TIMUA VUMBI : Namungo mnapaswa kujiandaa kisaikolojia

Thursday November 29 2018

 

By Mwanahiba Richard

LIGI Daraja la Kwanza (FDL) inaendelea kutimua vumbi viwanja mbalimbali huku kuna baadhi ya timu zikiaminika kuwa zina nafasi ya kupanda kutokana na uwezo wa pesa ambazo wanazo.

Miongoni mwa timu ambazo zinatazamiwa kumaliza nafasi ya juu na kupanda Ligi Kuu Bara ni Dodoma FC iliyokuwa chini ya Kocha Jamuhuri Kihwelo ‘Julio’ ambaye msimu uliopita ilikosa nafasi dakika za mwisho.

Timu nyingine ambayo inatazamwa kuwa na nguvu ya kupanda ni Arusha United ambayo ipo chini ya Kocha Fred Felix ‘Minziro’ akipata nguvu ya kutosha kutoka kwa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo.

Timu hizo zote hazipo nafasi mbaya kama zitakaza misuli zitapanda lakini kubwa zinachotakiwa kufanya ni kuonesha soka imara uwanjani kama inavyofanya Pamba kwani licha ya kutokutajwa mwanzoni mwa msimu inaongoza kwenye kundi lake.

Mashabiki wa Namungo ya Lindi Wilaya ya Luhangwa wanatembea kifua mbele wakiamini timu yao inaweza kuwa ya kwanza kupanda msimu huu kutokana na nguvu ya pesa iliyonayo.

Namungo kabla ya kuanza ligi ilicheza mechi nyingi kubwa za kirafiki ikiwemo dhidi ya mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara Simba ambayo ilikuwa imesheheni nyota wake wote lakini matokeo yaliisha kwa sare.

Katika kuhakikisha mambo yanakwenda sawa ndani ya timu ilipatiwa usafiri wa uhakika ili kwenda kucheza mechi kokote inakohitajika, lakini kama haitoshi ni miongoni mwa timu yenye kiwanja kizuri cha nyumbani.

Uwanja wa Namungo unatambulika kama Majaliwa Stadium na katika kuhakikisha timu hiyo inafanya vizuri viongozi waliamua kumuajili kocha mzoefu, Fulgence Novatus ili kuhakikisha timu hiyo msimu ujao inacheza Ligi Kuu.

Wachezaji na watumishi wote wa Namungo wanapata posho, mishahara na mahitaji mengine yote kwa wakati kwa mujibu wa uongozi wa timu hiyo ni wazi yote hayo yanatimia kwa kupata nguvu ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

Habari njema zaidi katika klabu hiyo ya Namungo ambayo ipo katika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 13 sawa na Mlale FC inawawinda nyota ambao wametamba katika Ligi Kuu na klabu mbalimbali.

Mashabiki wa Namungo wanaendelea kutoa maneno ya kijeli ya kuzitambia timu nyingine kuwa katika dirisha dogo wanaweza hata kumsajili, Emmanuel Okwi, Heritier Makambo na wengine wengi ili kuimarisha kikosi chao.

Hata hivyo taarifa zilizopo ni kuwa nyota wa Azam FC, Mbaraka Yusuph na Oscar Masai, Mohammed Rashid na Marcel Kaheza wote kuna taarifa wapo njiani kujiunga na Namungo.

Kwa kwa upande wa Yanga, wachezaji Patho Ngonyani, Said Makapu na Yohana Mkomola nao wanaweza kujiunga na chama hilo.

Ni wazi shabiki yeyote akiona timu yao inapata kila kitu kwa wakati hasa katika kipindi hiki ligi haina mdhamini, usajili wa wachezaji wa maana ambao muda tu unasubiriwa ili kutambulishwa kujiunga na Namungo lazima wajiamini na kutoa maneno haya ya kujigamba.

Timua vumbi wiki hii inawakumbusha na kuwataka mashabiki wa Namungo wajiandae kisaikolojia kwani mbali mbali ya timu yao kupata au kuwa na kila kitu inaweza isipande kulingana na matokeo ya uwanjani.

Mashabiki wa Namungo wanatakiwa kujiandaa kisaikolojia na si kwenda uwanjani wakiwa na matokeo yao binafsi wakiamini timu yao inahaki ya kupanda kuliko nyingine kutokana na nguvu ambayo wanayo.

Namungo wanatakiwa kujiandaa vyema uwanjani ili kupata matokeo ya ushindi na si kufikiria maandalizi mengi ya nje ya uwanja kama ambavyo imezoeleka mechi za FDL zinapochezwa.

Dodoma FC msimu uliopita ilikuwa ikipata kila kitu na kuaminika ingeweza kupanda Ligi Kuu msimu huu lakini katika mechi za mwisho ilishindwa kujiandaa vizuri kwa kupata matokeo ya ushindi na kujikuta ikipoteza nafasi hiyo.

Viongozi, wachezaji na benchi la ufundi wanatakiwa kuweka nguvu kubwa katika uwanja yaani ndani ya kila dakika 90 za mechi 22 ambazo timu yao itacheza msimu huu ili kupata ushindi wa uhalali na kupata pointi za kutosha ambazo zitawasaidia kufikia malengo yao.

Timu kama PSG ya Ufaransa ina nguvu ya kipesa, wachezaji wenye viwango bora duniani na hata benchi la ufundi lina makocha wenye viwango walikini inashindwa kuchukua ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya ambao kila mwaka inaishia njiani.

Wachezaji, makocha, mashabiki na viongozi ambao wamewekeza pesa kwa ajili ya kuiona Namungo inapanda Ligi Kuu wanatakiwa kujiandaa kisaikolojia kwa kuamini chochote kinaweza kutokea.

Wanatakiwa wawe na moyo kama wa PSG ya Ufaransa inayotaka taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya. Wanatakiwa wawe na moyo kama wa Dodoma FC ambayo imekubali matokeo na kujipanga upya msimu huu.

Hawatakiwi kuchanganyikiwa na kuanza kutafuta mchawi pindi timu yao ikishindwa kufanya vizuri.

Advertisement