TIMUA VUMBI : Hata wanachama wajipime kuchagua viongozi

Muktasari:

  • Wanachama wamekuwa na maamuzi ya kuwagharimu mara nyingi, hatima yake huishia kwenye malalamiko, manung’uniko na majuto yasiyokuwa na ufumbuzi.

MARA nyingi wanachama wa klabu za soka hapa nchini huwa hawajipimi kiundani zaidi katika kuamua jambo lao liwe muhimu sana ama la kawaida, sio mara moja ama mara mbili wanachama wanaamua kufanya jambo halafu baadaye wanajutia wenyewe kwa maamuzi yao.

Wanachama wamekuwa na maamuzi ya kuwagharimu mara nyingi, hatima yake huishia kwenye malalamiko, manung’uniko na majuto yasiyokuwa na ufumbuzi.

Hivi sasa klabu kongwe ya Simba itafanya Uchaguzi Mkuu wa kupata viongozi, wanachagua Mwenyekiti na Wajumbe sita akiwemo mwanamke mmoja. Wajumbe hawa saba wataingia kwenye Bodi ya Wakurugenzi ambapo watawawakilisha wanachama kwa upande wa klabu.

Kwa mujibu wa Katiba yao hawatakuwa na mamlaka makubwa sana kama itakavyokuwa upande wa pili wa Mwekezaji ambaye naye anaingiza wajumbe saba ingawa upande huu watakuwa nane pamoja na Mwenyekiti wao ambaye anamiliki hisa asilimia 49.

Kwa kanuni za makampuni, mtu anayemiliki hisa nyingi ndiye mwenye nguvu ya kutoa maamuzi yote, nadhani hilo hata wanachama wa Simba wanalitambua kama kweli somo la hisa liliwaingia ama wanalifahamu.

Uchaguzi huo utakaowaweka madaraka viongozi hao kwa akipindi cha miaka minne utafanyika Novemba 4, Jumapili ya wiki hii jijini Dar es Salaam ambapo utatanguliwa na Mkutano Mkuu wa wanachama ambao kikawaida unafanyika mara moja kwa mwaka.

Wagombe nafasi ya ujumbe wapo 17 na Mwenyekiti mmoja, Swedy Mkwabi ambaye ni mgombea pekee baada ya mgombea mwenza Mtemi Ramdhani kusoma alama za nyakati na kuamua kukaa pembeni.

Uwepo wa Mkwabi kwenye kinyang’anyiro hicho akiwa mgombea pekee haumaanishi kwamba amepita moja kwa moja, kwani ili apite analazimika apate kura alisimia 50+1 na si vinginevyo, hivyo bado uchaguzi huo upande wake ni mgumu.

Wanachama wa Simba ndiyo wenye nguvu ya kuamua nani awaongoeze kwa kipindi hicho kwani wao ndiyo wanaopiga kura za ndiyo ama hapana ndani ya kisanduku cha kura ambacho ni siri baina na kisanduku na mpira kura.

Hivi sasa wagombea wanaendelea na kampeni zao, ni kampeni za waziwazi na zenye utulivu ingawa mihemko kwa baadhi ya wagombe na wanachama ikiwemo kwa asilimia ndogo sana, waliowengi wana utulivu mkubwa.

Utulivu huu haumaanishi kwamba wote wanaoenda kupiga kura wanaelewa nani anafaa kuwawakilisha kwenye Bodi hiyo, laa! h hasha, wengine wametulia na kusubiri liende na kumalizika.

Jambo hili la uchaguzi ni zito na nyeti, ikiwa na maana kwamba wapiga kura wanatakiwa kuwa makini na kile wanachokwenda kukifanya siku hiyo ndani ya masanduku ya kura, kwani kukosea kuchagua viongozi bora ndiko kunakopelekea kuwa na majuto makubwa hapo baadaye.

Majuto hayo husababishwa kwa asilimia kubwa na nyie wanachama ambao wanakosa kuchanganua akili zao na kuchagua kiongozi bora wa kuwaongoza kwa kipindi hicho ambaye atasimamia maslahi ya klabu na mambo mengine yanayopaswa kufanyika ndani ya klabu hiyo inayohitaji mafanikio makubwa.

Wanachama wamekuwa wakiwalalamikia viongozi wao kwa utendaji mbovu wa kazi ama yale waliyoyaahidi walipokuwa wakiomba kura lakini chanzo cha hayo yote ni wanachama wenyewe ambao wanashindwa kupima hoja za wagombea wanapoomba kura zao, wao hurubuniwa na vitu vidogo tu vyenye majuto makubwa baadaye.

Hivyo kuelekea uchaguzi huo, wanachama mnapaswa kujithamini na kujipima weledi wao wanapokwenda kufanya maamuzi muhimu kama hayo. Kupiga kura ni jambo siri kubwa kwa kila mmoja lakini ndio hubeba maisha ya timu hiyo kwa namna mtakavyokubwali kuwachagua viongozi mtakaokubali waweze kuwaongoza na hata yale watakayoyafanya ina maana ndio limefanyika na Wanasimba wote bila kujali nani kafanya kwa manufaa yapi aliamua kufanya.

Nawatakia uchaguzi mwema utakaozaa matunda bora ndani ya Klabu ya Simba.