TIMUA VUMBI : Senzo usikae na maumivu moyoni, funguka

Friday October 11 2019

 

By Mwanahiba Richard

WACHEZAJI wanne wa Simba hawakuwa miongoni mwa kikosi kilichosafiri kwenda Kanda ya Ziwa kucheza mechi mbili za Ligi Kuu ya Vodacom.

Wachezaji hao ni Jonas Mkude, Clatous Chama raia wa Zambia, Erasto Nyoni na Gadiel Michael. Nyota hawa wamezua sintofahamu kwa mashabiki wao kutokana na mwenendo wao wa sasa kwani kabla ya kuitwa timu ya taifa ni kama walisimamishwa kuendelea na mazoezi na wenzao ndani ya Simba wakisubiri hatima yao.

Simba ilianza kucheza mjini Bukoba na Kagera Sugar ambapo ilishinda ba0 3-0 ikasafiri hadi Musoma kucheza na Biashara United ambako iliibuka na ushindi wa mabao 2-0 hivyo kurudi Dar es Salaam ikiwa na pointi sita bila nyota hao ambao mara nyingi huanza kikosi cha kwanza cha Patrick Aussems.

Nyota hao hata timu iliporejea jijini Dar es Salaam hawakujiunga na wenzao kwenye mazoezi yao ingawa kwasasa wapo timu ya taifa inayojiandaa kucheza mechi ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya Rwanda itakayochezwa mjini Kigali, Septemba 14 mwaka huu.

Wachezaji hao baadhi yao wanadaiwa kuwa na utovu wa nidhamu kwani wakati timu ilipotakiwa kusafiri walidaiwa kwamba walichelewa kuamka na kukuta wenzao wameondoka ingawa taarifa zingine upande wa Nyoni na Gadiel wao wanadaiwa kuwa walikuwa na matatizo.

Mwanzo kabisa ilielezwa kwamba Nyoni alikuwa akiuguliwa na mwanaye jambo ambalo lilimfanya ashindwe kuhudhuria mazoezi ya timu ikijiandaa na safari ya Kanda ya Ziwa huku Gadiel ni kwamba anasumbuliwa na majeraha.

Advertisement

Yote hayo yanawezekana kwa wachezaji hao wawili ingawa pia inadaiwa kwamba Patrick Aussems kocha mkuu wa Simba aliwataka wachezaji hao waripoti kambini mapema kutokana timu ya taifa ambako walikuwa na majukumu ya kitaifa ila hawakufanya hivyo na walipokwenda walipeleka sababu za matatizo yao.

Wawili wengine Mkude na Chama tatizo lao bado ni kizungumkuti kwani kila mmoja huzungumza lake ingawa baadhi ya viongozi wa Simba husema kwamba ni utovu wa nidhamu kwa kushindwa kujiunga na wenzao huku wakijua ratiba ya safari hiyo ikoje.

Yote kwa yote, tufanye wachezaji hao wamefanya makosa lakini hii tabia kwa wachezaji wetu itakwisha lini maana wengine wamekuwa sugu na tabia kama hizo, na wengi wao ni wale hawawazi kama kuna kucheza soka la kimataifa ama kuna maisha mengine nje ya mpira.

Mpira una muda wake endapo mchezaji atashindwa kujitunza, kiwango kitashuka na ataachwa na timu yake, je atakuwa amejiaandaaje kimaisha ama kuishi maisha mengine nje ya mpira wake aliouzoea siku zote.

Nadhani kuna haja kwa kila mchzaji, si Mkude, Chama na wengineo kubadilisha mfumo wa maisha yao na kuangalia pale panapofaa zaidi kwa ajili ya familia na jamii inayowazunguka kwenye hayo maisha.

Wengi huiga ama tabia zao hubadilika kutokana na makundi wanayokutana nayo ingawa wengine hizo ndiyo tabia zao hata uwabadilishe vipi ama kupigiana nao kelele hawawezi kubadilika zaidi tu ya kukaa vikao nao visivyokuwa na mwisho.

Inakuwa inaleta taswira mbaya na mbovu kwa klabu zao pale inapotajwa wachezaji fulani ama mchezaji yule wa timu fulani tabia yake kubwa ni utovu wa nidhamu, sio jambo jema.

Kwa umri wa wachezaji wengi wa Kitanzania bado ni wadogo, hivyo wautumie vyema umri wao kutengeneza maisha yao kupitia mpira kwani walio wengi pia hata wakishindwa kucheza soka hawana pa kukimbilia kutokana na mifumo ya maisha yao ilivyo. Ni wachache tu wanaoweza kunufaika hata nje ya mpira na ni wale tu waliowekeza ama kujiendeleza na jambo fulani baada ya maisha ya mpira kumalizika, hakuna mchezaji asiyefahamu maisha ya mchezaji mwenzake ambaye alishindwa kujitunza, kujilinda na kuwekeza pale alipofanikiwa kushika pesa nzuri wakati anacheza.

Kama kweli wachezaji hao ambao ni vipenzi vya mashabiki wa soka nchini wamefanya makosa basi wana kila sababu ya kutubu, wanawakosea mashabiki wao, wanapaswa kuwa mfano mzuri kwa vijana wanaochipukia.

Nyota hao wana kila sababu ya kuacha alama nzuri kwenye soka kutokana na viwango vyao, umri wao na klabu wanayoichezea. Wajaribu sasa kuwa na malengo ya kuona mbali kwamba

Simba sio mwisho wao iwe njia ya kutokea kucheza soka la kulipwa.

Kama watashindwa kubadilika basi mwisho wao utakuwa ni kucheza hapa hapa mpaka kustaafu kwao, hii isiwe kwa wachezaji hao tu bali wachezaji wote wenye tabia kama hizo

wajiangalia walikotoka, walipo na wanakokwenda ikiwa ni pamoja na kuhusishanishwa na matendo yao. Ujana upo lakini unapaswa kuwa na kikomo kulingana na nyakati.

Hakuna aliyeweka wazi juu ya matatizo ya wachezaji hao ambapo hata wenyewe wamekuwa waoga kuzungumzia kilichosababisha kukaa pembeni kwa siku hizo ingawa taarifa zinasema kwamba Mkurugenzi Mtendaji, Senzo Mazingisa ndiye aliyeshika hatima ya nyota hao.

Hivyo basi mbivu na mbichi zitajulikana pale ambapo Senzo ataamua kuweka mambo hadharani juu ya wachezaji hao maana hata Aussems hana madaraka juu ya hili katika kulizungumzia.

Advertisement