TIMUA VUMBI : Lyon isiifanye Ligi Kuu kama kikombe cha kahawa

Muktasari:

  • Ingawa mchezo wa soka umekuwa na matokeo ya kushangaza, Lyon inaweza kubakia katika Ligi Kuu. Kwa uhalisia nafasi yake kufanya hivyo ni finyu kulingana na ushindani uliopo kwenye Ligi Kuu msimu huu.

AFRICAN Lyon ipo katika nafasi mbaya katika msimamo wa Ligi Kuu Bara. Inashika mkia ikiwa na pointi zake 22 ilizozipata baada ya kuibuka na ushindi kwenye michezo minne tu, kutoka sare 10 na kupoteza 17. Hali ni mbaya kwelikweli.

Ikiwa mkiani mwa msimamo wa ligi, Lyon imezidiwa pointi nane na timu iliyo juu yake ambayo iko nafasi ya 19 kwenye msimamo wa ligi, ambayo ni Biashara United kutoka mkoani Mara. Hawa wamepanda msimu huu na kuna hatari kubwa wanaweza kurudi walikotoka kama mambo yasipobadilika.

Ikumbukwe kuwa kanuni za Ligi Kuu Bara msimu huu zinafafanua kuwa timu mbili zinazoshika mkia zinashuka moja kwa moja wakati timu mbili zitakazoshika nafasi ya 18 na 17 zitacheza mechi dhidi ya timu mbili za Ligi Daraja la Kwanza kusaka nafasi mbili za kucheza Ligi Kuu msimu ujao.

Kwa maana hiyo kwa idadi ya mechi ambazo imebakiza kabla ya ligi kumalizika, African Lyon ina mlima mrefu wa kupanda ili ikwepe rungu la kushuka daraja msimu ujao.

Ingawa mchezo wa soka umekuwa na matokeo ya kushangaza, Lyon inaweza kubakia katika Ligi Kuu. Kwa uhalisia nafasi yake kufanya hivyo ni finyu kulingana na ushindani uliopo kwenye Ligi Kuu msimu huu.

Na kwa bahati mbaya kadiri ambavyo ligi imekuwa ikiendea African Lyon imekuwa ikizidi kufanya vibaya na haionyeshi dalili zozote kama inaweza kujinusuru na balaa linaloinyemelea.

Ikiwa Lyon itashuka daraja, itakuwa ni mwendelezo wa rekodi zake zisizovutia za kushindwa kudumu kwenye Ligi Kuu kwa angalau hata kwa misimu miwili kwani kila mara imekuwa ikipanda na kushuka msimu unaofuata.

Ni timu ambayo imekuwa haionyeshi ushindani kwenye ligi na imekuwa msindikizaji mara kwa mara.

Na hilo linajidhihirisa kupitia pointi zake 22 ilizonazo kwani zinailazimisha kuziombea timu zilizo juu yake zipoteze angalau mechi nne mfululizo na yenyewe ishinde idadi kama hiyo ya michezo ili ijiondoe kwenye janga la kushuka daraja.

Lakini ukijaribu kuifuatilia kwa ukaribu African Lyon, utabaini matokeo ambayo imekuwa ikiyapata kwenye ligi ni matunda ya mbegu ambazo huwa inazipanda kabla ya kuanza kwa msimu katika suala zima la upande wa ufundi na utawala.

Kosa la kwanza ambalo limekuwa likiigharimu Lyon ni namna ya usukaji wa kikosi chake ambapo imekuwa ikisajili wachezaji kwa kuwakusanya pamoja na kuwafanyisha majaribio.

Lyon imekuwa ikilenga kuwapata wachezaji wale wa gharama nafuu jambo linalosababisha iwe na wachezaji wa kawaida ambao wanashindwa kuipatia timu kile kilicho bora huku wengine wakiwa hawana uzoefu.

Lakini udhaifu mwingine wa Lyon ni wachezaji kutopata huduma na stahiki kama posho na mishahara jambo ambalo limekuwa likishusha morali ya nyota wa kikosi chake.

Pamoja na hayo kingine kinachoiangusha African Lyon ni kukosa maandalizi mazuri ya kiufundi mwanzoni mwa msimu (Pre Season) .

Mambo hayo yanaifana timu kukosa muunganiko kwa kuchelewa kuingia kambini hali inayosababisha wachezaji wasiwe fiti kiasi cha kuweza kuhimili ushindani wa ligi.

Lakini haya yote yanamezwa na sababu moja kubwa ambayo ni viongozi kushindwa kutimiza majukumu hasa kutafuta vyanzo vya mapato ili waweze kujiendesha na kugharamia mahitaji muhimu.

Kufanya vibaya kwa African Lyon kila msimu, kunapaswa kuzifungua macho na kuwa darasa kwa klabu zetu nyingine ziwe zinafanya maandalizi mazuri kabla ya kupanda Ligi Kuu.

Zikiendelea kuishi kwa njia hii ambayo African Lyon inatumia, ni wazi zitaishia kuwa wasindikizaji kila uchao na zitaigeuza Ligi Kuu kama kijiwe cha kahawa ambacho mtu akishakunywa anaweza kuondoka muda wowote kwasababu ameshambaliza mahitaji yake.