TIMUA VUMBI : Ipo siku Azam FC itavuna inachopanda sasa

Muktasari:

Ukweli unauma, ila ndio hakuna namna. Benchi la ufundi na wamiliki wa timu hiyo wanapaswa kuondoa matabaka ndani ya timu ambapo wengine wanaonekana ni wachezaji wa wamiliki wa klabu na wengine wapo tu kutokana na viwango vyao wanavyoonyesha dimbani.

HAKUNA ubishi kwamba Klabu ya Azam FC ndio pekee kati ya 20 zinazoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara ambayo imewekeza kwa kiasi kikubwa kuliko klabu yoyote.

Ni klabu ambayo ina kila kitu kinachotakiwa kwenye soka japokuwa si kongwe kama zilivyo Simba na Yanga, ambazo zina zaidi ya nusu karne tangu zilipoanzishwa.

Katika mafanikio yao, Azam FC wamewahi kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu, Kombe la Shirikisho, Kombe la Mapinduzi na Kombe la Kagame linaloshirikisha vilabu kutoka kanda ya Afrika Mashariki. Kwa ufupi imeonja makombe yote muhimu.

Pamoja na mafanikio na uwekezaji wote huo bado kuna mambo yanaonekana ndani ya Azam FC kuwa hayajakaa sawa.

Waswahili wanasema lisemwalo lipo na kama halipo basi linakuja, labda lizuiwe kwa haraka kabla mambo hayajaharibika au kutokea.

Kinachoonekana ni kuwa, upande wa wachezaji hali haipo shwari kama inavyotazamwa kwa nje, kwani kuna madai kuwa ndani ya kikosi hicho kuna matabaka baina ya wachezaji kwa wachezaji.

Ukweli unauma, ila ndio hakuna namna. Benchi la ufundi na wamiliki wa timu hiyo wanapaswa kuondoa matabaka ndani ya timu ambapo wengine wanaonekana ni wachezaji wa wamiliki wa klabu na wengine wapo tu kutokana na viwango vyao wanavyoonyesha dimbani.

Hilo ni suala baya kwani linaleta mpasuko kwenye timu na kamwe timu haiwezi kufanya vyema. Hali kama hii inayoendelea ndani ya Azam FC inanikumbusha miaka kadhaa ndani ya Simba ambapo baadhi ya wachezaji walitengenezewa ufalme.

Ufalme huo uliitesa sana timu kwani wale ambao walionekana kuwa kama watoto yatima hawakuwa na ushirikiano na wale ‘wafalme’ hata uwanjani ushirikiano wao ulikuwa mdogo sana.

Matokeo yake Simba wachezaji walikuwa waliamua leo tuipe matokeo timu ama tujishushe viwango, kisa tu wengine walilelewa vizuri tena bila vificho huku wengine wakitaabika.

Ishukuriwe Simba ni klabu ambayo viongozi wake kipindi hicho walielewa haraka hasa pale ambapo walipogundua kuna tatizo kwa wachezaji na mambo yanaharibika, walianza kutafuta chanzo na hatimaye kukifanyia kazi haraka.

Ufalme ndani ya Simba ulizikwa haraka baada ya kuliachia majukumu mengi benchi la ufundi.

Na ni kitu ambacho sasa kimehamia upande wa Azam FC, kuna wafalme wa timu ambao hawataki kuguswa na wanaonyesha wazi ufalme wao, kisa walio nyuma yao wana nguvu kubwa kwenye timu.

Kiukweli hii itasababisha hata kuyumbisha benchi la ufundi ambalo ni wazi litaanza kufanya kazi kwa uoga na maelekezo kutoka juu pasipo kujali kiwango cha mchezaji, ila atapangwa tu kwa sababu watapokea amri ya kwamba ni lazima fulani acheze.

Azam kiukweli haijafikia hatua hiyo ya kuwa na wafalme ndani ya timu, wachezaji wote wanapaswa kuonekana wapo sawa labda tu kwa kuzidiana umri wanapaswa waheshimiane kwa kila mmoja.

Benchi la ufundi nalo linapaswa kuondoa uoga, wafanye kazi yao kulingana na taaluma ingawa inasemekana kwamba kwa timu za Tanzania jambo hilo ni gumu, ila makocha wakiamua wanaweza kutokomeza kwa kuwafanya wachezaji wote kuwa sawa.

Mwenye uwezo na kufanya vizuri mazoezini ni vyema apangwe na si kuangalia huyu kaletwa na nani ama kupokea maagizo kutoka juu.

Inasikitisha kusikia kwamba kuna baadhi ya wachezaji ndani ya timu hiyo hawazungumzi.

Hata katika kufanya kwangu uchunguzi nimethibitisha hivyo, sasa hii haileta afya ndani ya klabu hiyo inayoaminika kwamba italeta mapinduzi katika nyanja ya soka.

Umoja ndani ya Azam FC unaweza kupoteza ile ‘team work’ kwani itatoweka ghafla.

Na kutokana na baadhi ya wachezaji kubebwa na watu fulani, basi unakuwa ni mwanzo wa nidhamu kushuka kwenye timu - nidhamu ikishuka kila mmoja atafanya kile anachoona kinafaa na matokeo yake kutakuwepo na anguko la Azam FC.

Timu hii tunayoitazama kwa nje basi iendane na ile tuifikiriayo kwa ndani, klabu iendeshwe kwa weledi na si kubebana hata kama wachezaji hawana viwango.

Ni vyema benchi la ufundi liachwe lifanye kazi yake, mambo ya kuangalia huyu anasimamiwa na nani ili apangwe muda mwingine yanaharibu mipango ya timu.

Ni wakati wa kumuacha kocha afanye kazi yake ili akiharibu zigo la lawama libaki kuwa lake mwenyewe.

Sasa hivi kocha anaweza kuangushiwa zigo la lawama, lakini wakati tatizo linajulikana lilipoanzia.

Nachoshauri ni kuwa, ni wakati sasa mabadiliko yaanze ili kufikia malengo ya timu, vinginevyo uwekezaji wenu hautakuwa na maana na kuuacha ufalme ubaki mikononi mwa timu za Simba na Yanga.

Ni vyema uongozi wa Azam FC ukafahamu kuwa, mwanzo mzuri wa timu hii ulizitikisa sana timu hizi mbili kongwe na kuzifanya zionekane kuwa zipozipo, lakini iwapo wataruhusu hali ya kutofurahisha klabuni, basi ni wazi kwamba kutakuwepo na hali ya hamkani kimkakati na matokeo yake ni kuwa, Azam FC inaweza kuziacha Simba na Yanga zikaendelea kujiona bab’kubwa.