TIMUA VUMBI : Yanga mjipange, msimu huu hamna chenu

Thursday May 9 2019

 

By Mwanahiba Richard

YANGA imebakiza mechi nne sasa imalize Ligi Kuu Bara. Imekusanya pointi 81 na ndiyo timu pekee ambayo imedumu kileleni kwa muda mrefu tangu msimu huu uanze.

Huenda kudumu kwa Yanga kileleni kwa muda mrefu kulitokana na watani zao Simba kutocheza mara kwa mara mechi za ligi huku Azam ikishindwa kutoa upinzani mkali kwa Yanga.

Azam sasa inashika nafasi ya tatu kwenye msimamo baada ya kushushwa na Simba ambao jana Jumatatu walicheza dhidi ya Coastal Union kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Achana na ushindani uliopo sasa kwenye mechi za lala salama za ligi hiyo, Simba ndiyo yenye nafasi kubwa ya kutetea ubingwa wao kutokana na kubakiwa na mechi saba huku Azam nao wakitinga fainali ya Kombe la FA na watacheza dhidi ya Lipuli.

Azam angalau wanaweza kujipa matumaini kwamba watapambana kuhakikisha wanatwaa ubingwa wa FA kwa kuwafungwa Lipuli, tofauti na Yanga ambao hata wakishinda mechi zote nne bado nafasi ya kutwaa ubingwa ni finyu.

Hata Yanga wakishinda zote nne na simba ikapoteza tatu kati ya saba zikizobaki bado watakuwa mabingwa kutokana na wingi wa mabao ya kufunga.

Advertisement

Haya, wiki iliyopita Yanga walipata uongozi mpya chini ya Mwenyekiti Dk Mshindo Msolla na msaidizi wake Fredrick Mwakalebela. Hawa ni watu wa mpira. Hata kama mmoja ni mwanasiasa lakini maisha yake mengi yapo kwenye utendaji na soka sio propaganda za kisiasa.

Nadhani Dk Msolla ambaye pia kitaalamu ni kocha ataisaidia Yanga kuanzia msimu ujao kwani msimu huu anapaswa kuuacha upite tu, akili yako inapaswa sasa kufikiri msimu ujao utaifanyia nini Yanga.

Upo kwenye mpira kwa miaka mingi pengine kumdhidi hata msaidizi wako, hivyo ni wazi wewe ni mhimili mzuri ndani ya Yanga na siyo uwepo wako uwe wa kurudisha nyuma klabu hiyo ambayo miaka miwili sasa haijawa na mwenendo mzuri.

Ili ufanikiwe ni lazima uwe na safu nzuri huku chini ikiwa ni kuunda kamati zenye uwezo kiutendaji na sio kuangalia urafiki ambao hawana uwezo na kuwajaza kwenye kamati nyeti.

Mafanikio ya Yanga yatatokana na uongozi bora na imara kutoka kwa Dk Msolla vivyo hivyo kufeli kwa Yanga kutasababishwa na uongozi wa hovyo kama mwenyekiti atashindwa kutengeneza safu bora na imara.

Wanayanga wanatarajia mambo mengi ambayo yaliahidiwa wakati wa kampeni ikiwemo mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji, timu bora na imara itakayokuwa na ushindani na yenye kikosi kipana kitakachompa uhuru kocha Mwinyi Zahera katika maamuzi.

Ingawa kuna majukumu mengi mbele yako lakini ni vyema ukaanza kukisuka kikosi kwani furaha kubwa ya wanachama na mashabiki wa Yanga ni kuona timu inafanya vizuri na kutwaa ubingwa.

Sahau matokeo ya sasa, haya hayawahusu bali mnapaswa kujipanga na safu yenu kupambana na kuhakikisha msimu uhao Wanayanga wanapata moja ya makombe mawili yanayogombaniwa ukiachana na yale ya mashindano mengine.

Niwatakie utendaji kazi mzuri uwe na malengo yaliyowapeleka madarakani pasipo kuwepo mvurugano wowote, makombe ya msimu huu myasahau mpiganie yajayo kwa kukisuka upya kikosi chenu.

Advertisement