TIMUA VUMBI : TPL unasakwa ubingwa, zawadi inapatikana CAF

Muktasari:

  • Baadhi ya timu ambazo hazijamaliza mechi za mzunguko wa kwanza ni zile ambazo hazijakutana na Simba iliyocheza mechi 17 kutokana na kukabiliwa na mechi za kimataifa kwani inashiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi.

LIGI Kuu Tanzania Bara inaelekea ukingoni huku baadhi ya timu hazijamaliza mechi za mzunguko wa kwanza.

Baadhi ya timu ambazo hazijamaliza mechi za mzunguko wa kwanza ni zile ambazo hazijakutana na Simba iliyocheza mechi 17 kutokana na kukabiliwa na mechi za kimataifa kwani inashiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi.

Timu zingine zinaendelea na mechi za mzunguko wa pili ambao ni wa lala salama huku baadhi zikiwa zimecheza mechi 24 hadi sasa kati ya mechi 30 za msimu mzima wa ligi hiyo.

Tangu mkataba wa udhamini wa Ligi Kuu na Kampuni ya Mawasiliano ya Vodacom ulipomalizika, Shirikisho la Soka nchini (TFF) hawajapata mdhamini mwingine zaidi ya udhamini wa Azam Tv ambao pia sio mdhamini mkuu wa ligi.

Katika udhamini huo, timu ambayo inatwaa ubingwa wa ligi huwa anapewa Sh 84 milioni ambayo kiuhalisia ni pesa ndogo ila timu hunufaika kupata nafasi ya kushiriki michuano ya kimataifa ambapo wakifanya vizuri kuna pesa nzuri wanapata kutoka CAF.

Pesa inayopatikana CAF hasa timu ikifika hatua ya makundi ambayo ni zaidi ya Sh 1 bilioni ndizo zinazopigawani huku chini kwenye ligi vinginevyo timu hushiriki ligi kwa hasara kubwa.

Hasara inayopata timu ni kutumia gharama kubwa kwenye maandalizi ya ligi, usajili, mishahara, kambi, usafiri na mambo mengine ambayo hata kama udhamini ungekuwepo napo kwa baadhi ya timu kama Simba, Azam, Yanga isingetosha kabisa kwani wao hulenga zaidi kimataifa kuliko zawadi ya pesa ya ubingwa ambayo ni ndogo sana kuliko mahitaji yao.

Msimu huu umekuwa mgumu kwa klabu kwani hakuna kitu chochote cha kuwapooza koo, timu zinashiriki katika mazingira magumu ambapo wenye uwezo kidogo ndiyo wanaonufaika hata wakienda kucheza mechi za mbali angalau wanakuwa na uwezo wa kupunguza safari kwa kutumia usafiri wa anga.

Wale wenye uwezo wao mdogo, wanakuwa kwenye wakati mgumu kufika sehemu nyingine kutokana na umbali kwani waliowengi hutumia usafiri wa barabara, hata uwekezaji wao ni mdogo na pigo kubwa hata kifuta jasho cha kupunguza makali kutoka kwa mdhamini mkuu hakuna.

Lakini yote hayo ni moja ya changamoto katika maisha na taasisi ambapo kuna kupata na kukosa, ingawa ukata huo unaweza kuchangia kwa baadhi ya timu kugawa pointi hasa mechi hizi za lala salama kwa timu zenye uwezo mkubwa.

Hivyo kwenye ligi sasa timu zinapigania kutwaa ubingwa wa usio na zawadi zaidi ya kombe lakini wanahitaji kupata pesa kutoka CAF ambazo zitawasaidia kuendesha maisha ya wachezaji na shughuli zingine za klabu zao.

TFF ilitangaza kupata neema kutoka kwa kampuni moja ambayo haikutajwa wazi kuwa ndiyo itakayodhamini Ligi Kuu msimu ujao, hivyo maumivu ya msimu huu kwa klabu yatamalizwa kama si kupunguzwa msimu ujao.