NINAVYOJUA : Tanzania tunaponzwa na wachezaji wenye vimo vifupi

Muktasari:

  • Maumbile hayo ya wachezaji wetu yalionekana madogo mbele ya wachezaji wa nchi kama Niger, Mali na Angola ambazo zilikuwa kundi moja na kufikia kuonekana kama wadogo zao.

INAWEZEKANA mwaka jana wakati kikosi cha Vijana cha Taifa cha U-17, Serengeti Boys kilichocheza fainali za vijana kule Gabon ndicho kilichokuwa na wachezaji wenye vimo vifupi kuliko nchi nyingine kwenye michuano hiyo.

Maumbile hayo ya wachezaji wetu yalionekana madogo mbele ya wachezaji wa nchi kama Niger, Mali na Angola ambazo zilikuwa kundi moja na kufikia kuonekana kama wadogo zao.

Kuelekea vita vya mchezaji mmoja mmoja ndani ya uwanja hali haikuwa sawa maana kwa wale wa timu pinzani walikuwa wakishinda vita hivyo. Hili siku zote linaendelea kututesa Watanzania na kupunguza nafasi za kushinda.

Haya kile kikosi cha Gabon ambacho tuliwaona wachezaji wetu wakiwa na vimo vifupi ukiwaacha baadhi ya wachezaji ambao walikuwa na vimo sahihi kama kina Ramadhani Kabwili, Israel Patrick Mwenda, Yohana Mkomola, Ali Ng`anzi lakini bado nao walionekana wafupi na kupigana chini ya magoti ya wachezaji wa nchi za Afrika Magharibi.

Hali hiyo iliwalazimu kutafuta aina nyingine ya uchezaji, hata hivyo kazi ilikuwa kubwa mno.

Achana na kikosi hicho. Sasa tunayo timu nyingine itakayoshiriki michuano hiyo itakayofanyika mwakani hapa nyumbani.

Ndani ya kikosi hicho huwapo tena kina Mwenda na Mkomola. Kwa sasa ukiwaona wachezaji wetu utaona jinsi gani vimo vyao vilivyo. Ukiachana na makipa wawili wenye vimo vizuri, wengine kwa asilimia 95 wana vimo vya chini ya mita 5. Binafsdi nadhani hii inatuathari sana kwenye ushindani wa soka la kisasa na hata huko tulikotoka.

Nimekuwa nikijiuliza tumekumbwa na tatizo gani Watanzania au ni uvivu na kuamua kuwachagua wachezaji wanaoonekana machachari?

Kwanza lazima tukubali wachezaji wenye vimo virefu ni wengi na wana faida nyingi kuliko wachezaji wenye vimo vidogo licha ya kile kinachoitwa ‘exceptional’ yaani ya kitofauti au ya kipekee. Lakini kwa hapa Tanzania kunaweza kuwa na sababu zifuatazo;

Moja - Kukosa watu sahihi waliosomea namna ya kutambua kipaji cha mchezaji mwenye maisha marefu au mafupi ndani ya soka, hatuna watambuzi ( scouting team) ambayo kazi zake ni hizo tu.

Pili, uvivu wa kubaini vipaji vinavyoweza kuendelezwa kirahisi kuliko vile vinavyoonekana kujiendeleza vyenyewe. Kwa jumla wachezaji wengi wenye vimo vifupi huwa na uwezo binafsi na hujiendeleza lakini ni wachezaji wanaofikia mwisho wa ujenzi wa miili na misuli yao haraka huku wale wenye maumbo marefu wakitumia muda mrefu kujengwa misuli yao na huishi muda mrefu baada ya ujenzi huo .

Tatu ni kukubali kuchukua wachezaji wanaonekana kama wameshajua zaidi kuliko wenzao. Hii hutokea kwa wenye vimo vifupi na maumbile madogo kuonekana kuwa sawa na wenye vimo virefu. Kwa mazingira ya Kitanzania mchezaji mfupi mwenye umri wa miaka 17 anaweza kuonekana mdogo hata kwa kijana mrefu mwenye umri wa miaka 14. Hapa ndipo tunapochagua kwa kuangalia nyuso za vijana badala ya uhalisia wa mchezaji.

Nne ni uvivu wa kumuendeleza mchezaji kwa muda mrefu. Hii kwetu hasa makocha huamua kuchukua mchezaji anayeonekana kuiva moja kwa moja kwa maana kuonekana anajua zaidi na hivyo badala ya kumchukua na kumkuza huo muda huwa hatuna. Hapo ndipo mchezaji huchukuliwa ili mradi tu.

Mwisho ni kushindwa kuchagua mchezaji kutokana na sifa za wanapotakiwa kucheza. Si vibaya wachezaji wafupi kucheza mabeki wa pembeni na mawinga. Lakini ni kosa kumchagua beki wa kati mfupi na kumuacha mrefu.

Kwa miaka mingi uchaguzi huu ungeushuhudiwa kwenye timu za Mtibwa na Prisons zilitawaliwa na sifa hizo. Makocha wengine huwachagua wachezaji wafupi kwenye nafasi ya ushambuliaji wa kati.

Kwa Serengeti Boys suala la vimo si ajenda tena kwa kuwa timu imeshachaguliwa na kilichobaki ni kusubiri fainali hizo za hapa nchini.

Kwa hilo, hatuna budi kuifanya timu yetu icheze kwa ushindani dhidi ya wachezaji watakaokuja wakiwa na maumbileo makubwa.

Tukubali kama ilivyokuwa kizazi cha kina Xavi Hernandez, Andres Iniesta, Lionel Messi na wengineo walioiunda Barcelona yenye wachezaji wafupi lakini machachari kwa aina yao ya soka la chini chini na pasi za haraka huku wakiwa hawategemei mipira ya kona wala krosi.