ya ushambuliaji. Hapo ndipo alipomwaanzisha Marouane Fellaini kwenye nafasi ya mabeki wa kati. Big Fela alisimama katikati ya mabeki wawili wa kati, Chris Smalling na Victor Lindelof. Akawa anakaba mipira yote inayompita Nemanja Matic na Paul Pogba kwenye kiungo.

Big Fela akawafanya Luke Shaw na Antonio Valencia kuwa na uhuru wa kwenda mbele kushambulia, huku Pogba akicheza kwa uhuru. Jambo hilo lilimfanya pia kuwa na washambuliaji watatu mbele, Alexis Sanchez, Romelu Lukaku na Jesse Lingard.

Big Fela alicheza chini sana kuwakinga mabeki wa kati Smalling na Lindelof. Lakini, Mourinho alitumia pia mbinu moja ya kucheza fomesheni inayoitwa boksi, ambapo wachezaji wanatengeneza pembe nne kwenye sehemu ya ulinzi, na hiyo ilifanywa na Big Fela, Matic, Shaw na Valencia, ambayo ilikuwa na majukumu ya kuzuia mipira yote ya juu na chini ya wachezaji wa Burnley.

Zilikuwa mbinu ambazo zilimfanya Matic kucheza kwa uhuru. Zilikuwa mbinu zilizomfanya Big Fela kucheza kwa uhuru. Hakuna ubishi ni mtindo wa kiuchezaji ambao Mourinho anaweza kuutumia tena kwenye mechi zijazo. Timu yake ilitengeneza nafasi nyingi na haikuwa ile Man United, ambayo imekuwa ikidaiwa kwamba wachezaji wake ni kama wanacheza wakiwa wamefungiwa kwenye boksi, hawatembei. Pogba alipewa eneo kubwa tu kuuchezea mpira na kumfanya awe afurahie mchezo wake.

Bila shaka kama Mourinho ataendelea na mbinu hizo na kuwapa wakali wake Sanchez na Pogba uhuru ndani ya uwanja, hakuna mashaka Man United itaanza kuvuna matokeo ambayo inayataka.

Advertisement