TIMUA VUMBI : Mwandami, Sima pengine washindwa ama kuzidiwa

Thursday February 20 2020

Mwandami, Sima pengine washindwa ama kuzidiwa,SINGIDA United ,Ligi Kuu Bara,SIMBA VS YANGA,

 

By Mwanahiba Richard

SINGIDA United ya mjini Singida huu ni msimu wake wa tatu kushiriki Ligi Kuu Bara. Ni timu ambayo ilianza kwa mbwembwe ikijikusanyia kijiji cha wadhamini mpaka kuzitisha timu kongwe nchini, za Simba na Yanga.

Wadau wa soka waliisifia Singida United kwa udhamini waliokuwa wakiupata, walishangaa wakongwe Simba na Yanga kukosa wadhamini wengi kama ilivyokuwa kwa timu changa ya mjini Singida.

Uongozi wa klabu hiyo haukuchagua udhamini walikusanya ilimradi kila mmoja anatoa kile anachoona kifaa kuisaidia Singida United - maana ni timu nyingi zinakosa bahati ya kupata mdhamini hata mmoja tu, yaani hata yule wa kuwapa maji.

Katika kipindi hicho ilipopanda daraja ilisaji kwa mbwembwe, wachezaji wa kigeni kibao kiasi kiasi kwamba hata Simba na Yanga walikuwa hawaoni ndani. Singida walijiamini kwelikweli - tena vibaya mno.

Hakuna aliyepingana na maendeleo yaliyokuwa yanaonekana kuwekezwa ndani ya Singida United huku Mwigulu Nchemba wakati huyo akiwa ni Waziri wa Mambo ya Ndani, basi kila kitu kilienda mswano.

Mwigulu alianza kuonekana zaidi timu hiyo ilipopanda daraja ingawa ilidaiwa hata wakati ipo Ligi Daraja la Kwanza (FDL) alikuwa akiisaidia kimtindo. Naam! Wadau waliona mageuzi na ushindani wa soka la Bongo unaongezekana baada ya uwepo wa timu kama Azam FC ambayo inaongoza kwa uwekezaji nchini, ila waliamini kwamba kasi ya Singida United itazipa changamoto timu zingine.

Advertisement

Hata hivyo, msimu wa pili tu Singida ilianza kupoteana wale viongozi wao walioipigania timu hiyo kupanda daraja akina Yusuph Mwandani akiwa mwenyekiti wa klabu na Abdulrahiman Sima ambaye alikuwa katibu mkuu wakianza kukaa kando.

Mwandami na Sima walimezwa kabisa na uongozi chini ya kina Mwigulu na Festo Sanga ambao ndio wameonekana kila kitu kwa Singida United.

Viongozi hao wawili hadi sasa ni kama hawapo kabisa ndani ya timu na kama wapo, basi yamebaki majina na wanategeana kwenye uwajibikaji wakiichana timu waliyotumia nguvu na pesa nyingi kuipandisha pasipo msaada mkubwa wa viongozi waliowameza.

Sasa hivi Singida United ni kama imeshuka daraja, inashika nafasi ya 20 yaani mkiani kabisa ikiwa na pointi 11, imecheza mechi 23. Inasikitisha.

Singida United haina wapiganaji ingawa kuna timu zingine nazo zipo kwenye hatari kama wao ikiwemo Mwadui FC - timu inayomilikiwa na mgodi wa Mwadui Gold Mine, Mbeya City - timu ya Halmashauri ya Jiji la Mbeya, KMC inayomilikiwa na Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni na zingine kama Mbao FC na Ndanda FC ambazo zote ziko hatarini.

Mwandami na Sima hebu jitokezeni ipiganieni timu kwani kuzorotoka kwake kumechangiwa pia na mambo ya kuongoza timu katika mazingira yanayotajwa kuwa ya kisiasa.

Kwa viongozi waliopo kwa kuwa inaonekana ni kama imewashinda, huu ni mpira wapeni timu wanaojua soka ambao wana uchungu na soka na sio ilimradi kiongozi aongoze kwa kutaka sifa ama kuwa njia yake ya kupitia kwenye mambo yake, timu imeathirika na itaharibikiwa zaidi.

Nadhani kuna haja ya viongozi wengine ndani ya Singida United kubaki kama viongozi wa kutoa tu ushauri, lakini sio suala la utekelezaji, hilo lifanywe na watu wanaoujua mpira na wana uchungu nao.

Endapo Singida United itashuka daraja na kushiriki Ligi Daraja la Kwanza (FDL), kwa hakika watakaoanza kuipigania tena kuipandisha ni Sima na Mwandani, na mambo yakiwa mazuri ndipo tutawasikia wengine wakijitokeza hata kama siyo hawa waliojitokeza ilipopanda daraja awamu hii. Raha ya soka ni kuwa na timu yenye ushindani kuanzia ndani ya kikosi chenyewe ndipo kwenye timu pinzani. Kwa hakika hili halipo ndani ya Singida iliyoonekana msimu wa kwanza.

Singida sasa ni timu iliyojaa madeni, yapo wazi maana yalitangazwa kabisa mpaka TRA nao waliwapelekea deni lao huku wachezaji wakilalamika kutolipwa stahiki zao. Ni msongo wa mawazo, sidhani hata kama wachezaji wana morali ya kuipambania isishuke.

Ni wakati sasa kabla ya mambo yote kufanyika timu ingerudishwa tu kwa wananchi kama ilivyokuwa mwanzo kabla haijabadilishwa kuwa kampuni, maana hili lilifanyika kwa mbwembwe kubwa mara tu baada ya kupanda daraja na kubadilisha mfumo wa uendeshaji ambao haujawasaidia kwa lolote.

Kwa hali iliyopo ndani ya Singida United basi inaonyesha kwamba kama Mwandami na Sima timu iliwashinda kuongoza, basi walizidiwa nguvu na wale wasioujua soka.

Soka linapochezwa vizuri na kuwafurahisha mashabiki ni wazi kwamba watu wataipenda timu na hata kuichangia inakuwa rahisi.

Advertisement