TIMUA VUMBI : Stars safi, sasa ni Serengeti Boys, Twiga Stars

Thursday March 28 2019

 

By Mwanahiba Richard

TUNAPOZUNGUMZIA ishu za kitaifa kwenye michezo tunamaanisha timu zote za Tanzania, iwe klabu ama timu za taifa, zinapocheza kuwakilisha nchi kimataifa.

Taifa Stars tayari imefuzu fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) zitakazochezwa nchini Misri kuanzia Juni 21 hadi Julai 21 mwaka huu kufuatia ushindi wa 3-0 dhidi ya Uganda ambayo ilikuwa imeshafuzu.

Timu ya taifa ya vijana ya U-17, Serengeti Boys itakuwa mwenyeji wa AFCON ya vijana kuanzia Aprili 14 jijini Dar es Salaam; timu ya taifa ya wanawake Twiga Stars itawakaribisha Congo Aprili 5 katika kuwania tiketi cha kufuzu kwa michezo ya Olimpiki;

Na klabu ya Simba ambayo imetinga hatua ya robo-fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, itawakaribisha TP Mazembe katika mechi yao ya awali ya robo-fainali Aprili 6.

Huo ni mfululizo wa matukio ya kitaifa yanayoikabili nchi kwa sasa na kila Mtanzania anapaswa kujivunia na kutoa sapoti yake katika kusaka mafanikio.

Baada ya miaka mingi ya kufeli, Tanzania sasa imepata matumaini mapya katika michezo na ni jambo la kujivunia.

Licha ya kufuzu, Stars iliwaweka Watanzania katika presha kubwa kutokana na mazingira ya mechi yao ya mwisho dhidi ya Uganda.

Stars ilikuwa ni lazima ishinde. Lakini ushindi peke yake ulikuwa hautoshi kufuzu. Ilikuwa ni lazima Watanzania ‘waicheze’ pia mechi nyingine ya kundi hilo iliyokuwa ikichezwa nchini Cape Verde dhidi ya Lesotho. Wakati Stars ikiongoza kwa kujiamini kwa 3-0 kwenye Uwanja wa Taifa, mashabiki walikuwa roho juu kufuatilia mechi hiyo ya Cape Verde maana goli moja tu kutoka kwa Lesotho lingemwagia mchanga pilau la sherehe Tanzania.

Lakini Mungu si Athuman. Sare ya Cape Verde ilitosha kuwapeleka Stars kwenye fainali za Afrika kwa mara ya kwanza katika miaka 39 na ya pili kwa ujumla tangu fainali hizo zianzishwe.

Kundi hilo lilihitimishwa kwa Uganda kumaliza vinara wakiwa na pointi 13 na Tanzania ikifuatia na pointi nane.

Hilo limepita. Baada ya Shirikisho la Soka nchini (TFF), serikali na Watanzania wote kuungana kwa pamoja kuhakikisha Stars inafuzu, sasa muda mwafaka wa kugeuzia nguvu katika maandalizi kwa ajili ya fainali hizo.

Nguvu ziwekwe katika kuhakikisha Serengeti Boys, Twiga Stars na Simba zote zinafanikiwa katika mechi zinazowakabili.

Yote yanawezekana kama nia na malengo yatawekwa huku kila mmoja akijitoa kwa nafasi yake kuhakikisha timu hizo zinaweka historia kwenye medani ya soka nchini.

Nina uhakika kwamba TFF, Serikali na wadau wa soka nchini watajitoa kwa kila hali ikiwamo kuwapa morali ya ushangiliaji siku ambazo watacheza mechi zao kama ilivyokuwa mchezo uliopita.

Timu zote zinaiwakilisha nchi, hivyo kufanya vizuri kwao kutaleta heshima kwa taifa zima.

Mechi zote hizi zilizo mbele yetu zikichukuliwa kitaifa, tutafika tu kwenye kilele cha mafanikio. Mungu ibariki Tanzania.

Advertisement