TIMUA VUMBI : Hii Simba isiwe ya majaribio, umakini unatakiwa

Thursday January 24 2019

 

By Mwanahiba Richard

MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Bara, Simba ni miongoni mwa timu bora kabisa kwenye ligi. Ni miongoni mwa timu inayotumia pesa nyingi sana kwenye ligi na ina wachezaji wazuri, huku pia ikiwa na kikosi kipana.

Kikosi hicho chenye uwekezaji mkubwa wa fedha sasa kinashiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na tayari wamecheza mechi mbili, waliifunga JS Saoura nyumba mabao 3-0 na kuchezea kichapo cha mabao 5-0 RD Congo dhidi ya AS Vita sasa wanajiandaa kwenda Misri kucheza na Al Ahly.

Hatua hiyo ya Simba ni kubwa ukilinganisha na jinsi ushiriki wa timu za Tanzania kwenye michuano hiyo mikubwa kwani ni zaidi ya miaka 10 tangu Tanzania ifike hatua kubwa kama hiyo kwa upande wa klabu.

Hata hivyo, Waswahili wanasema hakuna jambo zuri lisilo na kasoro ni hivyo hivyo hata kwa Simba pamoja na ubora wao waliouwekeza kwa mamilioni ya pesa bado wana mapungufu ambayo wanapaswa kuyaona kwa jicho lingine.

Kongole kwa malengo yao ya awali ya kudhamiria wanafika hatua hiyo ya makundi, hilo wamefanikiwa na sasa wanajaribu kupambana ili kufikia hatua nyingine ya robo fainali, hamu hii imeingilia kati ila hayakuwa malengo yao, hivyo lolote kwao linaweza kuwa sahihi kufanikiwa ama kutofanikiwa.

Lakini pamoja na hayo yote, wakati wa usajili wa dirisha dogo, Kocha Patrick Aussems alihitaji asajiliwe mchezaji wa haraka baada ya kutokea na dharura ya kuumia kwa beki wao Shomary Kapombe ndipo alipoletwa Zana Coulibaly kutoka Ivory Coast ikielezwa ndiye mbadala wa Kapombe.

Aisee, Mungu amjaalie Kapombe afya njema kwani mbadala wake ni wazi hata theluthi yake hajafikia ingawa ilielezwa kocha ameridhishwa na kiwango chake ndiyo maana wamempa mkataba huo wa miezi sita, ila hata zile mechi tu alizocheza za ndani ikiwemo michuano ya Kombe la Mapinduzi bado kiwango chake hakijashawishi.

Kutokushawishi kwa kiwango cha Zana sasa kunawafanya viongozi wa Simba kuanza kuhangaika kutafuta wachezaji wengine ambao wapo huru ili pengine wawasajili kwa ajili ya michuano ya Ligi ya Mabingwa maana ni wazi Zana hawezi kuongezwa kwenye usajili huo kwani Simba inahitaji mafanikio makubwa zaidi ya hayo waliyoyafanya.

Hivi sasa kuna wachezaji wawili ambao walianza mazoezi kwa ajili ya majaribio chini ya Aussems ambao ni Moro Lamine kutoka Ghana ambaye ni beki wa kati na Chunlede Kissimbo Ayi wa Togo huyu ni straika ingawa kuna taarifa kuna mshambuliaji mwingine kutoka Namibia, wote hao wapo kwenye majaribio.

Inawezekana ni wazuri na pengine Simba wameshindwa kuwapata wachezaji ambao hawajacheza michuano hii kama wanataka kusajili kwa ajili ya Ligi ya Mabingwa na sheria inawabana mchezaji anayesajiliwa na klabu ili acheze michuano hiyo basi awe yule ambaye hajacheza kwa wakati huo.

Mchezaji ambaye anaruhusiwa kucheza akisajiliwa ni yule mchezaji huru ama ambaye jina lake halijapelekwa Caf ikiwa na maana hajacheza kabisa, waliokuja kwenye majaribio Simba ni wachezaji huru ila bado haijafahamika kama huo kwao hawajacheza ligi zao ama mashindano yoyote kwa muda gani.

Zana inajulikana hakucheza mashindano yoyote kwa miezi mitano hadi alipokuja Simba, na ilitegemewa kabisa kwamba dirisha la usajili wa Caf lilipofunguliwa angeongezwa kikosini lakini malengo yamekuwa tofauti.

Simba wanapaswa kuwa makini kwenye usajili wao kama kweli wanahitaji kufika mbali zaidi ya hapa na pesa wanayopanga kuitumia kwa kipindi chote cha mafanikio, ni bora wasajili mchezaji mmoja kwa gharama kubwa lakini mwenye uwezo mkubwa na anacheza huko na yule ambaye yupo kwenye timu yake ya Taifa ili aingine kikosini moja kwa moja.

Inasikitisha zaidi kuona Simba hii bado itaendelea kujaribu jaribu wachezaji, Zana iwe shule tosha kwao kwa kuongeza umakini na kufanya uchunguzi zaidi wa kupata wachezaji bora watakaoendana na kasi ya Simba.

Advertisement